Kwa miezi kadhaa, nimekuwa nikiwazia kuandika makala juu ya utangulizi wa The Dilemma of a Ghost, tamthilia ya Ama Ata Aidoo wa Ghana. Utangulizi huu umeitwa "Prelude" katika tamthilia hiyo, ambayo Ama Ata Aidoo aliitunga alipokuwa mwanafunzi wa chuo kikuu Ghana, Legon, ambapo alihitimu mwaka 1963. Tamthilia yake iliigizwa kwa mara ya kwanza mwaka 1964 na kuchapishwa mwaka 1965.
Nimefundisha tamthilia hii mara kadhaa, na kwa miezi kadhaa nimepata hamu ya kuchambua utangulizi wake, yaani "Prelude." Nimeona kwamba hakuna mhakiki yeyote ambaye ameichambua sehemu hii ya tamthilia hii kwa kiwango kinachoniridhisha. Hii "Prelude" si rahisi kuifafanua. Ninahisi hii ndio sababu ya wachambuzi kuiacha kando.
Ni katika kuwazia jadi hii ndio nikajikuta ninamkumbuka Shakespeare. Katika "Prelude" yake, Ama Ata Aidoo ametumia dondoo za lugha ambazo zinatupeleka kwa Shakespeare. Sishangai, nikizingatia kuwa Ama Ata Aidoo alisomea ki-Ingereza na fasihi katika mfumo wa elimu wa ukoloni wa ki-Ingereza. Kwa maana hiyo, Ama Ata Aidoo alilelewa katika mfumo ambao walilelewa waandishi wa enzi zake, na waliofuatia, kama vile Efua Sutherland, Wole Soyinka, na James Ngugi, ambaye baadaye alibadili jina na kujiita Ngugi wa Thion'go.
Baada ya kujiridhisha kwamba kuna athari za Shakespeare katika "Prelude" ya The Dilemma of a Ghost, ndipo nikawa nawazia kutafuta ushahidi katika tamthilia za Shakespeare. Kwa miezi yote hii, nilikuwa na uhakika kwamba baadhi ya athari zimetoka katika tamthilia kadhaa na pia mashairi ya Shakespeare, na baadhi ya athari nilihisi zilitokana na au tamthilia ya The Merchant of Venice au Hamlet.
Kwa miezi kadhaa, kabla ya kuanza kufukuafukua maandishi ya Shakespeare leo, nimekuwa nikitafakari vipengele vya "Folklore" ambavyo ninavyoviona katika "Prelude." Pia nimekuwa nikitafiti zaidi vipengele hivyo, kwa kufuatilia maandishi ya wataalam kama William Bascom. Sina shaka kwamba tafakari hiyo na utafiti vitaniwezesha kuifafanua "Prelude" na matumizi ya "Folklore" katika tamthilia nzima ya The Dilemma of a Ghost.
No comments:
Post a Comment