Sunday, September 4, 2016

Naomba Kitabu Changu Kipigwe Marufuku

Naiomba serikali ikipige marufuku kitabu changu, CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Kitabu hiki kina mawazo ambayo ni kinyume na yale yanayotakiwa na serikali. Kama vile hii haitoshi, kitabu hiki ni cha uchochezi. Tusikubali kurudia makosa kama yale ya kale ambapo Socrates alikuwa anawachochea watu, hasa vijana, wahoji mambo yanayokubalika katika jamii.

Imenibidi nitoe ombi hili la kupigwa marufuku kitabu changu kwa sababu za msingi. Kwanza kama mtu mwingine yeyote mtiifu kwa serikali, ninatambua wajibu wangu wa kuripoti jambo lolote linalokwenda kinyume na maelekezo au matakwa ya serikali. Pili, mimi sina mamlaka kisheria ya kukipiga marufuku kitabu chochote. Kwa hivi, ninaiangukia serikali.

Mawazo yaliyomo katika kitabu hiki yasipodhibitiwa, yakiachwa yaenee, yatajenga ukaidi miongoni mwa raia na tabia ya kutowaheshimu viongozi. Ninaelewa kuwa ni juu ya serikali kufikiri na kufanya maamuzi. Wajibu wa raia ni kutii. Raia wakiachwa huru kufikiri na kujiamulia mambo, kuna hatari kwamba misingi imara ya amani na utulivu nchini itaharibika na itakuwa vigumu kwa nchi kutawalika.

6 comments:

Mzalendo Mpenda Nchi said...

Profesa mjinga fia huko huko Marekani na uzee wako utuachie nchi yetu salama. Eti kitabu, hicho nacho ni kitabu? Tangu lini kijarida kikawa kitabu? Mawazo ya kijinga tu yasiyo na mbele wala nyuma ndiyo unaita mawazo ya kianaharakati? Kuna nini kipya humo ambacho hakijasemwa na majizi akina Mbowe na akina Lowassa? Pengine dementia au Azheimer imekuanza. Na ni nani aliyekisoma hicho kijarida chako?

Kila kukicha kukosoa serikali. My ghosh! Mafisadi yalikuwa yanakusaidia nini huko Marekani? Kama una ubavu si uje nyumbani uje ukione cha moto. Unafikiri kujificha Minnesota kwenye baridi ndiyo ujanja? Ningekuwa polisi ningehakikisha siku unakuja nyumbani nakudaka pale airport halafu nakuweka Segerea kwa wiki moja tu mpaka unyooke. Mchonganishi mkubwa unataka nchi yetu ivurugike wakati wewe uko mbali huko umejificha. Mtu mwenyewe umezeeka na umekaribia kufa. Njama zako za kutumiwa na mabeberu kuvuruga amani yetu na ZISHINDWE MILELE NA MILEE na ukifa uzikwe huko huko usiletwe Songea kabisa. Tutalipiga mawe jeneza lako!

Mbele said...

Mzalendo Mpenda Nchi

Nilipoona umeandika hapa, nilidhani umejadili ujumbe wangu. Katika kusoma ulichoandika, nimeona huongelei nilichoandika, bali umekurupuka na kuleta mambo yako ambayo hayana uhusiano na nilichosema. Je, hii ndio akili unayojivunia?

Umekurupuka na kuongelea mambo ya akina Mbowe, Lowassa, na mafisadi, bila kuhusianisha na ujumbe wangu. Hayo ni maajabu, na maajabu zaidi ni jinsi unavyodai, bila ushahidi, kuwa ninaikosoa serikali. Na hata kama ningeikosoa, huelewi kuwa kuna kitu kinachoitwa uhuru wa kutoa mawazo?

Unavyokuja kwa jazba na vitisho, unanipa ushahidi kuwa wewe una tabia ya kidikteta. Sasa basi, nakupa fundisho. Hii blogu yangu ni uwanja huru, na hayo uliyoandika yatabaki hapa. Ningekuwa dikteta, mwenye kutumia jazba na kutokwa povu kama wewe, ningefuta ujumbe wako. Ninategemea kuwa wewe na madikteta wengine mtaona mfano wa kuigwa kutoka kwangu.

Ungekuwa mtu makini, ungetafakari jambo hilo. Ungejiuliza kwa nini nimekuacha huru kuandika hayo uliyoandika, lakini wewe mwenyewe unapandisha jazba na kutokwa povu unapokutana na mawazo yanayopingana na yako. Sambaza fundisho hili kwa wenzako wenye mwelekeo wa kidikteta.

