Wednesday, May 21, 2014

Biashara, Ujasiriamali, na Vitabu

L
Nina vitabu kadhaa kuhusu biashara na ujasiriamali. Mara moja moja huvipitia. Ninajielimisha katika uwanja wa ujasiriamali kwa mategemeo kuwa nami nitakuwa mjasiriamali. Ninavutiwa na ujasiriamali jamii, ambayo ni tafsiri yangu ya "social entrepreneur." Mjasiriamali jamii hawanii kujitajirisha yeye binafsi kwa fedha, bali hutafuta hizo fedha ili zimwezeshe kutoka mchango wa manufaa kwa jamii.

Kitabu kimojawapo ambacho nakipenda sana na nakipendekeza kwako msomaji wa blogu hii ni  Leaving Microsoft to Change the World: An Enterpreneurs Odyssey to Educate the World's Children (New York: HarperBusiness, 2007) kilichoandikwa na John Wood.

Wakati huu, nasoma kitabu kiitwacho Reengineering the Corporation: A Manifesto for Business Revolution (New York: Harper Collins Publishers, 1993) kilichoandikwa na Michael Hammer na James Champy.

Reengineering the Corporation ni kitabu maarufu sana. Nilikinunua miaka michache iliyopita baada ya kusoma kauli za wataalam zilizoonesha ubora wake. Siku chache zilizopita, niliamua kukisoma. Ninaamini kama vile ingekuwa dini, umuhimu wa kusoma vitabu, hasa kuhusu nyanja ambazo mtu huna ujuzi nazo. Inakupanua akili na kadiri unavyosoma vitabu unakuwa tajiri wa fikra, mawazo, na mitazamo kuliko yule asiyesoma. Ni lazima tukubali hilo.

Reengineering the Corporation ni kitabu kinachofundisha jinsi makampuni na mashirika yanavyopaswa kujibadilisha daima ili kujipatia ufanisi zaidi na kuweza kukabiliana na hali halisi ya utandawazi na ushindani. Hakuna namna nyingine bali kujibadilisha kwa hali zote na muda wote, vinginevyo shirika au kampuni inajichimbia kaburi.

Mambo yanayohitaaji mabadiliko ni pamoja na muundo wa shirika au kampuni, mtindo wa utoaji huduma, mahusiano miongoni mwa wafanyakazi, na baina ya wafanyakazi na wateja, pia matumizi ya tekinolojia mbali mbali, kama vile "information technology." Ni muhimu kutong'ang'ania jadi na mazoea. Lazima kufanya mabadiliko mapema kwani hali halisi ya dunia, wateja, na ushindani hubadilika daima na haitabiriki.

Ningekuwa mfanyabiashara ningefanya kila juhudi kujielimisha kwa kusoma vitabu vya aina hii, kwani elimu ni mtaji muhimu.


No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...