Juzi nilienda chuoni Lake Forest, maili kadhaa kaskazini ya Chicago. Nilishinda pale jana yote. Hapa kushoto ni picha ya Student Center, ambamo wanafunzi hupata chakula na kupumzika. Nilienda na profesa kutoka chuo cha Wheaton, kutathmini programu ya Area Studies. Hii ni programu ambayo inampa mwanafunzi fursa ya kusoma masomo mbali mbali kuhusu sehemu moja ya dunia, kama vile Mashariki ya Kati, Amerika ya Kusini, Afrika, au Asia. Anasoma masomo kama historia, siasa, uchumi, na hata lugha ya sehemu husika. Pia, ikiwezekana, anaenda kusoma katika sehemu hiyo.
Utaratibu wa kutathmini programu na idara mbali mbali za masomo ni wa kawaida katika vyuo vya Marekani. Hufanyika baada ya miaka kadhaa; yaweza kuwa saba, au kumi, na kadhalika.
Shughuli ya kutathmini programu huhitaji mtu usome taarifa mbali mbali zinazoelezea malengo na utaratibu wa masomo hayo, ratiba za masomo, na tathmini kutoka kwa wanafunzi waliosoma masomo hayo. Pia kuna taarifa kuhusu wafundishaji, elimu yao, masomo wanayofanyia utafiti, mihadhara ya kitaamula waliyotoa, vitabu na machapisho mengine waliyoandika, na kadhalika.
Shughuli za kusoma taarifa tulizifanya kabla ya kufanya ziara. Ziara ilitupa fursa kamili ya kuongea na walimu, wakuu wa idara, na mkuu wa kitivo. Kwa siku chache zijazo, kazi yetu sisi wawili itakuwa ni kuandika ripoti yetu na kutoa mapendekezo.
Shughuli hii imeniwezesha kuifahamu vizuri programu ya Area Studies ya chuo cha Lake Forest. Hii haikuwa mara yangu ya kwanza kutembelea chuo hiki. Niliwahi kualikwa na chuo hiki mwaka 2003, kutoa mhadhara ulioitwa "Neo Colonialism and African Development."
Kumbe, dunia ni mzunguko. Mkuu wa programu ya Area Studies, profesa ambaye anasema karibu atastaafu, alinikumbusha mhadhara niliotoa. Anakumbuka hata baadhi ya hoja zangu, na anasema anazitumia katika kufundisha. Yeye ni profesa wa somo la biashara, ambaye anazingatia kipengele cha utamaduni katika mahusiano ya kibiashara hapa duniani. Ametembelea nchi yapata 20 katika utafiti wake.
Nilifurahi kuongea na profesa huyu, ambaye aliniambia anazingatia niliyoandika katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Tuliongea kirefu kwa siku zote mbili nilizokuwa chuoni hapo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
No comments:
Post a Comment