Ungekuwa mtu unayefahamu uwanja wa vitabu, ungejua kuwa vitabu huandikwa kwa malengo maalum. Ni uamuzi wa mwandishi kuandika kitabu kikubwa au kidogo. Waandishi wa kila aina hifanya hivyo.

Nikupe mifano michache ya waandishi maarufu. Karl Marx, pamoja na kuandika vitabu vikubwa sana, kama "Das Kapital," aliandika pia vitabu vifupi, kama vile "The Communist Manifesto." Albert Einstein aliandika kifupi sana, hata katika uwanja wake wa fizikia. Aliandika pia vitabu vifupi ambavyo ni mkusanyiko wa insha fupi fupi sana juu ya masuala ya jamii, siasa, na kadhalika. Vyote ni vifupi kabisa, kuliko hata hicho changu.

Mwalimu Julius Nyerere naye aliandika vitabu kadhaa vifupi kabisa, kama vile "Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania." Frantz Fanon, pamoja na kuandika vitabu vikubwa kama vile "The Wretched of the Earth" na "Black Skin, White Masks," aliandika pia vitabu vifupi sana, kama vile "A Dying Colonialism," ambacho ni mkusanyo wa insha. Chinua Achebe, Wole Soyinka, Mario Vargas Llosa, na wengine wengi wasiohesabika, nao ni hivyo hivyo.

Lakini wewe, pamoja na kujiweka kimbele mbele, inaonekana hujui hayo. Na jambo la msingi ambalo, pamoja na mbwembwe zako, inaonekana hulijui ni kuwa suala si ukubwa wa kitabu, bali kilichoandikwa humo. Ungekuwa makini, ungezingatia hilo. Ungekuwa umesoma hicho kitabu changu, ungeleta angalau dondoo chache katika huu ujumbe wako. Huu ndio utaratibu wanaotumia wasomi. Acha kuparamia uwanja ambao huna ufahamu nao.

Tanzania si nchi ya watu fulani tu, watu wa aina yako peke yenu. Tafakari huo ujinga wako. Hata hiyo serikali unayojifanya kuitetea ina akili kukuzidi juu ya suala hilo. Inawatambua wanadiaspora, na inafanya juu chini kuwaunganisha katika kuliendeleza Taifa. Fikra zako ni za kuhujumu Taifa. Kama ni kukamatwa na hao polisi, ukamatwe wewe, kwani unahujumu malengo ya serikali.

Kama unasubiri nipate hayo maradhi na kifo, kumbuka kuwa mwenye kupanga ni Mungu. Unaweza kuyapata wewe kabla yangu, na ukafa kabla yangu, ushindwe hata kulipiga jiwe jeneza langu. Mungu ameridhika kuniweka hai na mwenye akili timamu mpaka wakati huu. Alhamdulillah, ninaendelea na ufundishaji, uandishi na utafiti na ninaendelea kutoa mada kwenye mikutano ya wanataaluma ulimwenguni. Hata kama wewe unaniona mjinga, unajisumbua bure. Ni bora uende shule ukajipunguze ujinga unaokusumbua.

Anonymous said...

Pole Profesa, nimesikitishwa sana na namna ya kujeli na lugha ya maudhi isiyo kuwa na staa ya mchangiaji wa mwanzo. Hii ndio picha halisi ya kizazi hiki kisicho na utashi wa kupambana na hoja iliyoko mezani bali lugha za kejeli na kuudhi ili kupotosha maana halisi ya hoja husika, wasikuvunje moyo katika kuandika maana ni watu wa namna hii wanaoliangusha taifa letu pendwa kwa mawazo yso finyu yenye ubinafsi wa kutaka mawazo yao yasikilizwe bila kukosolewa. Inasikitisha ila tunasafari ndefu huko tuendako ila mchango wako ni muhimu katika safari yataifa letu maana hasi na chanya ndio huzalisha umeme usivunjike moyo

Mbele said...

Ndugu Anonymous

Shukrani kwa ujumbe wako. Usikose usingizi, tafadhali. Mimi kama mwendeshaji wa blogu, ningeweza kuifanya blogu yangu isipokee kabisa maoni yoyote, bali niwe nachapisha maoni yangu tu. Au, ningeweza kuchagua maoni yepi ya kuyaruhusu na yepi ya kuyatupa kapuni.

Lakini mimi kama msomi ninasimama upande wa uhuru wa watu kutoa mawazo. Sijawahi kumzuia yeyote. Nimejengeka hivyo. Na ndio maana ninaitetea katiba ya Tanzania na sheria ya vyama vya siasa ambazo zote zinatambua haki na uhuru wa watu kutoa mawazo, kufanya mikutano na maandamano kwa amani.

