Sunday, July 12, 2015

Kesho Naanza Tena Kufundisha

Hiki ni kipindi cha kiangazi, ambacho kwa ki-Ingereza huitwa "summer." Katika chuo chetu cha St.Olaf, walimu hatuwajibiki kufundisha kipindi hiki, ambacho hudumu karibu miezi minne. Ila kama mwalimu anapenda, anaweza kufundisha. Kozi za kipindi hiki cha kiangazi hudumu wiki yapata tano, lakini kozi inafanana kwa uzito wake sawa na kozi za muhula wa kawaida.

Kwa miaka niliyofundisha hapa, mara kwa mara nimefundisha kozi wakati wa kiangazi. Uzuri wake mojawapo ni kuwa wanafunzi huwa wachache, na kwetu tunaofundisha fasihi, ni wakati mzuri wa kujaribisha vitabu vipya. Kozi ambayo nitafundisha kipindi hiki ni fasihi ya Afrika (African Literature).  Nitatumia vitabu kutoka sehemu mbali mbali za Afrika.

Kitabu kimojawapo ni Minaret, ambayo ni riwaya ya Leila Aboulela wa Sudan. Nilifundisha riwaya hii muhula uliopita, na iliwavutia wanafunzi na mimi pia. Ingawa ni hadithi ya kubuniwa inatupa picha nzuri ya maisha ya watu wa Khartoum, ambao ni wa-Islam wa tabaka la juu, si walalahoi. Wanafunzi wangu walishukuru kusoma riwaya hii kwa vile iliwapa fursa ya kuielewa angalau misingi ya u-Islam. Kutokana na jinsi tulivyopendezwa na riwaya hii, niliamua kuifundisha tena, na ninapangia kufundisha riwaya zingine za Leila Aboulela siku za usoni, panapo majaliwa.

Kitabu kingine ni The Thing Around Your Neck, ambacho ni mkusanyo wa hadithi za Chimamanda Ngozi Adichie wa Nigeria. Huyu ni mwandishi ambaye ametukuka miaka ya karibuni na anasifika sana. Nimefundisha kazi zake kadhaa: Purple Hibiscus, Half of a Yellow Sun, na Americanah. Ni mwandishi mwenye kipaji sana, ingawa ni mdogo kwa umri.

Nitafundisha pia tamthilia mbili za Ama Ata Aidoo wa Ghana: The Dilemma of a Ghost and Anowa. Aidoo ni mwandishi mkongwe, ambaye alianza kujipatia umaarufu kimataifa miaka ya sitini na kitu kwa tamthilia na hadithi fupi, na hatimaye riwaya. Nimefundisha baadhi ya kazi zake. Nimefundisha The Dilemma of a Ghost mara kadhaa.

Kitabu kingine nitakachofundisha ni The Tuner of Silences, ambayo ni riwaya ya Mia Couto wa Msumbiji. Sijawahi kusoma chochote alichoandika mwandishi huyu, lakini ninajua kuwa ni maarufu. Kwa hivyo, niliona nijiongezee ufahamu wangu sambamba na kufundisha kazi ya fasihi kutoka katika lugha ambayo si ya ki-Ingereza. Riwaya hii imetafsiriwa kutoka k-Reno. Ingawa katika idara yetu ya ki-ingereza hapa chuoni St. Olaf tunapendelea kufundisha kazi zilizoandikwa kwa ki-ingereza, tunaona si vibaya mara moja moja kufundisha kazi zilizotafsiriwa kwa Ki-Ingereza.

Nitafundisha pia tamthilia ya Athol Fugard iitwayo Valley Song. Huyu ni mwanatamthilia maarufu wa Afrika Kusini, ambaye tamthilia zake kadhaa nimewahi kufundisha. Mifano ni Master Harold and the Boys, A Lesson From Aloes, na Sorrows and Rejoicings. Nimefundisha Sorrows and Rejoicings mara kadhaa, na kila mara nazidi kuguswa upya.

Kitabu cha sita ni The Beautiful Things That Heaven Bears, ambayo ni riwaya ya Dinaw Mengestu, mwandishi chipukizi wa Ethiopia. Sijawahi kusoma kazi yoyote ya mwandishi huyu, ila najua kuwa tayari ameshajijengea sifa. Nimeanza kusoma hii riwaya yake na ninaiona ni yenye mvuto mkubwa kwa jinsi inavyoelezea maisha ya vijana wa ki-Afrika hapa Marekani. Hii ni dhamira moja muhimu katika riwaya ya Americanah ya Chimamanda Ngozi Adichie, ambaye nimemtaja hapo juu.2 comments:

NN Mhango said...

Kaka nakutakia ufundishaji mwema hasa wakati huu wa kiangazi ambapo wengi wa walimu hutumia kwenda kujipumzisha mbali. Nami kiangazi hiki nimekitumia kumalizia miswada yangu mitatu ambayo nimeishawasilisha kwa wachapishaji. Mswada wa mwisho wa BORN WITH VOICE niliuwasilisha jana tu wakati nikiendelea na mwingine.
Kimsingi, ni bora kuchapa kazi wakati bado una nguvu ili ukistaafu upate vitu vya kukushghulisha kama kurejea baadhi ya kazi zako na kujikosoa na kujisoma.

mandela pallangyo said...

Kila la kheri mwl