Showing posts with label Ama Ata Aidoo.. Show all posts
Showing posts with label Ama Ata Aidoo.. Show all posts

Thursday, March 16, 2017

Nimenunua "Two Thousand Seasons" (Ayi Kwei Armah)

Leo nilienda St. Paul, na wakati wa kurudi, nilipitia Apple Valley kuangalia vitabu katika duka la Half Price Books, kama ilivyo kawaida yangu. Hilo duka lina maelfu ya vitabu, na wateja wanapishana humo tangu asubuhi hadi jioni.

Kila ninapoingia katika duka la vitabu, ninajikuta nikianza kuangalia kama kuna vitabu vipya juu ya mwandishi Ernest Hemingway. Leo sikuona kitabu kipya juu ya Hemingway, nikaenda sehemu nyingine humo dukani, kwenye kona kabisa, ambapo sikosi kupitia.

Hapo, katikati ya msitu wa vitabu, niliona kitabu cha Ayi Kwei Armah, Two Thousand Seasons. Sikutegemea kukuta kitabu cha Armah. Nilikichukua hima, huku nikikumbuka enzi za ujana wangu Tanzania, kwani ni wakati ule ndipo nilianza kusikia habari za Ayi Kwei Armah.

Tangu nikiwa mwanafunzi sekondari, nilikuwa nafuatilia sana fasihi ya ki-Ingereza. Somo la fasihi ni somo nililolipenda na kuliweza sana. Nilipoingia Chuo kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1973, ndipo nilipofahamu kuwa Ayi Kwei Armah alikuwa anaishi Dar es Salaam. Alikuwa anafundisha chuo cha ualimu Chang'ombe, lakini tulishangaa kwa jinsi alivyokuwa hatumwoni kokote, hata chuo kikuu. Tulitegemea angejihusisha na chuo kikuu, lakini sidhani kama aliwahi hata kukanyaga pale.

Jambo hilo lilitushangaza, hasa kwa kuzingatia umaarufu wake kama mwandishi katika Afrika na ulimwenguni. Tulisoma riwaya yake, The Beautyful Ones Are Not Yet Born, na mimi binafsi nilisoma pia Fragments, Why are we So Blest?, na Two Thousand Seasons. Ayi Kwei Armah tulimfahamu pia kutokana na insha yake, "African Socialism: Utopian or Scientific?"

Nilijua tangu wakati ule kuwa wahakiki walikuwa wanalumbana kuhusu uandishi wa Armah. Baadhi walilalamika jinsi anavyoielezea Ghana katika The Beautyful Ones Are Not Yet Born. Anaelezea uozo wa kina namna. Wahakiki na wasomaji walishangaa kwa nini aliamua kuanika uozo huo machoni pa ulimwengu.

Two Thousand Seasons inahusu biashara ya utumwa iliyosababisha mamilioni ya wa-Afrika kupelekwa bara la Amerika kama watumwa. Armah kwa kushughulikia mada hii, alikuwa anaendeleza jadi ya waandishi wenzake wa Ghana, kama vile Ama Ata Aidoo katika tamthilia zake mbili: Dilemma of a Ghost na Anowa.

Tuesday, September 20, 2016

"The Dilemma of a Ghost:" Tamthilia ya Ama Ata Aidoo

The Dilemma of a Ghost ni tamthilia ya kwanza ya Ama Ata Aidoo wa Ghana. Aliitunga alipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Ghana, Legon, ikaonyeshwa mara ya kwanza mwaka 1964, na kuchapishwa mwaka 1965. Ama Ata Aidoo aliendelea kuandika na bado anaandika, na kazi zake ni pamoja na tamthilia nyingine iitwayo Anowa, ambayo ilichapishwa mwaka 1970, hadithi fupi, na riwaya kadhaa.

The Dilemma of a Ghost inaongelea juu ya kijana wa Ghana aitwaye Ato aliyekwenda masomoni Marekani na huko akakutana na Eulalie, binti Mwamerika Mweusi. Huyu ni kati ya wale wa-Marekani Weusi wanaoiwazia Afrika kwa hamu kama mtu aliyeko ugenini anavyowazia nyumbani kwake.

