Sunday, September 11, 2011

Nyumba za Ibada Mjini Songea

Kama ilivyo katika miji mingine ya Tanzania, na hata katika vijiji vingi, mjini Songea kuna nyumba za ibada za dini mbali mbali, nami huvutiwa ninapoziona. Ni faraja kuona jinsi wa-Tanzania tulivyo na jadi ya kuishi pamoja bila kujali tofauti za dini. Picha hizi zinazoonekana hapa ni za baadhi ya nyumba za ibada zilizopo katikati ya mji wa Songea.

Hapa kushoto ni kanisa ambalo nalikumbuka tangu nilipofika Songea kwa mara ya kwanza, kwenye mwaka 1963 mwanzoni, nilipokuwa nakwenda kuanza darasa la tano katika Seminari ya Hanga. Kila ninapopita karibu na kanisa hili kumbukumbu hizi zinarudi akilini mwangu.






Hapa kushoto ni kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Songea. Nimewahi kuhudhuria misa katika kanisa hili.












Hapa kushoto ni msikiti. Sioni shida kupiga picha makanisa, lakini sina hakika kuhusu misikiti. Niliwahi kupiga picha msikiti mmoja katika mji fulani mkubwa Tanzania na dakika chache baadaye walikuja watu kunihoji kwa nini nimefanya hivyo. Nilifanya kazi kubwa kuwapa maelezo, na bado haikuwa rahisi kuwaridhisha. Lakini mimi natafuta kumbukumbu na taarifa hizi kwa nia njema, kama nilivyoelezea hapa. Sisiti kukiri kuwa navutiwa na taswira za misikiti.

Hapo nje ya msikiti niliwaona watu wakiuza vitu mbali mbali, kama vile vitabu. Nilivutiwa na uwepo wa vitabu, kwani tangu mwanzo wake, dini ya Islam ilikuwa inahimiza elimu. Inavyoonekana, hata dhana ya madrasa ilimaanisha mahali pa kufundishia taaluma mbali mbali, sio dini tu. Kama kumekuwa na upotoshaji, umetokea baadaye.

8 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Nakusifu sana kwa kutafuta kumbukumbu...Hilo kanisa yaani hapo jimboni ni mara nyingi tu nimesali...huo msikiti wa mkoa nimepita hapo sijui mara ngapi na kusema kweli nilikuwa natamani kweli kupiga picha lakini niliogopa kama ulivyosema wengi wakiona unapiga picha basi maswali kibao . Mwaka 2007 nilienda kijiji cha LUNDO nilipozaliwa na nilichofanya nilisahau kabisa kupiga picha ile shule na pia nyumba niliyokulia ila ipo siku nitafanya tu hili. ... Kazi nzuri Sana...

Mbele said...

Ni kweli kuwa nami katika kukua kwangu Tanganyika na halafu Tanzania nilikuwa naiogopa misikiti. Lakini, miaka ya 1989 na 1990 nilipata fursa ya kwenda Lamu, pwani ya Kenya, ambao ni mji wa kale wa ki-Islam.

Wakati nakiwa safarini kwenda kule, hofu ilinigubika, maana sikujua itakuwaje kwangu mimi mKristu katika mji wa kale wa ki-Islam.

Ajabu ni kuwa niliona mji ule, ingawa una misikiti kila kona, una pia kikanisa chetu waKatoliki. Sio hivyo tu, bali wazee wa kiIslam walinikaribisha vizuri sana, nikawa napiga nao stori kwenye vijiwe vyao.

Wakati wa kwenda msikitini kusali, walikuwa wanatoa udhuru na kuniambia niwangoje hapo kijiweni. Wanaporudi, tunaendelea na stori.

Sio hivyo tu, bali walinipeleka hadi ndani ya misitiki na kunielezea habari za misikiti hiyo. hapo ndipo ikawa mwanzo katika maisha yangu kuona ndani ya msikiti. Wala hawakusita kunieleza utaratibu wa misikiti. Kwa mfano, waliniambia kuwa msikitini sio mahala pa kusali tu, bali hata kupumzika humo ni ruksa. Na kweli, niliwaona watu wamo msikitini wamejilalia usingizi.

Kifupi ni kuwa bila kwenda Lamu, labda ningekuwa bado naiogopa misikiti. Au labda sisi Tanzania tumejijengea jadi hii ya ajabu ya kuogopa nyumba za ibada za dini zingine. Sijui.

haliembe said...

asante sana kwa jithada zako naomba unipe historia ya jiwe la urobi?

Mbele said...

Ndugu Haliembe, shukrani kwa ujumbe. Bahati mbaya sina picha za jiwe la Ulobi, ingawa nilifika juu yake nilipokuwa mdogo. Na kwa vile nilikulia katika kijiji cha karibu yake, nilikuwa naliona daima.

Suali lako limenipa changamoto. Safari ijayo nitakapokuwa nyumbani itabidi niandae picha na kumbukumbu za jiwe hilo.

Nimeandika "Ulobi" kwa sababu katika ki-Matengo hakuna "r." Ndio maana utakuta wa-Matengo walikuwa wanaimba nyimbo za Nyelele, sio Nyerere.

Unknown said...

Mwalimu Mbele salamu, Hili unalosema ni kanisa dogo uliloona 1963 ukiwa unaenda Hanga Sekondari, sio sahihi. Hilo jengo liliitwa "Town Hall" au "Nyumba ya Maendeleo", miaka ya 1960s, hapo palikuwa ukumbi wa disko na shughuli nyingine kama vikao vya watu binafsi na hata maofisi ya serikali wakati fulani. Kabla ya 1968, kukamilika kwa Kanisa kuu la katoliki Songea mjini katisa kuu lilikuwa Matogoro. Mimi ni mdogo nimezaliwa miaka ya 1970s lakini historia hii ndogo naijua vema, miaka ya 1970s kina Bora brothers walionyesha sinema hapo, hilo jengo halijawahi kuwa kanisa. mimi nimezaliwa maeneo hayo na nimecheza sana katika jengo hilo. Labda unalifananisha na Kanisa la Anglikana lilikuwa pale bondeni karibu na Masika Hotel, baadae palikuwa na jengo la KAURU, rekebisha historia hiyo itapendeza ukiweka vizuri. Najua pia kuwa ulisoma na Betram Komba, yule mpiga kinanda chini ya uongozi wa Pr. Mwl. Fratera Gama au siyo? Basi vema rekebisha kidogo. Situmii akaunti yangu halisi katika kupost mawazo haya.

Mbele said...

Ndugu Simba Dume,

Shukrani kwa sahihisho. Lengo ni kuweka taarifa zilizo sahihi, na ni wajibu wa yeyote anayejua ukweli, akiona dosari, afanye ulivyofanya. Kila la heri.

Anonymous said...

kazi nzuuuriiii saaaaaaaaaaaaaaanaa kwa wazawa

Mbele said...

Shukrani, Anonymous, kwa kutembelea "hapa kwetu." Ningekuwa ninaishi huko nyumbani Ruvuma ningekuwa nachapisha picha na taarifa mara kwa mara. Ningekuwa niko Tanzania, ningefanya hivyo hivyo. Mara kwa mara nimewazia kuwatafuta wapiga picha wa Ruvuma wajumuike nami, kwani nina hamu ya kuitangaza Ruvuma.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...