Tuesday, June 7, 2011

Mwaliko Nyumbani kwa Wateja Wangu

Jana jioni nilikuwa nyumbani kwa familia inayoonekana katika hii picha. Ni familia ya Shannon Gibney, mwandishi chipukizi ambaye tayari ni maarufu.

Miaka michache iliyopita, Shannon Gibney alisoma kitabu changu cha Africans and Americans, akaandika mapitio katika Minnesota Spokesman Recorder, kama nilivyosema hapa.

Siku chache zilizopita alinialika nyumbani kwake kwa chakula cha jioni, tukapanga hiyo tarehe ya jana. Aliniambia kuwa mume wake, ambaye anatoka Liberia, na bado ni mgeni hapa Marekani, amekuwa akisoma kitabu changu.

Nilifurahi kukutana na familia hii. Kwa zaidi ya saa mbili nilizokuwa nao, maongezi yetu yalihusu masuala niliyoongelea katika kitabu, yaani tofauti za tamaduni za wa-Marekani na wa-Afrika. Wote wawili wanakifahamu vizuri sana kitabu hiki, na walikuwa wananikumbusha mengi, ingawa mimi ndiye mwandishi.

Huyu bwana aliezea mshangao wake kwa jinsi maelezo ya kitabu hiki yanavyofanana na hali ya Liberia, ingawa mimi mwandishi sijafika kule. Niliguswa na furaha yake kwamba niliyoandika yamemwelewesha mambo ya wa-Marekani ambayo yalikuwa yanamtatiza. Nami nashukuru kwa hilo.

Familia hii ilinikarimu vizuri sana, nami nimebaki nashangaa kwa jinsi uandishi wa kitabu unavyoweza kukujengea urafiki na watu kiasi hicho.

11 comments:

emu-three said...

Unajua profesa, kitabu kinasimama badala ya mtu, ndio maana wanasema mwandishi wa vitabu faki, anakufa kiwiliwili tu, lakini kifikira tupo naye daima
Ndio maana walipokuona na kukumbuka kitabu chako, walijua walikuwa nawe siku zote...au nimekosea profesa!

Yasinta Ngonyani said...

Hakika asiye kisoma hiki kitabu na akitafuta na ataelewa mwenyewe...

Mbele said...

emu-three, shukrani kwa ujumbe wako. Dhana kwamba mwandishi wa vitabu hafi (nadhani ndivyo ulivyotaka kuandika) ni ukweli, na sehemu mbali mbali za dunia ukweli huu unatamkwa.

Kuandika kama njia ya kujihakikishia maisha yasiyo na mwisho (ki-Ingereza wanasema "immortality") ni dhana inayofahamika sana. Katika hadithi ya kale kabisa ya Gilgamesh, ambayo iliandikwa miaka labda elfu sita iliyopita, Shujaa Gilgamesh anafanya mkakati wa kwenda sehemu ambapo ataweza kuandika habari zake ili zidumu baada ya yeye kufariki.

Hata leo, tunajionea sisi wenyewe kuwa watu kama Shakespeare, Milton, Mwana Kupona, Shaaban Robert au Mwalimu Nyerere bado wako, na wataendelea kuwepo.

Basi nami najikongoja niishi milele :-)

Shukrani Dada Yasinta. Nawe kwa vile ni mwandishi chipukizi ila makini, napendekeza utuandikie mambo ya Sweden, kama mimi nilivyoandika ya Marekani. Utakuwa umetupanua upeo na utaturahisishia mahusiano yetu na hao wenzetu.

John Mwaipopo said...

ngoja niandike 'kiudaku-udaku'

yasinta deal hilo!!!

Mbele said...

Ndugu Mwaipopo, ajabu ni kuwa hiki kitabu changu kinachoongelewa hapo, ingawa kinawagusa watu kwamba kinasema ukweli, lakini ajabu ni kuwa kimeandikwa kiudaku udaku.

Nilijifunza kutoka kwa mwandishi Ernest Hemingway, ambaye aliamini kuwa ili kitabu kionekane na wasomaji kuwa kinasema ukweli, sio lazima uandike ukweli kama tunavyoelewa dhana ya ukweli. Alisema kuwa hata kama unayoandika hayana uthibitisho wa kitaaluma, wewe yaandike kwa namna ya kumfanya msomaji ajisikie anachosoma ni ukweli.

Kwa maana hiyo, kwa kiasi fulani kitabu changu ni udaku orijino :-)

Anonymous said...

Nimekisoma hakina chochote kipya, ni kama vitabu vingine.

Mbele said...

Anonymous, shukrani kwa ujumbe wako. Wewe inaonekana uko anga za juu kutuzidi sisi wengine. Kwa hivi, nakuomba mambo kadhaa, utusaidie sisi tusio na upeo kama wako.

1) Nilipoandika kitabu hiki, nilikuwa nimeshafanya utafiti na sikuona kitabu kilichoongelea masuala niliyotaka kuongelea, kwa mtindo nilioona unafaa. Huo ni wajibu kwa mtu anayeandika kitabu, yaani kuleta jambo jipya kwa namna moja au nyingine.

Tena nilikuwa sio peke yangu bali na wengine wengi tukiendesha program za vyuo vikuu hapa Marekani, za kupeleka wanafunzi kwenye nchi za Afrika, na ikaonekana kuwa hatuna kitabu kinachofaa kwa maandalizi yanayohusu tofauti za tamaduni. Kutokana na vyuo hivi kutambua shida hiyo ndio nikahamasishwa niandike kitabu cha aina iliyohitajika.

Kama unataka kujua baadhi ya vyuo hivyo, ni Chicago, Grinnell, Macalester, Colorado, Carleton, St. Olaf, Coe, Monmouth, Beloit, na Lake Forest. Sasa tuambie hivi vitabu vingine unavyosema vipo ambavyo ni sawa na changu ni vipi. Sisi hatuvijui, na ukitutajia tutavitumia. Wewe unaonekana una upeo mkubwa kuliko sisi tuliohangaika na bado tunahangaika kwenye hivi vyuo.

2) Kwa vile wewe unaonekana uko kwenye upeo wa juu kutuzidi, unachotakiwa kufanya ni kuandika kitabu bora zaidi kuliko hiki tunachoongelea.

3) Kama huna muda wa kuandika hicho kitabu bora kwa sasa, na unasema umesoma kitabu changu, basi angalau andika mapitio uchapishe hata kwenye gazeti. Kwa kufanya hivyo utaonyesha jinsi ulivyo makini, na uweke jina lako kamili ili umma uweze kukutafuta kwa ajili ya kupata elimu zaidi.

4) Ukipitia blogu zangu mbili, utaona kuwa naeleza kwa uwazi ni jumuia zipi, taasisi zipi, vyuo vipi ambako kitabu changu kinatumika, hasa kwa vile wanawasiliana nami. Hakuna siri. Kwa hivyo, ukiwa na nia njema ya kuwasaidia binadamu kama ninavyojaribu kufanya mimi, unatakiwa uchangie kwa kuwapelekea orodha ya hivi vitabu unavyosemea. Kidole kimoja hakivunji chawa. Na ni hivyo hivyo kwa vitabu. Kama viko vitabu vingine kuhusu suala fulani, ni wajibu kuvisoma vyote. Kwa hivi, unao wajibu mzito hapo wa kuvitaja hivi vingine.

Kwa kumalizia, ni kwamba nimekuwa nikiandika kitabu kingine kuhusu masuala ya aina ile ile ya kitabu tunachoongelea. Karibu nitamaliza, na nahisi kitakuwa maarufu zaidi. Habari ndio hiyo, wakati tunangojea kitabu chako wewe mtaalam wetu.

Michuzi said...

Profesa,
Nafarijika sana kusoma makala zako, japo ukweli sijakisoma hicho kitabu tajwa hapa. Nnachotaka kusema ni kwamba wewe ni mmoja wa wachache wanaopeperusha bendera ya watu kujisomea, bendera ambayo imenywea mlingotini kutokana na uhaba wa upepo wa wasomaji vitabu, mbadala ukiwa mtandao. Mie nasoma sana vitabu na maandiko mbalimbali, ila nasikitika watoto wangu hata mmoja sijamuona akijisomea, achilia mbali mambo ya masomo. Nyumbani nina vitabu lukuki kabatini, lakini haviguswi. Wao ni Luninga na majarida ya habari za starehe na za vijana tu. Sijui tunaelekea wapi kwani najaribu kuwashawishi wasome vitabu, lakini wanakuwa wagumu. Profesa hebu tupe tathmini yako ya hili swala, ambapo mtandao umekuwa 'kitabu' kwa vijana wetu, na nyie mnaojikunja kutuletea vitabu tujisomee jasho lenu litakwenda vipi?

Mbele said...

Mheshimiwa Michuzi,

Kwanza samahani sikupata fursa ya kujibu mapema ujumbe wako. Nilikuwa safarini Chicago jana nzima. Leo ndio napata wasaa wa kuandika hapa.

Suala unaloibua ni zito sana. Huku Marekani kuna wazazi ambao hawana televisheni majumbani, kwa hoja kuwa ina athari mbaya kwa watoto. Wazazi wengi ingawa wana televisheni majumbani wanawapangia watoto muda wa kuangalia televisheni, na vipindi vya kuangalia. Wazazi hao wanafuatilia ili kuhakikisha kuwa muda mwingine watoto wanafanya kazi za shule, kama vile kusoma vitabu na kufanya mazoezi au kuandika yale ambayo walimu wameagiza.

Jambo moja ambalo nadhani linaweza kusaidia kujenga utamaduni wa kusoma vitabu miongoni mwa watoto wetu ni kuanzishwa kwa klabu za usomaji vitabu. Ninashawishika kusema kuwa endapo watu wetu maarufu ambao hata watoto wanawahusudu, kama vile hao tunaowaita mastaa, wakianzisha klabu za vitabu, nadhani watawavutia watoto.

Hebu fikiria, kwa mfano, Lady Jay Dee aanzishe klabu ya vitabu, au Hashim Thabit, Kanumba, Ali Kiba, Afande Sele, Sugu, Masanja Mkandamizaji, na kadhalika. Ninahisi mastaa wetu wanaweza kuwavuta watoto na vijana kwenye usomaji wakifanya hivyo.

Hao mastaa wakiwa na vipindi vya usomaji katika televisheni, na wawe wanazunguka pia nchini, kwenye maktaba, kwa mfano kwenye maktaba, wanaweza kuwavuta watoto na vijana. Nimeona hayo hapa Marekani. Kuna rafiki yangu moja anaitwa Floyd Stokes, m-Marekani Mweusi, kule Pennsylvania ambaye anafanya shughuli hizo za kuhamasisha watoto kusoma, na zinafanikiwa vizuri sana. Tovuti yake ni hii hapa.

Mcharia said...

Mimi nitakipataje hicho kitabu???

Mbele said...

Ndugu Mcharia, shukrani kwa ulizo lako. Vitabu vyangu vinapatikana sehemu mbali mbali, kama nilivyoeleza hapa.