Ato na Eulalie wanaoana na kurejea Ghana, ambako wanakumbana na mambo magumu. Kwanza ndugu zake Ato wanashtuka kusikia kuwa Ato ameoa bila kuwashirikisha. Halafu binti mwenyewe hana kabila wanalolitambua, na hata jina lake wanashindwa kulitamka, na kibaya zaidi, kwa mtazamo wao, ni kuwa binti huyo ni kizalia cha watumwa. Wanaukoo wanaona Ato amewasaliti.

Halafu, Eulalie naye anashindwa kuelewa na kufuata mila na desturi za hao ndugu. Wao wanamwona kama kizuka, kwa tabia zake, ikiwemo kukataa kunywesha dawa za kienyeji za kumwezesha kupata mimba. Mama mkwe wake, Esi Kom, anapofanya ukarimu wa kumletea konokono, ambao ni chakula cha heshima, Eulalie anashtuka, na haamini macho yake, na hatimaye anawatupilia mbali hao konokono. Jambo jingine linalowashangaza ndugu hao ni jinsi Eulalie anavyovuta sigara. Basi, inakuwa shida juu ya shida, na hatimaye binti anajikuta katika upweke na msongo wa mawazo.

Lakini, hatimaye, mama yake Ato anaridhia kumpokea huyu mkwe wake na anachukua hatua za kuwashawishi ndugu wote wampokee, kwa hoja kwamba mgeni hastahili kulaumiwa, bali mwenye lawama ni mwenyeji, yaani Ato. Ato anajikuta akiwa mpweke, aliyesongwa na mawazo, karibu kuchanganyikiwa. Ndivyo tamthilia inavyokwisha.

The Dilemma of a Ghost imejengeka katika mfumo wa hadithi za jadi ambazo huitwa "dilemma tales" ambao ni muundo unaowaacha wasikilizaji wakiwa na masuali yasiyojibika kirahisi. Katika tamthilia hii, suali moja muhimu ni nani wa kulaumiwa kwa matatizo yanayoibuka. Tamthilia hii inatumia pia aina nyingine za fasihi simulizi, kama vile nyimbo na methali. Vile vile kuna imani za jadi, kama vile juu ya mizimu na matambiko.

Ama Ata Aidoo ni mmoja wa waandishi wa ki-Afrika ambao ni hodari wa kutumia miundo na dhamira za masimulizi ya jadi. Hilo suala la kijana kujifanyia mwenyewe uamuzi wa kuoa au kuolewa bila kuwahusisha wazazi ni dhamira maarufu katika fasihi simulizi za Afrika, na matokeo ya kiburi hiki huwa si mema. Katika tamthilia ya Anowa, Ama Ata Aidoo ameiweka pia dhamira hiyo. Msichana Anowa anaamua kuolewa na kijana aliyemkuta bila wazazi kuhusika.

Tangu mwanzo, nilivutiwa na mtindo huu katika uandishi wa Ama Ata Aidoo, ambaye miaka ile alikuwa anajulikana kwa jina la Christina Ama Ata Aidoo. Ninakumbuka vizuri, kwa mfano, hadithi yake moja ya mwanzo kabisa iitwayo "In the Cutting of a Drink" ambayo niliisoma kwa mara ya kwanza miaka ya sitini na kitu, nilipokuwa mwanafunzi katika shule ya sekondari.

Nilivutiwa sana na hadithi hiyo kwa mtiririko wake sawa na wa mtambaji hadithi. Miaka ya baadaye, nilipojifunza somo la fasihi simulizi, nilianza kuelewa vizuri jinsi waandishi kama Ama Ata Aidoo wanavyotumia jadi hiyo.

Jambo muhimu sana jingine kuhusu Ama Ata Aidoo ni kuwa ni mwandishi mwenye kuchambua masuala ya jamii. Alivyokuwa anatunga The Dilemma of a Ghost, masuala kama ya mshikamano na mahusiano ya watu weusi ulimwenguni yaani "Pan-Africanism," yalikuwa yakivuma na kuwashughulisha viongozi maarufu kama George Padmore, W.B. Dubois, Kwame Nkrumah, Ahmed Sekou Toure, Jomo Kenyatta, na Julius Nyerere. Miaka iliyofuatia, Ama Ata Aidoo amekuwa akienda na wakati kama mwanaharakati katika masuala ya ukoloni mambo leo, haki za wanawake, na hata ujamaa. Sawa na ilivyokuwa kwa Mwalimu Julius Nyerere, Ama Ata Aidoo ni muumini wa fikra za kijamaa.

Saturday, September 3, 2016

Shakespeare Ametawala Mawazo Yangu Leo

Leo Shakespeare ametawala mawazo yangu, nami ninapenda kuelezea ilivyotokea. Ni maelezo yanayoweza kubainisha namna akili yangu inavyofanya kazi ninapohangaika kuandika makala ya kitaaluma.

Kwa miezi kadhaa, nimekuwa nikiwazia kuandika makala juu ya utangulizi wa The Dilemma of a Ghost, tamthilia ya Ama Ata Aidoo wa Ghana. Utangulizi huu umeitwa "Prelude" katika tamthilia hiyo, ambayo Ama Ata Aidoo aliitunga alipokuwa mwanafunzi wa chuo kikuu Ghana, Legon, ambapo alihitimu mwaka 1963. Tamthilia yake iliigizwa kwa mara ya kwanza mwaka 1964 na kuchapishwa mwaka 1965.

Nimefundisha tamthilia hii mara kadhaa, na kwa miezi kadhaa nimepata hamu ya kuchambua utangulizi wake, yaani "Prelude." Nimeona kwamba hakuna mhakiki yeyote ambaye ameichambua sehemu hii ya tamthilia hii kwa kiwango kinachoniridhisha. Hii "Prelude" si rahisi kuifafanua. Ninahisi hii ndio sababu ya wachambuzi kuiacha kando.

Katika kuitafakari hii "Prelude," nimeona kuwa ujuzi wangu wa taaluma ya "Folklore" utakuwa nyenzo muhimu. Vile vile, nimeona kuwa italazimu kugusia jadi ya tamthilia ya nchi za Magharibi kuanzia Ugriki ya zamani.

Ni katika kuwazia jadi hii ndio nikajikuta ninamkumbuka Shakespeare. Katika "Prelude" yake, Ama Ata Aidoo ametumia dondoo za lugha ambazo zinatupeleka kwa Shakespeare. Sishangai, nikizingatia kuwa Ama Ata Aidoo alisomea ki-Ingereza na fasihi katika mfumo wa elimu wa ukoloni wa ki-Ingereza. Kwa maana hiyo, Ama Ata Aidoo alilelewa katika mfumo ambao walilelewa waandishi wa enzi zake, na waliofuatia, kama vile Efua Sutherland, Wole Soyinka, na James Ngugi, ambaye baadaye alibadili jina na kujiita Ngugi wa Thion'go.

Baada ya kujiridhisha kwamba kuna athari za Shakespeare katika "Prelude" ya The Dilemma of a Ghost, ndipo nikawa nawazia kutafuta ushahidi katika tamthilia za Shakespeare. Kwa miezi yote hii, nilikuwa na uhakika kwamba baadhi ya athari zimetoka katika tamthilia kadhaa na pia mashairi ya Shakespeare, na baadhi ya athari nilihisi zilitokana na au tamthilia ya The Merchant of Venice au Hamlet.

Kwa hivi, leo nimeteremsha kabatini buku langu kubwa liitwalo The Yale Shakespeare, ambalo lina tamthilia zote za Shakespeare na mashairi yake yote. Kila tamthilia imetanguliwa na insha iliyoandikwa na mchambuzi mahiri na imeambatana na maelezo ya dhana, misemo na maneno ambayo watumiaji wa leo wa ki-Ingereza inaweza kuwawia vigumu kuelewa.

Kwa miezi kadhaa, kabla ya kuanza kufukuafukua maandishi ya Shakespeare leo, nimekuwa nikitafakari vipengele vya "Folklore" ambavyo ninavyoviona katika "Prelude." Pia nimekuwa nikitafiti zaidi vipengele hivyo, kwa kufuatilia maandishi ya wataalam kama William Bascom. Sina shaka kwamba tafakari hiyo na utafiti vitaniwezesha kuifafanua "Prelude" na matumizi ya "Folklore" katika tamthilia nzima ya The Dilemma of a Ghost.

Wednesday, July 20, 2016

Ki-Ingereza cha Shakespeare

Miaka mia nne imepita tangu alipofairki Walliam Shakespeare. Lakini dunia haiwezi kumsahau, kwa mchango wake uliotukuka katika utunzi wa tamthilia na mashairi. Leo, ninarejea tena kwenye mada hii ya mchango wa Shakespeare, ambayo nimekuwa nikiiongelea katika blogu hii. Napenda kujikumbusha suala la ki-Ingereza cha Shakespeare.

Kumbukumbu hii imenijia leo kwa sababu maalum. Leo, katika kozi yangu ya African Literature, nimeanza kufundisha The Dilemma of a Ghost, tamthilia ya Ama Ata Aidoo. Nimeongelea mistari nane ya mwanzo ya "Prologue," yaani utangulizi, nikataja mambo mengi, kuanzia "folklore" hadi tamthilia za Shakespeare. Mistari hiyo ni hii:

I am the Bird of the Wayside--
The sudden scampering in the undergrowth,
Or the trunkless head
Of the shadow in the corner.
I am the asthmatic old hag
Eternally breaking the nuts
Whose soup, alas,
Nourished a bundle of whitened bones--

Miaka yetu, tulipokuwa tunasoma sekondari,  ambayo kwangu ilikuwa ni 1967-70, tulisoma na kuelewa ki-Ingereza cha Shakespeare. Tulipokutana na maneno magumu au misemo isiyoeleweka, tulifuatilia hadi kuelewa. Aghalabu, maelezo yalikuwemo katika vitabu tulivyokuwa tunasoma. Vinginevyo, tuliangalia kamusi. Tulikuwa na tabia ya kujituma.

Utamu wa ki-Ingereza cha Shakespeare unaonekana katika maandishi yake yote. Humo tunaona nidhamu ya hali ya juu katika matumizi ya maneno na uundaji wa sentensi. Kila neno lina umuhimu, na limewekwa mahali panapostahili. Hakuna sehemu inayolegalega.

Kumsoma Shakespeare ni chemsha bongo. Ni kunoa akili, sio tu kutokana na namna Shakespeare anavyotumia lugha bali pia kutokana na ukweli kuwa Shakespeare ndiye aliyekuwa na msamiati mkubwa kuliko mtumiaji mwingine yeyote wa ki-Ingereza. Hapa naleta mfano kutoka katika tamthilia yake ya Hamlet, ambayo nimeikumbuka leo kwa namna ya pekee, ili angalau wale tuliosoma zamani tujikumbushe enzi zile, ambapo shule ilikuwa shule kweli:

ACT I SCENE III A room in Polonius' house.
[Enter LAERTES and OPHELIA]
LAERTESMy necessaries are embark'd: farewell:

And, sister, as the winds give benefit

And convoy is assistant, do not sleep,

But let me hear from you.
OPHELIADo you doubt that?
LAERTESFor Hamlet and the trifling of his favour,

Hold it a fashion and a toy in blood,

A violet in the youth of primy nature,

Forward, not permanent, sweet, not lasting,

The perfume and suppliance of a minute; No more.
OPHELIANo more but so?
LAERTESThink it no more;10

For nature, crescent, does not grow alone

In thews and bulk, but, as this temple waxes,

The inward service of the mind and soul

Grows wide withal. Perhaps he loves you now,

And now no soil nor cautel doth besmirch

The virtue of his will: but you must fear,

His greatness weigh'd, his will is not his own;

For he himself is subject to his birth:

He may not, as unvalued persons do,

Carve for himself; for on his choice depends20

The safety and health of this whole state;

And therefore must his choice be circumscribed

Unto the voice and yielding of that body

Whereof he is the head. Then if he says he loves you,

It fits your wisdom so far to believe it

As he in his particular act and place

May give his saying deed; which is no further

Than the main voice of Denmark goes withal.

Then weigh what loss your honour may sustain,

If with too credent ear you list his songs,30

Or lose your heart, or your chaste treasure open

To his unmaster'd importunity.

Fear it, Ophelia, fear it, my dear sister,

And keep you in the rear of your affection,

Out of the shot and danger of desire.

The chariest maid is prodigal enough,

If she unmask her beauty to the moon:

Virtue itself 'scapes not calumnious strokes:

The canker galls the infants of the spring,

Too oft before their buttons be disclosed,40

And in the morn and liquid dew of youth

Contagious blastments are most imminent.

