Thursday, September 29, 2016

Darasa ni Popote

Tangu nilipokuwa mdogo, nilikuwa nataka kuwa mwalimu. Mungu si Athmani, ndoto yangu ilitimia. Ninafurahia kazi yangu na ninaifanya kwa dhati na kwa uadilifu. Ninaona raha kuwa na wanafunzi katika kutafakari masuala.

Zaidi ya kufundisha darasani katika jengo, ninapenda kushiriki matamasha. Matamasha hayo ni kama shule, fursa ya kuongea na watu juu ya shughuli zangu, kama vile utafiti na uandishi.

Uandishi ninauchukulia kama aina ya ufundishaji. Ni ufundishaji usio na mipaka, kwani maandishi yanakwenda popote, iwe ni vitabu halisi au vitabu pepe, iwe ni makala katika majarida au mtandaoni,  zote hizo ni njia za kuniwezesha kufundisha bila mipaka.

Ninafurahi kuwa nimejiingiza katika uwanja wa blogu. Blogu ni kumbi zinazonipa fursa ya kueneza mawazo yangu, ingawa kwa ufupi. Mara kwa mara ninaongelea vitabu na kutoa dondoo za kiuchambuzi zinazoweza kumpa mtu fununu ya mambo muhimu yaliyomo katika vitabu hivyo. Blogu zangu zinatoa fursa kwa watu kuchangia mawazo na mitazamo. Ninaendesha blogu kwa mtindo huo kwa kuwa ninaheshimu uhuru wa fikra ambao ndiyo injini inayoendesha elimu.

Ni wazi kwamba tafsiri yangu ya shule au darasa ni tofauti na ilivyozoeleka. Tekinolojia za mawasiliano zimeleta mazingira na fursa mpya. Fikra zetu kuhusu darasa au shule sherti zibadilike. Katika mazingira ya leo, darasa au shule ni dhana isiyofungwa au kufungamana na kigezo cha jengo, madawati, au mwalimu na wanafunzi kuonana ana kwa ana.

Leo kwa kutumia tekinolojia za mawasiliano, mwalimu anaweza kuendesha darasa kwa njia ya Skype, kama nilivyowahi kufanya kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Montana, au anaweza kuendesha darasa mtandaoni na wanafunzi wakiwa wametapakaa sehemu mbali mbali za dunia. Ninategemea kuwa wa-Tanzania, wakiwemo wanaotaka nirudi Tanzania nikafundishe, watasoma na kutafakari hayo niliyoandika hapa.

No comments: