Saturday, January 11, 2014

Yule Mama Kutoka Togo Kaja Mara ya Tatu Kununua Vitabu

Yule mama kutoka Togo, ambaye nimemtaja mara kadhaa katika blogu hii, kaja tena leo. Amenunua nakala sita za kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Amesema ni kwa ajili ya mabosi kazini kwake, kuwasaidia kufahamu namna ya kuhusiana na wa-Afrika.

 Nakala nilizokuwa nazo zimeisha sasa. Imebaki moja tu. Watu siku hizi, hasa hapa Marekani, hununua vitabu mtandaoni. Tekinolojia imepiga hatua. Sio kama zamani, ambapo mwandishi alikuwa na shehena ya vitabu vyake nyumbani, na watu wakawa wanavipata kwake. Mimi mwenyewe huwa na nakala kiasi tu, kwa ajili ya matamasha ya vitabu ninayoshiriki, ambayo nayaelezea katika blogu hii mara kwa mara.

 Lakini, hata hapa Marekani kuna watu wanaosita kununua vitu mtandaoni, wakihofia usalama wa "credit card" zao. Hao ni baadhi ya wale wanaomwendea mwandishi, au wanakwenda kwenye maduka ya vitabu kama tulivyozoea.

 Kutokana na kuishiwa nakala zangu, leo hii nimeagiza nakala 20 huko mtandaoni www.lulu.com/content/105001. Nami hulipia, ingawa, kwa vile ni mwandishi, napata punguzo la bei huko huko mtandaoni.

No comments: