Tuesday, September 8, 2015

Udini Katika Kampeni za Urais

Katika kipindi hiki cha kampeni za urais nchini Tanzania, tunashuhudia mengi. Kwa mfano, kwa siku mbili tatu hivi tumekuwa tukisikia shutuma nyingi dhidi ya mgombea wa UKAWA, Edward Lowassa kwamba anafanya udini. Chanzo cha shutuma ni kauli anayoonekana akitoa katika video alipokuwa anaongea na waumini wa ki-Luteri. Anasikika akiomba wamwunge mkono, awe m-Luteri wa kwanza kuwa rais.

Kauli hiyo imewasha moto miongoni mwa wapinzani wake, kwa mfano CCM. Wamekazana kupaaza sauti wakisema kuwa mgombea huyu hafai; anatugawanya kwa msingi wa dini, na atatuletea maafa akiwa rais.

Binafsi, sioni kama watu hao wana hoja ya msingi. Lowassa hana tabia hiyo inayosemwa. Tumemshuhudia kwa miaka anavyojumuika na waumini wa dini mbali mbali katika shughuli zao. Tumemwona akiongoza harambee za kuchangia misikiti na makanisa ya madhehebu mbali mbali sehemu mbali mbali za nchi. Kwa kufahamu alivyo na ushawishi mkubwa, viongozi na waumini wa dini mbali mbali wanafurahi kumwalika kwenye shughuli zao hizo.

Kwa kuizingatia hayo, ni wazi kuwa alichosema kwa waumini wenzake akiwaomba wampe kura siwezi kukiita udini. Siamini kama alikuwa na nia mbaya. Ni jambo la kawaida kabisa tunapokuwa na watu wa aina yetu tunazungumza kwa namna tofauti na tunapokuwa katika mazingira mengine.

Lowassa hakuwa anaongea na umma wa wa-Tanzania. Alikuwa anaongea na wa-Luteri wenzake, sawa na mimi ninavyoweza kuongea na wa-Matengo wenzangu au wa-Katoliki wenzangu, si kwa nia mbaya ya kibaguzi hata kidogo. Naweza kukubali kuwa labda Lowassa aliteleza katika kauli yake, lakini sikubali kuwa yeye anafanya udini.

Kinachonishangaza ni kuwa katibu mwenezi wa CCM, Nape Nnauye, ambaye ndiye, kama msemaji wa CCM, alitoa tamko la kumshutumu Lowassa, alisema siku kadhaa zilizopita kuwa CCM lazima ishinde uchaguzi, hata kwa goli la mkono. Aliwaambia hivyo wanahabari. Yaani aliitangazia dunia dhamira hii ya kuhatarisha amani. Ni tofauti na Lowassa ambaye alikuwa anaongea na wa-Luteri wenzake kanisani.

Nape Nnauye angekuwa ameongea na wanaCCM wenzake peke yao, huenda hata sisi wengine hatungesikia kauli yake. Hata kama tungesikia, yaani kama kauli yake ingevuja, kama ilivyovuja ya Lowassa, ningemhukumu kwa namna hiyo ninayomhukumu Lowassa. Lakini yeye amevuka mstari na kuutangazia ulimwengu dhamira ambayo ni mbaya kwa Taifa. Haoni hilo kosa lake kubwa, ila anajipa jukumu la kumshutumu Lowassa. Inanishangaza.

1 comment:

NN Mhango said...

Japo Lowassa anaweza kutokuwa na nia ya udini, kauli yake ya kutaka awe "mlutheri" wa kwanza kuwa rais ina kila upenyo wa kuweza kutafsirika kama ya kidini. Hivi angewaambia wamasai wenzake wampe kura ili awe mmasai wa kwanza kuwa rais unadhani isingeonekana kama ya kikabila? Kusema kuwa huamini kama Lowassa alikuwa na nia ya udini ni kumsemea msemaji. Si rahisi kujua nia ya mtu kwa kuangalia mazoea yake. Binadamu ni kiumbe asiyetabirika. Nadhani CCM hawajakosea kusema mameno ya Lowassa yana udini hasa ikizingatiwa kuwa: a) Wanamuona Lowassa kama tishio kwa ulaji wao wa miaka mingi. b) Pia jinsi UKAWA alivyoruhusu askofu wa kujipachia Gwajima kuwa msemaji na bingwa wa mikakati michafu na ya kijinga ya kumjibu Dk. Slaa kama alivyokarriwa hivi karibuni akisema mke wa Slaa ana mapepo jambo ambalo ni kufichua siri za waumini wake. Nadhani UKAWA na Lowassa wanapaswa kuwa makini na wale wanaopenda kuwatetea hata kwa kuwaonyesha tofauti na walivyo kama anavyofanya Gwajima.
Kuhusiana na CCM kudai Lowassa anahubiri udini ni dhahiri. Lowassa kusema ukweli ameitikisa CCM hadi kwenye mfupa. Hivyo, silaha yoyote inayoweza kumuangamiza hata kumuonyesha kama asiyefaa kwao "ruksa" kama ambavyo UKAWA nayo inaruhusu watu kama Gwajima ambao kimsingi hawaijengi bali kuibomoa. Hata hivyo, UKAWA wana bahati. Kwani Gwajima si askofu wa kweli kama wale tunaowafahamu zaidi ya kujipachika na kutafuta ulaji.