Be wary then; best safety lies in fear:

Youth to itself rebels, though none else near.

Friday, July 17, 2015

Tumesoma "The Dilemma of a Ghost" na "Anowa"

Leo Ijumaa tumemaliza wiki ya kwanza ya muhula wa kiangazi. Tumesoma tamthilia mbili za Ama Ata Aidoo wa Ghana: The Dilemma of a Ghost na Anowa, ambazo ni miongoni mwa tamthilia maarufu za Afrika. Hata hivi, kama ilivyo kawaida yangu, nimewatahadharisha wanafunzi kuwa dhana ya kumaliza kusoma kazi ya fasihi ni dhana potofu. Haiwezekani kumaliza, kwa maana ya kuielewa kikamilifu hadi kikomo, hata tukiisoma tena na tena

Ninapenda kufundisha The Dilemma of a Ghost sio tu kwa kuwa ni kazi nzuri kisanaa, bali pia kwa namna inavyoyaanika masuala ya maisha. Mfano muhimu ni suala la mahusiano baina ya wa-Afrika na wa-Marekani Weusi. Msingi wa mahusiano hayo katika tamthilia hii ni ndoa baina ya kijana aitwaye Ato, kutoka Ghana, na Eulalie, mwanamke m-Marekani Mweusi.

Hao wawili wanakutana na kuoana wakiwa Marekani, ambako Ato alikuja kusoma. Eulalie, kama walivyo wa-Marekani Weusi wengi, anafurahi sana kwamba atakwenda Afrika, ambako ni asili ya watu wake. Ana imani kuwa atapokelewa kama mtoto wa nyumbani na atakuwa na maisha ya raha. Ato anachangia matumaini hayo kwa kumwelezea Eulalie mambo mazuri ya Afrika, pamoja na kutia chumvi.

Hali inakuwa tofauti baada ya wawili hao kufika nyumbani kwa Ato. Eulalie anakumbana na madharau kutoka kwa ndugu za Ato kwa kuwa ni kizalia cha watumwa. Tofauti za tamaduni zinachangia matatizo baina yake na ndugu hao.  Hali inaendelea kuwa mbaya na kumkosesha raha Eulalie hadi hatimaye mama mkwe wake anapoamua kurekebisha hali na kuufanya ukoo umkubali.

The Dilemma of a Ghost imesheheni matumizi ya fani ya fasihi simulizi, kama vile nyimbo na hadithi za mapokeo. Dhamira ya kijana kujifanyia uamuzi wake wa kuoa bila kuwashirikisha wanafamilia ni dhamira inayojitokeza katika hadithi nyingi za mapokeo za Afrika. Katika riwaya yake, The Palm Wine Drinkard,  Amos Tutuola aliweka hadithi ya "The Complete Gentleman" yenye muundo huo.

Matumizi ya fani ya fasihi simulizi yanajitokeza zaidi katika tamthilia ya Anowa. Humo tunashuhudia mambo yanayompata Anowa, msichana mzuri kuliko wote ambaye alikuwa anawakataa vijana wote waliokuwa wanamchumbia. Hatimaye anajichagulia mwenyewe kijana ambaye wazazi wake hawaridhiki naye. Yeye na mume wake wanahama nyumbani na kwenda mbali ambako wanajitafutia maisha. Hata hivi mwisho wao si mzuri.

Muundo wa hadithi ni ule unaofahamika katika hadithi za ki-Afrika na zinginezo ulimwenguni. Majivuno na ukaidi kwa wazee, wahenga, au miungu, hayana mwisho mwema. Wagriki wa kale walikuwa na dhana ya "hubris," kuielezea tabia hii. Waandishi kadhaa wa Afrika wametunga hadithi zenye dhamira hiyo. Mifano ni riwaya ya Things Fall Apart ya Chinua Achebe na riwaya ya Chaka ya Thomas Mofolo.

Kumalizia wiki hii ya kwanza, na ili kuwapa wanafunzi fursa ya kutafakari masuala muhimu, nimewapa jukumu la kuandika insha fupi moja kufuatana na maelekezo haya:

1) Discuss a female character in The Dilemma of a Ghost or Anowa.

2) Write about children in The Dilemma of a Ghost and Anowa.

3) Discuss the relationship between one couple--a man and a woman--in The Dilemma of a Ghost or Anowa.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...