Niliposikia kuwa Tundu Lissu amesema kuwa rais ni dikteta uchwara, nilitegemea kuwa wahusika wangejibu tu hoja zake na kuthibitisha kuwa rais si dikteta uchwara. Hoja ingejibiwa kwa hoja, na biashara ingeishia hapo. Kwa utawala ambao unasemekana una wasomi wengi, nilitegemea hivyo.

Kuna usemi katika ki-Ingereza kwamba "charity begins at home," na ndio maana uhuru huo ninaulinda tangu hapa kwenye blogu yangu.

NN Mhango said...

Ama kweli ujinga ni mzigo. Siku nyingi sijapita hapa. Sikujua kuwa bado kuna watu wanaotumia makalio kufikiri. Nani huyo ambaye hatazeeka? Hata mawe huzeeka. Kama huna cha kusema ni bora kunyamaza. Laiti, usingeficha jina lako, ningekushughulikia na kukusulubu. Kama unataka kusoma vitabu na si vijarida je wewe umeandika vingapi na vipi tuvisome lau tujue uwezo wako wa kufikiri. Kama una hasira na akina Mbowe na unajidai uko Tanzania si uende ukapambane nao. Huu upupu ungeniandika mimi ningekushukia hadi mama yako akaujua alipoteza muda kubeba uchafu miezi tisa. POLE SANA ndugu Mbele kwa matusi ya kipuuzi. Huyu jamaa angekua ulivyofunga nyama wala asingepoteza muda kujivua nguo. Ashindwe na alegee.

Mbele said...

Ndugu Mhango

Karibu tena. Kama nilivyoelezea katika majibu yangu hapa juu, ninategemea kuwa huyu mchangiaji unayemwongelea na wengine kama yeye, waone umuhimu wa uhuru wa kutoa maoni, kama ulivyo katika hii blogu yangu. Huyu mchangiaji ameleta kauli zake hapa kwenye uhuru wa kutoa maoni, ingawa yeye mwenyewe anaonekana ni mtetezi wa mfumo wa CCM, ambao ni wa kidikteta, unaokandamiza uhuru wa watu kutoa maoni.

Hao akina Mbowe wanavyohamasisha harakati dhidi ya udikteta, wanavyopigania uhuru na haki zinazotambuliwa katika katiba na sheria za Tanzania, wanathibitisha kuwa wana busara kuliko huyu mchangiaji anayewashambulia. Nategemea wote wanaosoma ukurasa huu wanaona suala lilivyo, kwamba tuna mtu ambaye amekuja hapa kwenye blogu yangu na kufaidi uhuru uliopo, lakini mtu huyo huyo ni mtetezi wa serikali ya CCM, ambayo inahujumu uhuru wa wa-Tanzania.

Lakini nina mashaka na akili ya mchangiaji huyu. Anavyoongea kwa kubeza dhana ya kijarida, ninawajibika kusema neno juu ya suala hili. Katika historia, vijarida ("pamphlets") vimekuwa na mchango mkubwa katika kuchochea fikra na kuendeleza harakati za kijamii, hasa siasa. Ninaweza kutoa mifano.

Waandishi wa hivi vijarida, ambao kwa ki-Ingereza huitwa "pamphleteers," walikuwa na mchango mkubwa katika mapinduzi ya Marekani ("American Revolution"). Ulaya na Marekani, "pamphleteers" kama John Milton, Thomas Paine, na Jonathan Swift, walitoa mchango mkubwa katika harakati za kijamii.

Wala si Ulaya na Marekani tu, ambako "pamphleteers walitoa mchango katika harakati za jamii, bali sehemu zingine za dunia pia, ikiwemo Afrika. Nchini Kenya, kwa mfano, mwanaharakati na mshairi maarufu Abdilatif Abdalla wa Mombasa alichapisha kijarida chake "Kenya Twendapi," mwaka 1968, ambacho kilikuwa tishio kwa serikali ya Rais Jomo Kenyatta kiasi kwamba Abdilatif alikamatwa akafungwa kipindi cha 1969-72.

Kama nilivyosema katika jibu langu refu hapo juu, mchangiaji huyu anayejiita Mzalendo Mpenda Nchi alipaswa atambue kwamba suala si urefu au ufupi wa kitabu au kijarida. Suala ni kilichoandikwa humo. Aache uropokaji wake, na badala yake asome ajipunguze ujinga.