Wednesday, September 9, 2015

Vijana Wameonana Na Mzee Patrick Hemingway

Leo nimepata ujumbe na picha kutoka kwa Jimmy Gildea, anayeonekana kushoto kabisa pichani hapa kushoto, kwamba walikuwa mjini Bozeman, Montana, wakingojea kuonana na Mzee Patrick Hemingway na mkewe Mama Carol.

Jimmy alikuwa ni mmoja wa wanafunzi wangu katika kozi ya Hemingway in East Africaambayo nilifundisha Tanzania mwezi Januari mwaka 2013. Kutokana na kozi ile, na pia safari tuliyofunga kwenda Montana kuonana na Mzee Patrick Hemingway, Jimmy ametengeneza filamu iitwayo Papa's Shadow, ambayo kwa kiasi kikubwa inatokana na kozi ile.

Katika filamu hii, ambayo si ya maigizo, Mzee Patrick Hemingway na mimi tunaongelea maisha na maandishi ya baba yake, Ernest Hemingway, na tunaongelea kwa undani zaidi maisha na mizunguko yake Afrika Mashariki, miaka ya 1933-34 na 1953-54, na pia falsafa yake kuhusu masuala ya maisha na uandishi. Katika kutengeneza filamu hiyo, Jimmy ameshirikiana na hao vijana wanaoonekana pichani, na wengine ambao hawamo pichani.

Nimetamani sana kama nami ningekuwa Bozeman leo kuonana na Mzee Patrick Hemingway na Mama Carol. Hata hivi, nafarijika kwamba ninampigia simu wakati wowote nikipenda. Kwa kuwa aliishi miaka yapata 25 Tanganyika (na hatimaye Tanzania), ameniambia kuwa anafurahi kuongea na mimi, kwa kuwa hana watu wa kuongea nao kuhusu Tanzania na Afrika.

Kwa upande wangu, najifunza mengi kutoka kwa Mzee Patrick Hemingway, juu ya Ernest Hemingway, waandishi wengine, historia ya Tanganyika, na mambo mengine mengine. Pia ninaguswa kwa jinsi anavyokipenda kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Hata katika filamu ya Papa's Shadow anakitaja na kukinukuu. Katika hiyo picha ya pili, tuliyopiga nyumbani mwake mjini Craig, Montana, anaonekana Mzee na Mama Carol Hemingway, na kitabu kiko mezani hapo mbele yake.

No comments: