Friday, May 23, 2014

Tunawazia Kwenda Tena Montana Kuonana na Mzee Patrick Hemingway

Mwishoni mwa mwezi Aprili, mwaka jana nilienda Montana kuonana na Mzee Patrick Hemingway. Huyu ni mzee wa miaka 86 sasa, na ndiye mtoto pekee aliyebaki wa mwandishi maarufu, Ernest Hemingway. Niliandika kifupi kuhusu safari hii katika blogu hii.

Tulisafiri watu watano. Wanafunzi wangu ambao wanaonekana kushoto kabisa pichani, baba ya huyu mwanafunzi aliyevaa kaptura, na rubani wa ndege ya huyu baba mzazi. Mzazi wa mwanafunzi na rubani wake hawamo pichani. Mzee anayeonekana pichani ndiye Mzee Patrick Hemingway. Hapa tuko nje ya nyumba yake iliyoko katika mji mdogo wa Craig. Maskani yake hasa hasa, kwa miaka mingi, ni katika mji wa Bozeman, Montana.

Wanafunzi hao wawili ni kati ya wanafunzi 29 wa chuo cha St. Olaf, ambao nilienda nao Tanzania mwezi Januari, 2013, kuwasomesha kuhusu maandishi na safari za Hemingway katika Afrika Mashariki, miaka ya 1933-34 na 1953-54.

Wakati tukiwa Tanzania, wanafunzi hao walinisikia nikiongelea habari za Mzee Patrick Hemingway, kwamba ni mtoto pekee aliyebaki wa Ernest Hemingway, na kwamba nina mawasiliano naye kwa simu, na kwamba ninapangia kwenda Montana kuonana naye.

Huyu mwanafunzi aliyevaa kaptura alisema bila kusita kuwa baba yake angewezeza kutupeleka Montana kwa ndege yake. Hatimaye, siku tuliyopanga, alikuja na ndege yake hapa Minnesota, akitokea nyumbani kwake Ohio. Tulipokutana, nilikuja kufahamu kuwa baba huyu sio tu shabiki wa maandishi ya Hemingway, lakini pia ni msomaji hodari wa vitabu, vya fasihi ya ki-Ingereza, ingawa shughuli zake kimaisha ni biashara.

Kama nilivyogusia kabla, Mzee Patrick Hemingway aliwahi kuishi Tanzania kwa miaka yapata 25 akifanya shughuli kadhaa, ikiwemo ya utalii na kufundisha chuo cha Mweka. Alitukaribisha vizuri sana, tukaongea naye kwa masaa mengi. Huyu mwanafunzi mwingine ni mpiga picha na video, na alirekodi mazungumzo hayo, ambayo ni hazina kubwa. Yana mengi kuhusu maisha, maandishi na mitazamo ya Hemingway, na pia habari nyingi kuhusu waandishi wengine wa nyakati za Hemingway, hasa wale waliokuwa na mawasiliano au uhusiano na Hemingway.

Tuliwazia kwenda tena Montana huu mwezi Mei, kama mwaka jana, lakini kutokana na mimi kuumwa tangu mwanzo wa mwaka, hatujaweza kufanya hiyo safari. Tuna matumaini ya kwenda baada ya miezi michache kuanzia sasa, nitakapokuwa nimepona kabisa, Mungu akipenda.

Kuna mengi bado ya kuongea na Mzee Patrick Hemingway. Jambo moja muhimu ni maisha yake Tanzania. Hilo ni suala ambalo napenda kulifuatilia sana, hasa nikizingatia kuwa mwaka 1954, Hemingway mwenyewe alikwenda hadi Iringa kumtembelea mwanao Patrick akakaa yapat5a wiki tatu. Hiyo ni habari ambayo nataka kuifuatilia kwa undani. Hatujui, huenda Hemingway aliandika hiki au kile kuhusu Iringa, kwani hakuwa mtu aliyekaa mahali asiandike mambo ya mahali hapo. Suala hili linahitaji kufanyiwa utafiti wa kina katika hifadhi ya maandishi ya Hemingway yaliyoiko Cuba na pia maktaba ya John F. Kennedy kule Boston. Mungu akinijalia uzima, nategeme4a kwenda huko miaka ya usoni.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...