Nimeona nianzishe mjadala wa suala linalovuma wakati huu nchini Tanzania, ambalo ni: Je, Rais Magufuli ni dikteta uchwara?
Tundu Lissu, mwanasheria wa CHADEMA ndiye mwanzilishi wa dhana hii ya kwamba Rais Magufuli ni dikteta uchwara. Kwa kuanzia, ninapenda kuwashutumu polisi na watawala wa CCM kwa namna walivyolishughulikia suala hili.
Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, Tundu Lissu ana haki na uhuru wa kuwa na mawazo yake kuhusu suala lolote. Ana haki na uhuru wa kuwa na mtazamo wake juu ya Rais Magufuli. Ana haki na uhuru wa kutoa mawazo yake kama alivyofanya.
Mtu mwingine yeyote naye ana haki na uhuru huo. Kwa hivi, kauli ya Tundu Lissu haikuhitaji hatua zilizochukuliwa na polisi za kwenda kumkamata na kumsafirisha kutoka Singida hadi Dar es Salaam kwa mahojiano makao makuu ya polisi.
Jambo ambalo lingeweza kufanyika, bila taabu yote hii na ufujaji wa hela za walipa kodi, ilikuwa ni kwa serikali kujibu hoja za Tundu Lissu na kuthibitisha kuwa Rais Magufuli si dikteta uchwara. Malumbano ya hoja yangetosha.
Ndio utaratibu unaotakiwa katika jamii iliyostaarabika. Ninaamini kuwa wa-Tanzania wana akili timamu, na wana uwezo wa kuchambua mambo. Wana uwezo wa kusikiliza hoja za pande mbali mbali na kutambua upande upi ni sahihi. Madai ya polisi na watawala wa Tanzania kwamba kauli ya Tundu Lissu ni uchochezi ni ya kuwadhalilisha wananchi. Ni kusema kwamba wananchi ni wajinga, wasio na uwezo wa kutathmini na kuchambua mambo.
Ni kwa nini serikali haikuchukua njia hii ya kujibu hoja kwa hoja? Inamaanisha kwamba katika serikali nzima hakuna mtu mwenye akili ya kuweza kumpinga Tundu Lissu na kuthibitisha kuwa Rais Magufuli si dikteta uchwara? Inamaanisha kuwa watendaji wote wa serikali hii ya CCM ni watendaji uchwara, au ni watendaji hewa, au ni vilaza?
Rais Magufuli, kwa mtazamo wangu, amekuwa akivuka mipaka ya katiba kwa baadhi ya kauli zake. Hana mamlaka kikatiba wala kwa mujibu wa sheria za vyama vya siasa, kuweka vizuizi juu ya mikutano na maandamano ya vyama vya siasa. Taratibu zote zimeelezwa katika katiba ya Tanzania na katika sheria ya vyama vya siasa.
Kwa bahati nzuri, katiba ninayo na nimeisoma, na sheria ya vyama vya siasa, ambayo imewekwa kwenye tovuti ya ofisi ya msajili wa vyama, nimeisoma pia: http://www.orpp.go.tz/en/rules/. Kwa kupitia katiba na sheria, ni wazi kuwa Rais Magufuli anakiuka katiba na sheria, na kwa hivyo, kauli ya Tundu Lissu kwamba Rais Magufuli ni dikteta uchwara ni sahihi.
Vyama vya siasa vinawajibika kufanya mikutano na maandamo kwa amani, ili kutangaza sera zao, kutafuta wanachama wapya, na kadhalika. Rais Magufuli, au mtu mwingine yeyote hana wadhifa wa kuwawekea zuio kama alivyofanya. Hana mamlaka ya kusema kwamba watu wafanye siasa katika maeneo yao tu. Hana mamlaka ya kutangaza, hata kwa kisingizio cha "hapa kazi tu," shughuli zipi za kisiasa zisitishwe hadi mwaka 2020. Huu ni udikteta.
Mimi ni raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Ninachotaka ni kuona nchi inaendeshwa kwa mujibu wa katiba na sheria zilizopo. Ninataka utawala wa sheria, unaozingatia haki za binadamu.
No comments:
Post a Comment