Nimekuwa na hamu sana ya kupiga picha za ndege, lakini nimegundua ugumu wake. Ndege ni wajanja sana, wepesi kurukia tawi jingine unapotaka kuwapiga picha, au kuruka na kwenda zao. Lakini jana niliwaona ndege wawili wakubwa wakitembea pamoja. Sikuwa nimechukua kamera. Leo nilitoka tena, na ndege wale walikuwa sehemu ile ile ya jana wakitembea. Hao ingawa wanatembea, sio vigumu kuwapiga picha, nami nimepiga picha kadhaa. Kamera yangu ina "zoom" nzuri; kwa hivi sio lazima kuwasogea sana. Sina uzoefu na kamera hii; bado ninajifunza namna ya kuitumia katika vipengele vyake vyote.
Nmeamua kuwatafuta ndege na kuwapiga picha kutokana na kuvutiwa na picha anazopiga rafiki yangu, Profesa Bill Clemente wa Peru State College, Nebraska. Navutiwa sana na picha zake, na huwa nashangaa hao ndege anawawezaje. Picha zake nyingi huziweka katika Facebook. Hapo ndipo ninapoziona na kuzifurahia. Labda siku za usoni nami nitakuwa na uwezo kama wake.
No comments:
Post a Comment