Sunday, August 1, 2010

Ninasoma "Diwani ya Mnyampala"

Kwa siku hizi mbili tatu nimekuwa nikisoma Diwani ya Mnyampala, kitabu nilichonunua katika duka la vitabu la Chuo Kikuu Dar es Salaam tarehe 27 Julai. Nilizikuta nakala kadhaa, kuukuu, nami nikanunua moja, kwa bei ya shilingi 5,000. Kampuni iliyochapisha kitabu hiki, East African Publications, haiko tena, na kwa vile sina hakika kama kitabu hiki kinachapishwa mahali popote pengine, nilijiona nina bahati kukipata.

Ninaona fahari kuwa na kitabu hiki. Kitachangia juhudi zangu za kujiongezea ufahamu wa matumizi ya ki-Swahili, lugha ambayo nataka niweze kuitumia vizuri katika maandishi yangu. Azma hiyo nimeshaitaja kabla.

Mathias Mnyampala ni mwandishi maarufu. Sifa zake nilizifahamu tangu nilipokuwa kijana. Pamoja na tungo zake nyingi, alikuwa akihusishwa na chimbuko la ngonjera. Nilifahamu kuhusu kitabu chake cha Kisa cha Mrina Asali. Hatimaye, nilipokuwa nafundisha Chuo Kikuu Dar es Salaam, nilikijumlisha kitabu hiki katika orodha ya vitabu nilivyovitumia katika somo la fasihi simulizi, kama njia ya kuonyesha kuwa waandishi aghalabu wanakuwa wamejikita katika fasihi simulizi. Kisa cha Mrina Asali ni muendelezo wa hadithi za jadi za ushujaa, ambazo kwa ki-Ingereza zinaitwa epics. Tunaweza kuitafsiri dhana hii kijuujuu kama tendi.

Ninaifurahia Diwani ya Mnyampala. Ni kazi ya mshairi aliyekuwa na nidhamu ya hali ya juu katika utungaji wake. Mashairi yake yanafuata mtindo wa vina na mizani. Anathibitisha jinsi alivyokuwa sambamba na washairi wengine, kwa malumbano na majibizano mengine. Nimeguswa na jinsi anavyomwombea Mwalimu Nyerere, ambaye kwa wakati ule alikuwa anaanza kuiongoza Tanganyika.

Nimeguswa na namna anavyoomboleza kifo cha Shaaban Robert. Katika utungo moja anasema kuwa kufariki na kwa Shaaban Robert ni pigo kubwa, kama kuzimika kwa taa katikati ya usiku. Kama Shaaban Robert, Mnyampala alikuwa anaiheshimu sana lugha ya ki-Swahili, hata akaitungia shairi liitwalo “Lugha Yetu Kiswahili.” Diwani ya Mnyampala ni kioo murua ya masuala mbali mbali ya jamii yaliyokuwepo wakati wa maisha yake na Tanganyika ya wakati wake.

5 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Haki ya nani ni bahati na una haki ya kujivuna kupata hivyo vitabu sijawahi kuvisomalakini kwa kusoma maelezo yako tu nimejikuta kama vile nimesoma. Nina swali je? unaweza kuazimisha hicho kitabu? ni ombi au wazo tu.... nakutakia kila la kheri, akanono!

Mbele said...

Shukrani kwa ujumbe, Dada Yasinta. Niko hapa Lushoto kuanzia jana, nikifaidi hali ya hewa ya hapa. Nafurahi kuwa habari ya vitabu hivi inakuvutia. Tutawasiliana.

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Kichwa cha habari tu kinavutia..!

Ni wazi fasihi yetu huwa ni tamu sana! Tuiendeleze!

Unknown said...

Diwani ya mnyampala.nilikisoma mwaka 1980.lakini nimejitahidi kukitafuta mpaka leo sijafanikiwa kukipata.ninapenda mashairi sana huyu mzee alikuwa na uwezo kweli

yusuph kamote said...

kwanza binafsi nikupongeze kwa kuweza kupata nakala ya utamu na radha za ufasaha wa kutumia vyema lugha kulikofanywa na myampala katika diwani ya mnyampala ,naomba tuwasiliane mkuu ,mawasiliano yangu binafsi ni yuskamote@gmail.com

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...