Friday, May 16, 2014

Vitabu Vya Kutuendeleza Kimaisha

Katika ujumbe wangu wa jana, kuhusu nia yangu ya kuandika kitabu kingine kufuatia kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, nilisisitiza umuhimu wa kujiamini. Hilo ni fundisho linalotolewa katika vitabu vingi, labda niseme vyote, vinavyojadili suala la maendeleo ya mtu binafsi, kumweka katika hali ya kufanikiwa.

Pamoja na kujiamini, mtu unapaswa kuangalia uwezo wako na kuutumia, badala ya kukaa na kulalamika kuwa huna hiki au kile, au kuwasikiliza watu wanaojaribu kukukwamisha au kukukatisha tamaa. Hakuna sababu ya kuwa na watu kama hao, bali ambatana na watu wanaosonga mbele na wana mtazamo wa kusonga mmbele.

Jana hiyo, nilitaja kitabu kimojawapo ambacho ni maarufu, kiitwacho The Power of Positive Thinking. Sijui ni wa-Tanzania wangapi wanakifahamu kitabu hiki, wamekisoma, au wanakisoma. Kama wapo, watakuwa ni wachache sana, kama vile kijana Meshack Maganga wa Iringa, ambaye habari zake naziona kwenye mitandao kama Facebook.

 Kwanza, kuna suala la lugha. Wa-Tanzania wamepuuzia ki-Ingereza, kwa visingizio mbalimbali. Kwa hivi, ni lazima elimu iliyomo katika vitabu hivi inawapitia mbali; wanabaki gizani, wakiwa na fikra na mitazamo ya kuwakwamisha. Pili, kwa ujumla, wa-Tanzania hawana utamaduni wa kununua na kusoma vitabu. Hilo ni janga la Taifa.

Kwa miaka kadhaa nilikuwa nimekisikia kitabu cha The Power of Positive Thinking. Nimesoma baadhi ya vitabu vya aina hiyo, lakini sio hicho. Hivi karibuni, nilipolazwa kwa wiki sita katika hospitali ya Abbott Northwestern ya mjini Minneapolis, nilikwenda na nakala yangu ya kitabu hiki, nikawa najikongoja kukisoma kidogo kidogo, kutokana na hali ya kuumwa na kuwa kitandani siku zote.

Baada ya kuja kupumzika nyumbani, ingawa naendelea na matibabu, nimemaliza kukisoma kitabu hiki. Kina mafundisho mengi na ushauri wa thamani. Jambo moja ambalo limenikaa sawa sawa akilini ni kuwa fikra na mtazamo ulio nao, ndio msingi wa kufanikiwa au kutofanikiwa. Ukiwa na fikra za kutojiamini, au fikra kwamba hiki au kile huwezi, basi hutaweza. Utabaki hivi hivi ulivyo.

Fikra na mtazamo ndizo zinakuongoza au kukukwamisha maishani. Kama huna mafanikio, ni wewe mwenyewe unasababisha hali hiyo. Tukirudi Tanzania, tunaona matatizo makubwa. Wengi hawajiamini; hawaelewi kuwa kufanikiwa au kutofanikiwa ni juu yao, badala yake wanakuja na visingizio au wanatafuta wachawi.. Utawaona wanaenda kwa waganga wa kienyeji, kwa mfano. Au utawasikia wakitafuta wa kumlaumu, kama vile wa-Islamu wengi wa Tanzania wanavyoaminishwa kwamba tatizo ni "Mfumo Kristo."

Basi, napenda kusisitiza kuwa ni muhimu tujibidishe kusoma vitabu mbali mbali vinavyotufungua macho na akili ili tuwe watu wa kujiamini, kutambua uwezo wetu na neema tulizojaliwa; tuzitumie juhudi yote ili tufanikiwe. Ndio maana katika ujumbe wangu wa jana, nilielezea kwa kujiamini azma yangu ya kuandika kitabu kingine kufuatia kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nilitamka bila kusita kuwa hiki kitakuwa kitabu bora kabisa, kuliko hiki kingine, ingawa ni maarufu miongoni mwa wasomaji.

3 comments:

Lyimo said...

Nashukuru kwa kuwa wazi kugusia kati ya matatizo lukuki yanayoikabili ya jamii yetu y kitanzania na Bara nzima la Afrika kwa ujumla...

Nimesoma hichi kitabu na pia nimekielewa, ujumbe na maarifa niliyoyapata kutoka katika kitabu hichi kinanisaidia katika kupambana na mazingira yangu kwa ujumla na kuongeza kwa pamoja ufahamu,juhudi zangu na maarifa ya ubunifu wangu binafsi maisha yangu yanaendele vizuri

Anonymous said...

Si uandike hicho kitabu kwanza badala ya kuandika kwa mdomo prof? Actions speak louder than words.

Mbele said...


Ndugu Lyimo, shukrani kwa ushuhuda wako. Umeeleweka vizuri.

Anonymous, kauli yako inahitaji maelezo au mijadala katika nadharia ya uandishi. Hapa nitajibu kifupi tu.

Kama nilivyosema kabla, juzi hapo, mawazo ya kitabu cha pili nilianza kuwa nayo miaka mingi iliyopita na pia wasomaji wa kitabu kilichotangulia walishauri niandike kingine, tangu pale mwanzo.

Vile vile nilisema kuwa tayari nilishaandika sura kadhaa. Ni Insha fupi fupi, na kilichobaki ni kuongezea tu.

Kwa hivi, sio kwamba nimekurupuka tu na wazo la hiki kitabu kingine.

Kitabu huanzia mawazoni, na hata kukamilika, kabla hujakiweka kwenye karatasi. Hapo ndipo suala la nadharia ya uandishi inapoingia. "Kitabu" huwa kichwani mwa mwandishi kabla hakijawa kitabu tunachokiona sisi wasomaji.

Kwa hivi, ni kuwa sioti ndoto tu, ingawaje, kwa mtazamo mwingine, ndoto ni muhimu.

May 17, 2014 at 9:59 AM

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...