Friday, March 4, 2016

Dini ni Siasa Tu, Asema Mwandishi Nawal el SaadawiKatika kozi yangu ya Muslim Women Writers, tunajiandaa kusoma The Fall of the Imam, riwaya ya Nawal el Saadawi wa Misri. Nimeshawapa wanafunzi maelezo kuhusu historia ya fasihi andishi Misri, ambayo imekuwepo tangu miaka yapata elfu saba iliyopita. Hii ni kwa mujibu wa maandishi ya kale yaliyogundulika, kama vile hadithi na mafundisho ya dini, hasa The Egyptian Book of the Dead.

Miaka ilivyopita, fasihi ya Misri ilitajirika kwa kutokana na mikondo ya ndani na nje, na hiyo ya nje ni kutoka sehemu kama Mashariki ya Kati na Uarabuni, pande zingine za Afrika, na Ulaya. Kwa karne moja na kidogo iliyopita, wamejitokeza waandishi wengi maarufu nchini Misri. Mifano ni Naguib Mahfouz, Taha Hussein, Tawfiq al Hakim, Yusuf Idris, Nawal el Saadawi, Sonallah Ibrahim,  na Alifa Rifaat. Kwa ujumla wao, waandishi hao wametumia mikondo niliyoitaja.

Katika kozi hii ya Muslim Women Writers, nimemchagua mwandishi mmoja tu kutoka Misri, ambaye ni huyu Nawal el Saadawi. Na nimechagua riwaya yake moja tu. Ningeweza kuchagua riwaya tofauti ya mwandishi huyu, au ningeweza kufundisha hadithi za Alifa Rifaat, Distant View of a Minaret.

Nawal el Saadawi si tu mwandishi, bali ni daktari na mwanaharakati maarufu. Amekuwa akipambana na mfumo wa kijamii wa nchi yake, ambao unawakandamiza wanawake. Anazikosoa na kuzipiga vita itikadi zozote, zikiwemo dini, zinazohalalisha ukandamizaji wa wanawake. Nawal el Saadawi ni mama shujaa ambaye anajiamini na hatishiki, kama inavyonekana katika video niliyoweka hapa ambayo nitawaonyesha wanafunzi wangu kama maandalizi ya kujadili The Fall of the Imam.

7 comments:

Khalfan Abdallah Salim said...

Nawal saadawi si wa mwanzo wala wa mwisho kuwa na mtazamo dhidi ya dini na asiwe na uwezo wa kupambanua zaidi ya jamii yake. Tohara ya wanawake ni kongwe kuliko Uislamu au ukiristo au Uyahudi, ni tatizo pana la kijamii. Ni utamaduni wa watu wa jamii husika ambao wenyewe watafanya kila juhudi ili kudumisha hata ikiwa kwa kutumia dini.

Uelewa wa Nawal haujaenda ndani ya mafunzo ya dini yenyewe hususani dini ya Uislam, kwangu maneno yake ni ithibati ya ufinyu wake katika kuchambua dini na kumjua Mungu. Karl Marx alisema zaidi ya hayo...

Mbele said...

Ndugu Khalfan Abdallah Salim

Shukrani kwa ujumbe wako. Tangu tuanze kozi hii, ni wiki nne zimepita, na tunaendelea kusoma na kuchambua maandishi mbali mbali ya hao wanawake waliolelewa katika u-Islam. Ilikuwa ni nia yangu kuweka fursa ya kuchambua mitazamo mbali mbali. Jambo moja ambalo tayari limeshajitokeza vizuri ni namna tamaduni zilivyounganishwa na mafundisho ya dini na pengine kudhaniwa kuwa ndio mafundisho ya dini.

Ndio maana, nimekuwa nikirejea kwenye "Qur'an," ili wanafunzi wapate fursa ya kujionea kama kuna tofauti baina ya dini na tamaduni zinazoelezwa katika fasihi.

Papo hapo, kozi ya chuo kikuu, hata kama inaangalia dini, haifundishwi kwa lengo la kuwavutia watu katika dini yoyote. Inajengeka katika uchambuzi. Kwa msingi huo, nilishaanza kuwaeleza fikra kama hizo za Karl Marx, ambazo alizieleza kwa namna mbali mbali, ila muhtasari aliutoa hivi:

"Religious suffering is, at one and the same time, the expression of real suffering and a protest against real suffering. Religion is the sigh of the oppressed creature, the heart of a heartless world, and the soul of soulless conditions. It is the opium of the people."

NN Mhango said...

Ndugu Mbele,
Huyu bi mkubwa anasema ukweli wazi wazi na kwa lugha rahisi kwa kila mtu kumuelewa. Ni wachache waliofungia akili zao sehemu fulani wanashindwa kumuelewa na kumuona kama hajui anachosema. Mwandishi wa habari nguli wa Uingereza kwenye kitabu chake cha The Life of the Jackal anatukumbusha maneno muhimu kwenye taaluma ya uandishi kuna maneno makubwa mawili kati ya mengi. Kwanza, ni get your facts right. Na pili, ni Tell it as it was akimaanisha usiongeze kwenye ulichokiona. Huyu bi Mkubwa anaeleza uzoefu wake kijijini kwake na akisema kuwa mengi hakujifunza kwenye chuo kikuu. Ni kweli kuwa mila nyingi za kijinga zimejaa kwenye dini ambazo nyingi zake hujionyesha kama mkombozi zikikandia mila za wengine wakati nazo zina mizigo na makando kando yake. Bi Mkubwa anaeleza namna dini zote (kwenye jamii yake ya kijinga kama anavyosema) zilivyomsakama. Nimependa maneno yake kuwa dini- karibi zote- zimejengwa kwenye double standard. Kwangu hii ni kauli kubwa na yenye nguvu inayoonyesha ukweli ulivyo. Kama zimewewza kumuumba Eva mkosefu na mwepesi wa kudanganywa na nyoka hadi akaleta tunda kwa Adam zitashindwa nini kumdhalilisha Eva huyo ambaye kwa bahati mbaya hata maana yake ni Mwanamke ingawa wenzetu kwa kutojua walichokusa wakisema waligeuza sifa ya kijinsia kuwa jina la mtu mmoja. Walishindwa kuelewa kuwa watakuja watu kama sisi tuhoji utimamu wa akili ya Adam aliyedanganywa na kiumbe aliyeonekana kuwa na akili kidogo kuliko yeye tena aliyetoka ubavuni mwake? Hata hili la kutoka ubavuni ni ujinga mtupu uliolenga kumuonyesha mwanamke kama kiumbe dhaifu. Ni kweli dini zote nyemelezi za kimamboleo zinamdhalilisha mwakamke. Kwenye uislam hata kwenye kutoa ushahiidi, ushahidi wa mwanamke ni dhaifu kuliko wa mwanamme. Kwenye ukristo ndiyo usiseme. Mitume wote wa kike wamefutwa isipokuwa wachache kama vile Esther ndiyo waliowasahau kwa bahati mbaya tokana na ukubwa wa kitabu. Nimalizie kwa kuungana na huyu bi mkubwa kuwa anayosema ni mawazo ya kweli na ya kimapinduzi yanayoonyesha uhovyo na upogo wa dini hasa hizi nyemelezi zilizojifanya kukosoa na kutukana mila za wengine wakati nazo zikibeba uchafu ule ule. Ama kweli nyani haoni kundule!

Khalfan Abdallah Salim said...

Nakushukuru Prof. na Mhango kwa michango yenu.

Prof ni maneno mazito sana kumnasibisha mtu kuwa alilelewa katika Uislam hususan Nawal au hata mimi, lililosahihi kwangu ni kuwa 'nimelelewa katija jamii au na wazazi Waislamu'. Waliolelewa na Uislam leo hutowapata, sote ni mchanganyiko wa mafunzo ya dini na tamaduni mbalimbali.

Suala la FGM, kama nilivyosema ni kongwe na kitamaduni zaidi. Mimi familia yangu asili yetu ni Yemen, sijapata kusikia dada yengu yeyote aliyefanyiwa FGM wala yeyote katika familia yetu, upande wa mama na baba. Mimi ninasoma Uislam, hakuna mahala panaponiamrisha na kunitaka niwafanyie bint zangu FGM. Ninao bint watatu na hamna ambaye amefanyiwa au atafanyiwa FGM na sijawahi kufunzwa kuwa ni ibada au jambo la maana kufanya FGM.

Suala la kitambaa cha damu anapoolewa msichana bikira, pia ni la kitamaduni zaidi hakuna mafunzo hayo katika dini ya Uislamu wachilia mbali ndoa za watoto wadogo.

Mhango hawezi kusema kuwa ni katika Uislam pekee kuwa pepo ya mtoto wa kiislamu ipo katika ridhaa ya mama yake kama ambavyo hawezi kusema kuwa Uislam hauruhusu mwanaume kumpiga magumi au kibao mkewe. Kwa nini? Anaimba wimbo ule ule 'Dini zote ni kandamizi juu ya wanawake.'Mbele said...

Ndugu NN Mhango

Shukrani kwa mchango wako. Ninapenda blogu yangu iendelee kuwa uwanja wa kuchokoza fikra, kubadilishana mawazo na mitazamo, kugonganisha fikra, kwa uhuru kabisa. Kuhusu Dr. Nawal Saadawi, tunamwelewa kuwa amekulia katika jamii ya aina fulani na amepitia na ameshuhudia machungu, na ndiyo anayoyaongelea tena na tena katika maandishi, hotuba, na mahojiano. Ananikumbusha wanawake wengine, kama vile Wafa Sultan wa kutoka Syria na Ayaan Hirsi Ali wa kutoka Somalia.

Ninavutiwa na uchambuzi wako wa hizi unazoziita dini nyemelezi. Ingawa mimi ni muumini wa dini mojawapo, ninafurahia jinsi unavyozirarua. Ni muhimu kwa waumini kusikia mashambulizi kama hayo, ili waweze kutafakari vizuri kuhusu kile wanachoamini, wasiwe wanafuata kama vipofu. Siamini kama Mungu anatutaka tuwe waumini vipofu. Ingekuwa hivyo, akili alitujaalia ya nini?

Kwa hivyo, nakushukuru, na nakuomba usisite kuendelea kuwasha moto na kuchochea fikra hapa ukumbini pangu.

Mbele said...

Ndugu Khalfan Abdallah Salim

Shukrani kwa ujumbe wako. Umefanya vyema kufafanua dhana ya kulelewa katika u-Islam na kulelewa katika familia au jamii ya wa-Islam. Ninaona kuwa ni ufafanuzi muafaka.

Hoja yako kuhusu tamaduni tunaafikiana kabisa. Kwa mfano hii jadi ya kuweka kitambaa kitandani ili kuinasa damu ya bikira na kisha kukionyesha hadharani, ilikuwepo katika baadhi ya makabila ya Afrika tangu zamani, bila uhusiano wowote na u-Islam.

NN Mhango said...

Bwana Khalfan sijui kama umenielewa. Sijaongelea ridhaa ya mama na mtoto na hizo pepo upepo unaozoongelea. Nikizama kwenye pepo za dini nyemelezi wengi mtachukia. Kwani mimi siamini kama peponi -kama baadhi wanavyoaminishwa ni danguro ambapo mwanaume atapewa wanawake kibao. Wala siamini kwenye pepo za kwenda kuimba milele kama ndege. Huwa nashangaa pepo zeni kwa vile kwa watu wasio wapenzi wa ngono au nyimbo tunaachwa nje. Hayo tuyaache. Nadhani kama ungeelewa nilichoongelea basi ungegusia lau kwenye dhana ya kuumbwa mwanamke toka ubavuni mwa mwanaume kana kwamba Mungu alikuwa ameishiwa. Pia ungegusa japo kidogo kwenye dhana nzima ya dini mamboleo kuja na kutukana mila zetu wakati nazo zimesheheni uchafu. Huwa naamini kama binadamu wote ni sawa basi na njia zao zote ni sawa -zina mazuri na mabaya. Kimsingi, nilitegemea mwenye kuelewa akanushe hii aina mpya ya ukoloni wa kimila ambapo mila fulani hata ardhi huonekana takatifu kana kwamba kuna ardhi iliyolaaniwa. Huwa napata tabu kuamini kuwa jangwani kunaweza kuwa patakatifu kuliko Afrika yenye kila aina ya neema bila kusahau watu wake wakarimu lakini wajinga kidogo wanaopokea kila upuuzi bila kuuhoji wala kuutimlia mbali. Nimefurahi kusikia kuwa asili yako ni Yemen. Umenikumbusha jamaa zangu wengi wenye asili ya Mashariki ya kati wanavyotangaza dini kwa mkono wa kulia na kubagua waswahili kwa mkono wa kushoto. Ukienda Tanga utakuta vibinti vingi virembo vimeolewa na machotara lakini hapa hapo hakuna vibinti ima vya kiarabu au chotara vimeolewa na waswahili. Hapa ndipo utagundua ukandamizaji wa mwanamke. Anyway, leo sisemi mengi. Hata hivyo, mengi nayajadili kwenye kitabu changu kipya ninachomalizia cha THE NEED FOR DECOLONIZING EDUCATION. Hata kwenye kingine ninachotegemea kutoka hivi karibuni cha PSALM OF THE OPPRESSED nimeyafutu masuala haya kwa utuo.
Bwana Mbele nakushukuru kwa kugeuza blog yako aina nyingine ya chuo binafsi cha kunolea na kubadilishana mawazo.