Tuesday, May 27, 2014

How to Win Friends & Influence People

Kwa miezi kadhaa, labda  miaka, nimekikumbuka kitabu maarufu kiitwacho How to Win Friends & Influence People (New York: Pocket Books, 1982) kilichoandikwa na Dale Carnegie, na kuchapishwa mara ya kwanza mwaka 1936.

Imetokea tu kuwa hiki ni kimoja ya vitabu ambavyo vimetawala akili yangu kwa miezi kadhaa. Nimekumbuka jinsi katika ujana wetu tulivyokipenda kitabu hiki. Hapa Marekani, nimekuwa na kitabu hiki kwa miaka kadhaa. Kimekuwa kikinikumbusha ujana wangu.

Nilikuwa mwanafunzi Mkwawa High School, Iringa, miaka ya 1971-72, na hapo ndipo nilipokisoma kitabu hiki kwa mara ya kwanza. Wanafunzi wa wakati ule tulikuwa tunapenda sana kusoma vitabu. Wengi walisoma vitabu vya waandishi kama James Hadley Chase na Ian Fleming. Kitabu cha How to Win Friends & Influence People kilikuwa kimojawapo.

Nina hakika, kwa vile mimi sasa ni mwalimu wa ki-Ingereza, tabia hii ya kusoma sana vitabu vya ki-Ingereza ilichangia sana katika kutufanya tuifahamu na kuimudu vizuri lugha hiyo.

Kitabu cha How to Win Friends & Influence People kina mawaidha mengi ya kusisimua kuhusu namna ya kuhusiana na watu katika hali na mazingira mbali mbali. Kwa mfano, kama wewe ni kiongozi, unapaswa ufanyeje katika mahusiano yako na wale unaowaongoza ili wahamasike kufanya yale unayotaka wafanye, ili wakukubali na kukupenda.

Dale Carnegie ananukuu matokeo ya tafiti mbali mbali, kuthibitisha hoja zake. Moja ulionigusa ni utafiti uliofanywa na Carnegie Institute of Technology, utafiti uliothibitisha kuwa "even in such technical lines as engineering, about 15 of one's financial success is due to one's technical knowledge and about 85 percent is due to skill in human engineering--to personality and the ability to lead people." (uk. xiv)

Hapo utaona jinsi wa-Tanzania walivyopotoka wanapong'ang'ania kuwa vijana wao wasome masomo ya sayansi, bila kuzingatia umuhimu masomo ya elimu jamii kama vile fasihi na saikolojia. Jamii yetu imegubikwa na ujinga, na hapo ndipo ninapowajibika kusema kuwa utaratibu ule ambao nimeuona hapa Marekani, kwenye vyuo kama hiki chuo ninapofundisha, utaratibu wa kumfanya kila mwanafunzi asome masomo ya sayansi na ya elimu jamii, ni utaratibu wa kufaa sana. Hii huitwa "liberal arts education." Ni elimu inayomkuza mwanafunzi kiakili kwa namna mbali mbali, asiwe na ufinyu wa fikra na mtazamo.

Viongozi wengi hawajui hayo, na badala yake wanawakandamiza wale wanaowaongoza au wanamwaga mbwembwe ili waonekane wao ni mabosi na waogopwe. Kitabu hiki kinaelezea mbinu za kuwafanya watu waupokee msimamo wako katika masuala mbali mbali, sio kwa shinikizo bali kwa staili yako ya kuongea nao na kujieleza.

Ingawa hasemi hivyo wazi wazi, mwandishi ametumia vizuri sana taaluma ya saikolojia. Kukisoma tena kitabu hiki wakati huu, nimeona wazi kabisa kuwa matatizo mengi ya uongozi na mahusiano katika jamii yetu yangetoweka iwapo tungezingatia mawaidha yake.

Dale Carnegie aliandika vitabu vingine kadhaa. Leo nimeamua kukitaja hicho kimoja tu, ambacho kinavuma sana ulimwenguni, na kimeshauzwa nakala zaidi ya milioni 15. Cha zaidi ni kuwa kimeandikwa kwa lugha ya kuvutia. Ni mfano mzuri wa uandishi bora.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...