Tangu mwaka juzi, nimeendesha warsha Tanzania, kuhusu masuala ya utamaduni, utandawazi, na maendeleo. Nina malengo kadhaa katika kufanya hivyo.
Lengo moja ni kuwapa wa-Tanzania ujuzi ambao ninaendelea kuupata huku ughaibuni, kutokana na kusoma vitabu, kuongea na watu, na kuendesha warsha kuhusu masuala niliyotaja hapo juu. Natambua umuhimu wa kutoa fursa kwa wa-Tanzania kuyaelewa masuala hayo, waweze kujizatiti kwa ushindani wa dunia ya leo. Hakuna msingi bora na imara kuliko elimu.
Lengo la pili la kuendesha warsha hizi Tanzania ni kuleta mwamko mpya katika mfumo na uendeshaji wa warsha. Kwanza, kuna mtindo wa kutegemea wafadhili. Watu wamezoea kuona warsha zikifanyika kwa kutegemea fedha kutoka kwa wafadhili au taasisi fulani. Wahudhuriaji wa warsha wanategemea kulipiwa gharama za ushiriki, pamoja na posho. Vibahasha vya posho ni sehemu ya utamaduni wa warsha katika Tanzania.
Ninapinga utamaduni huu. Sitafuti wafadhili wa kulipia warsha zangu, na warsha zangu hazina posho. Badala yake, wanaohudhuria wanalipia.
Kwa mtazamo wangu, warsha ni fursa ya kujielimisha. Elimu ni mtaji mkubwa, pengine muhimu kuliko mitaji yote. Kama mtu analipia trekta limzalishie mazao shambani, kwa nini asilipie mtaji huu mkubwa kuliko yote, yaani elimu?
Huku Marekani, ninaona utaratibu huu wa kulipia warsha. Mimi mwenyewe nimeshalipia hela nyingi kuhudhuria warsha hizi. Ninajua umuhimu wake. Niligusia kidogo jambo hili katika blogu hii, nilipoongelea suala la kununua vitabu.
Ninanunua pia vitabu na kuvisoma. Kati ya vitabu nilivyonunua hivi karibuni ni Global Literacies. Kwa kusoma vitabu na kuhudhuria warsha, ninajiongezea mtaji wa elimu. Ufanisi wangu kama mtoa mada na mwendesha warsha unaendelea kuongezeka.
Katika kuendesha warsha zangu Tanzania, nataka kujenga utamaduni wa kuthamini elimu. Msimamo huu unanipa wajibu mkubwa. Nawajibika kujielimisha kwa uwezo wangu wote, ili niweze kuwa mwelimishaji bora. Ndio maana ninafanya bidii kuhudhuria warsha, kununua vitabu na kuvisoma, na pia kuendesha warsha. Ninaelimika hata ninapoendesha warsha.
Nawakaribisheni kwenye warsha zangu za mwaka huu:
Juni 12, "Culture, Globalization and Development," Meeting Point Tanga.
Julai 3, "Culture and Globalization," Arusha Community Church.
Julai 10, "Cultural Tourism," Arusha Community Church.
Natarajia kupanga warsha nyingine moja au mbili. Wasiliana nami: info@africonexion.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
1 comment:
Profesa,pongezi nyingi kwa warsha zako ambazo naamini ni nafasi nzuri kwa wahudhuriaji kujifunza mambo mbalimbali.Kuhusu tatizo la posho nadhani,kama alivyosema Balozi wa Sweden wakati anaaga baada ya kumaliza muda wake wa utumishi huko nyumbani,serikali yetu ni mahiri sana katika kuendeleza utamaduni huo.Na angalau posho hizo zingekuwa zinalipwa kwa minajili ya kufidia gharama wanazotumia wahudhuriaji wa semina,warsha,makongamano,vikao,nk.Nyingi ya posho hizo ni za kisanii licha ya ukweli baadhi ya mijumuiko hiyo haikupaswa kufanyika in the first place.Hata hivyo,naamini kwa ushauri mnaotoa walimu wetu kuna uwezekano wahusika wakasikia na kufanyia kazi.Haiyumkiniki kumlipa mbunge posho ya shilingi laki moja wakati kikao anachohudhuria ni sehemu ya ajira yake inayompatia mshahara wa mamilioni.Mbona walimu hawalipwi posho kwa kila kipindi wanachoingia darasani,au madaktari kwa kila wanapofika kazini?
Kingine,naomba kushauri kuwa uangalie uwezekano wa kuzifanya na sehemu nyingine kama hapa Uingereza,au mahala kwingineko duniani kwenye idadi ya kuridhisha ya Watanzania.
Na jingine dogo,japo la muhimu ,ni ombi langu kwa ninyi walimu wetu kuangalia uwezekano wa kutujumuisha sie vijana wenu kushiriki katika harakati kubwa mnazofanya kimataifa.
Nakutakia kila la heri Mwalimu.
Post a Comment