Friday, September 9, 2016

Nimeanza Kufundisha Leo

Jana tumeanza muhula mpya wa masomo hapa chuoni St. Olaf, nami nimeanza kufundisha leo. Masomo yangu kwa muhula huu ni matatu: First Year Writing, African Literature, na Muslim Women Writers.

Tumeanza vizuri. Nimepata fursa ya kuwaeleza wanafunzi mambo ya msingi kuhusu falsafa yangu ya ufundishaji, na kuhusu masomo. Nimesisitiza wajibu wa kufikiri na kuchambua masuala, wajibu wa kujenga hoja. Nimesisitiza msimamo wangu wa kulinda na kutetea uhuru wa fikra na kujieleza. Nimewahahakishia wanafunzi kuwa wawe tayari kukabiliana na fikra na hoja mbali mbali.

Siku ya kwanza ya muhula ni kama kitendawili. Hatujui safari itakuwaje, siku hadi siku, lakini tunategemea matokeo mema. Ingawa uzoefu wangu wa kufundisha unaendelea kuongezeka muda wote, haiwezekani kupanga na kuwa na uhakika nini kitatokea. Jambo pekee lisilobadilika ni kwamba kila muhula ni tofauti na mwingine.

2 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Hongera kwa kuanza kufundisha muhula mpya...

Mbele said...

Asante, dada Yasinta Ngonyani. Tangu nilipokuwa mdogo, nilisikia wito wa kuwa mwalimu. Miaka yote nilipokuwa shuleni, lengo langu lilikuwa ni ualimu. Mungu aliniongoza na bado ananiongoza vizuri katika njia hiyo. Ninamshukuru daima. Katika seminari ya Kanisa Katoliki ya Hanga na Likonde nilikosomea (mkoani Ruvuma), 1963-1970, tulifundishwa dhana ya ki-Latini, "ora et labora," yaani sali na kufanya kazi, na kazi iwe kwako kama sala. Ninashukuru kwa fundisho hilo la uwajibikaji.