Sunday, June 3, 2018

Vitendea Kazi vya Kampuni Yangu

Mwaka 2002, nilianzisha na kusajili kampuni ambayo niliita Africonexion, kama nilivyoandika katika blogu hii. Nilisajili kama kampuni binafsi, usajili ambao hapa Marekani hujulikana kama "sole proprietorship." Niliamua kuanzisha na kusajili kampuni hii ya kutoaelimu na ushauri wa masuala ya utamaduni kwa kuwa tayari nilikuwa na uzoefu wa shughuli hizo, nikihudumia vyuo, makanisa, mashirika, jumuia na watu binafsi.

Shughuli zangu hizi zimekuwa na mafanikio makubwa, kwa maana kwamba nimewasaidia watu kuelewa na kuepukana na mambo ambayo yanaweza kusababisha migogoro na kutoelewana. Wale ambao tayari walishakumbana na migogoro na kutoelewana nimewasaidia kufahamu kwa nini walijikuta katika migogoro na kutoelewana. Lakini mimi mwenyewe nimefanikiwa pia kujifunza mengi katika shughuli zote hizo.

Napenda kuelezea siri moja kubwa ya mafanikio haya. Siri hiyo ni kujielimisha kwa kutumia vitabu. Vitabu ndio vitendea kazi vyangu. Sichoki kununua na kusoma vitabu. Kulingana na shughuli za kampuni yangu, ninanunua na ninasoma vitabu kuhusu masuala kama utandawazi, utamaduni, na saikolojia. Jana, kwa mfano, bila kutegemea, nilikiona kitabu kiitwacho Riding the Waves of Culture, katika duka la Half Price Books, mjini Apple Valley. Nilipokiona tu, nilitambua kuwa kitakuwa kitendea kazi muhimu.

Mbali na kutumia vitabu vya wengine, ninatumia pia kitabu nilichoandika mwenyewe, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Kitabu hiki kilitokana na uzoefu nilioongelea hapa juu. Si mimi tu ambaye ninakichukulia kitabu hiki kama kitendea kazi muhimu. Mifano ni profesa na mwandishi maarufu Becky Fjelland Brooks, ambaye aliakiongelea kitabu katika blogu yake. Mzee Patrick Hemingway, ambaye aliwahi kuishi Tanzania miaka yapata ishirini na tano, aliwahi kuniambia kuwa kitabu hiki ni "a tool of survival" yaani kimbilio la usalama.

Hili suala la kuviona vitabu kama vitendea kazi ni muhimu. Hainiingii akilini mtu aanzishe biashara, kwa mfano, halafu asitafute na kusoma vitabu au maandishi mengine juu ya uendeshaji wa biashara. Atafanikishaje malengo yake kama hafahamu vitu kama saikolojia ya binadamu, ambao ndio wateja wake? Atafanikiwaje kama hafahamu namna ya kuwasiliana na watu? Kama wateja wake ni wa tamaduni tofauti na utamaduni wake, ni muhimu mno afahamu tofauti hizo.

Nilivutiwa na msimamo wa Mama Barbro Finskas Mushendwa, mmiliki wa kampuni ya utalii ya J.M Tours, yenye makao yake Arusha, Tanzania. Baada ya kusoma kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, aliamua kununua nakala kadhaa kwa ajili ya wafanyakazi wake, ambao walikuwa ni madreva wa watalii. Aliona haraka kuwa kitabu hiki kinafaa kama kitendea kazi na madreva wake walinithibitishia hivyo, kama nilivyoripoti katika blogu ya ki-Ingereza.

Mmiliki wa kampuni yoyote anajua ulazima wa vitendea kazi kama vile magari na kompyuta, sawa na mkulima navyojua ulazima wa jembe na shoka. Lakini sijui ni wamiliki wa makampuni na wafanya biashara wangapi wa Tanzania wenye mtazamo kama wa Mama Mushendwa, wa kutambua kuwa vitabu ni vitendea kazi. Ninaona wanaanzisha kampuni au biashara na kuziendesha kimazoea,  au kwa kutegemea kudra ya Mungu au hata waganga wa kienyeji. Daima ninaona matangazo ya waganga wa kienyeji wakinadi dawa za mafanikio kibiashara.

Ninapoongelea mada hii ya vitabu kama vitendea kazi, ninakumbuka juhudi aliyofanya Mwalimu Nyerere katika kutekeleza kile alichoita elimu yenye manufaa. Aliwahimiza watu kujisomea ili kuboresha shughuli walizokuwa wanafanya. Chini ya uongozi wake, vilichapishwa na kusambazwa vitabu kuhusu kilimo, uvuvi, useremala, na kadhalika. Ninakumbuka kwamba kijijini kwangu, vitabu hivyo vilihifadhiwa katika nyumba ya baba yangu.

Pamoja na mimi kutumia vitabu vya wengine kama vitendea kazi, ninashukuru kwamba nami ni mwandishi. Ninapangia kuendelea kuandika ili kuchangia ufanisi katika shughuli zangu na za wengine.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...