Wednesday, March 2, 2016

Picha za Mtoto Ernest Hemingway

Tarehe 27 Februari, nilitembelea Oak Park, pembeni mwa Chicago. kwa ajili ya kuzuru nyumba alimozaliwa mwandishi Ernest Hemingway na nyumba ya kumbukumbu, Hemingway Museum, kama nilivyoripoti katika blogu hii na blogu ya ki-Ingereza.

Katika Hemingway Museum, ambayo picha yake inaonekana hapa kushoto, niliona picha nyingi, zikiwemo za mtoto Ernest Hemingway.


Hapa kushoto anaonekana babu wa Ernest kwa upande wa mama yake, akiwa na wajukuu. Kushoto kabisa ni Ernest, na hao watoto wengine ni dada zake.
Hapa kushoto anaonekana mtoto Ernest, akiwa na bunduki na zana ya kuvulia samaki. Tangu utotoni, Ernest alifundishwa kuvua samaki na kuwinda.Hapa kushoto, mtoto Ernest anaonekana akimlisha mnyama ambaye kwa ki-Ingereza huitwa squirrel. Nimeangalia mtandaoni nikaona kuwa mnyama huyu anaitwa kindi kwa ki-Swahili.

Nilipoiona picha hii nilivutiwa kuona mnyama ametulia namna hii, lakini nilipoisogelea na kusoma maelezo yanayoonekana chini kushoto, nilitambua kuwa huyu si mnyama hai. Ni mzoga ambao umekarabatiwa na kufanywa uonekane kama mnyama hai.

Hata hivyo picha inanivutia, kwa namna inavyowasilisha ukweli muhimu juu ya Hemingway, jinsi maisha yake na hisia zake zilivyofungamana na maisha ya viumbe kama wanyama, samaki na ndege.

Mtoto Ernest alipokuwa shuleni aliandika kuwa ndoto yake maishani ilikuwa ni kuwa mwandishi na pia mtu wa kusafiri. Ilikuwa kama amejitabiria, kwani akiwa kijana wa miaka 18, alipelekwa Kansas City ambako aliajiriwa kama ripota wa gazeti la Kansas City Star.

Katika kipindi hicho yeye na waandishi wengine wa gazeti hili waliwajibika kufuata orodha ya amri kali kuhusu uandishi uliotakiwa. Watafiti wote wanakubaliana kwamba kufanya kwake kazi katika Kansas City Star kulimjenga Hemingway katika aina ya uandishi aliyotumia maisha yake yote.

Hapa kushoto Ernest anaonekana akiwa ameshika bunduki na ndege. Sikuona maelezo juu ya picha hii, ila ninahisi ilipigwa baada ya Hemingway kumpiga huyu ndege kwa risasi.

Jadi ya kupiga picha ya mwindaji na mnyama au ndege aliyemwua imekuwepo tangu zamani. Kuna picha kadhaa za Hemingway za miaka ya baadaye akiwa na wanyama aliowaua, si tu huku Marekani, bali pia sehemu zingine, ikiwemo Afrika Mashariki. Wachambuzi wa saikolojia wanaweza kuelezea vizuri maana ya jadi hii ya kuthamini hiki kinachoitwa "trophy" kwa ki-Ingereza.

No comments: