Kama ilivyo kawaida ninapokuwa Dar es Salaam, mwaka huu nilizungukia mara kadhaa maeneo ya Chuo Kikuu Dar es Salaam. Katika duka la vitabu la Taasisi ya Uchunguzi wa Ki-Swahili, ambako nilienda kuangalia vitabu, nilifurahi kuona kitabu kipya cha Haji Gora Haji kiitwacho "Siri ya Ging'ingi," ambacho kilichapishwa na Taasisi hiyo mwaka 2009. Nimeanza tu kukisoma.
Nilikuwa sijakisikia kitabu hiki na nilikinunua hima. Haji Gora Haji ni mtafiti na mwandishi maarufu katika masuala ya ushairi utamaduni na lugha ya ki-Swahili. Upeo wa fikra zake na kina cha uchambuzi wake ni hazina isiyomithilika.
Haji Gora Haji ni mzaliwa wa kisiwa cha Tumbatu. Hakusoma katika hizi shule tunazosomea sisi wengine. Elimu yake aliipatia katika madrasa, kisha akafanya kazi mbali mbali, kama vile uvuvi na ubaharia.
Nimebahatika kuonana naye mjini Zanzibar na kufanya mahojiano naye. Ni mtaalam aliyebobea, mwenye mengi ya kutufundisha. Nina vitabu vyake kadhaa, na napangia siku zijazo kuandika makala kuhusu mchango wake uliotukuka katika sanaa na taaluma. Kwa mfano, mbali na vitabu vyake vya tenzi na mashairi, amefanya utafiti wa kina na kuandika "Kamusi ya Kitumbatu," ambayo ni hazina kubwa.
Kitu kimoja kilichonivutia sana katika kamusi hii ni jinsi ilivyosheheni majina ya aina mbali mbali za samaki na viumbe vingine vya baharini. Yeyote anayedhani kuwa ki-Swahili hakina msamiati wa taaluma kama hii aangalie kamusi hii. Atatambua alivyopotoka.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
2 comments:
haji Gora Haji nifundi sana katika taaluma ya sanaa ya lugha.....kiukweli ninajifunza mengi kupitia kazi zake......ushairi wa KIMBUNGA umenikosha sana na kunisisimua na mshukuru sana kwa mchangowake katika tathnia hii.
Kiosso Mwambashi
Shukrani kwa ujumbe wako. Kutokana na namna ninavyoguswa na tungo za Haji Gora Haji, na ninavyotaka zifahamike ulimwenguni, nimekuwa nikitafsiri baadhi ya mashairi yake kwa ki-Ingereza. Hadi sasa, nimeshatafsiri "Kimbunga," "Nyang'au," na "Kibwangai."
Nimechapisha tafsiri hizi katika blogu zangu, na ninapangia kuendelea kutafsiri na kuchapisha katika majarida ya kimataifa. Kadiri siku zinavyopita, tungo za Haji Gora Haji zinaendelea kufahamika ulimwenguni. Nimeona tafsiri za ki-Ingereza, na hata tafsiri ya ki-Reno katika jarida moja la Angola.
Post a Comment