Nyumbani ni nyumbani. Leo nimeikumbuka Songea, nikaamua kuleta picha mbili tatu nilizopiga mwaka huu. Hapa kushoto ni barabara itokayo stendi kuu kuelekea bomani, hatua chache tu kutoka duka la vitabu la Kanisa Katoliki. Nyuma ya haya majengo ndipo kilipo Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki.
Hapa ni taswira ya uwanja wa Maji Maji, kutoka juu. Nilipiga picha hii kutoka ghorofa ya tatu ya hoteli niliyofikia, ng'ambo ya barabara kutoka kituo kikuu cha polisi. Kule ng'ambo ni kitongoji cha Lizaboni, njiani kuelekea Peramiho, Mbinga, na Mbamba Bay.
Hapa kushoto ni stendi kuu nikiwa na dada yangu na mdogo wangu.
Kama nilivyoelezea tena na tena, napenda kutembelea vyuo ninapokuwa Tanzania. Soma kwa mfano, hapa. Ni fursa ya kujiweka sawa katika ufahamu wa nini kinachoendelea, changamoto zilizopo, mikakati ya kuboresha elimu ya juu. Napata fursa ya kujadiliana na wahusika namna ya kushirikiana na kuchangia vyuo hivi. Tarehe 21 mwezi Julai, mwaka huu, nilitembelea tawi la Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustin, mjini Songea. Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustin ni mradi wa Kanisa Katoliki Tanzania. Ni mtandao ambao tayari una vituo sehemu mbali mbali za nchi. Kwa taarifa zaidi, soma hapa.
Hapa kushoto naonekana na Profesa Donatus Komba, makamu wa mkuu wa chuo
hicho mjini Songea. Yeye ndiye alikuwa mwenyeji wangu siku ya ziara
yangu, akinitembeza kila mahali na kunipa maelezo.
Hapa kushoto naonekana nikitia sahihi katika kitabu cha wageni.
Hapa kushoto ni jengo la utawala. Chuo cha Mtakatifu Augustin kina mipango mikubwa ya kupanua mtandao wake. Kwa upande wa Songea, tayari Seminari Kuu ya Peramiho imeshafanywa sehemu ya Chuo Kikuu, kwa masomo ya falsafa. Wanaofahamu taratibu za seminari za Katoliki wanajua kuwa tangu zamani, mapadri walitakiwa kusoma masomo ya kawaida tunayosoma sisi wengine, na baada ya hapo kwenda seminari kuu kusomea masomo ya teolojia na falsafa. Basi Peramiho sasa ni sehemu ya Chuo Kikuu, kwa masomo haya ya falsafa.
Kanisa Katoliki jimbo la Songea limetoa majengo yaliyowezesha chuo hiki kuanzishwa. Chuo kina mipango ya kuongeza majengo. Nilionyeshwa sehemu mbali mbali, kama vile madarasa, kumbi kubwa, na maktaba. Nilivutiwa kusikia kuwa, mapadri
wastaafu wamekuwa wakichangia hazina ya vitabu vyao katika juhudi za
kuitajirisha maktaba.
Tayari, chuo kikuu cha Songea kinaendesha masomo ya aina mbali mbali. Mimi kama mwalimu wa "Literature" nilifurahi kusikia kuwa hilo ni somo mojawapo katika chuo hiki, na nilifurahi kukutana na mhadhiri wa somo hili.
Kwamba hiki ni chuo cha Kanisa Katoliki haimaanishi kuwa wanaosoma, kufundisha, au kufanya kazi hapo, ni wa-Katoliki tu. Chuo hiki kinawapokea watu wa dini na madhehebu mbali mbali. Angalia, kwa mfano, orodha ya wanafunzi wapya kwa mwaka huu.
Nilijifunza mengi katika ziara yangu hii, na hapa juu nimetoa dondoo chache tu.
Mdau jipatie taarifa zaidi kwa kuangalia video hii inayoelezea ufunguzi wa chuo hiki: