Tuesday, June 28, 2011

Naenda kwa wa-Nyakyusa

Hivi karibuni, nitakuwa Tanzania na wanafunzi katika programu ya masomo inayoendeshwa na vyuo kadhaa vya Marekani kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kabla ya kuwafikisha Chuo Kikuu Dar es Salaam ambapo watasoma kwa muhula mmoja, nitakuwa nao maeneo ya nyanda za juu, hasa Iringa. Lakini, katika kupanga safari hii, nimeamua kuwafikisha hadi Mbeya na Ziwa Nyasa, wakaone na kujifunza. Iringa naifahamu vizuri, ila Mbeya nilipita tu mara moja, miaka ya mwisho ya sabini na kitu.

Wakati nangojea kwenda Mbeya, nawazia utamaduni wa wa-Nyakyusa. Mimi kama mtafiti, nimesoma kiasi kuhusu masimulizi yao ya jadi. Ninakumbuka maandishi ya watafiti kama Monica Wilson. Nina kitabu kiitwacho The Oral Literature of the Banyakyusa, kilichoandikwa na Christon S. Mwakasaka. Nadhani nilikinunua Dar es Salaam, nikawa nakisoma mara moja moja.

Lakini wakati huu ninapongojea safari ya Mbeya, kitabu hiki kinanivutia kwa namna ya pekee. Kina hadithi za jadi, lakini vile vile nyimbo na tungo zingine zinazoelezea mambo ya hivi karibuni ya historia na siasa u-Nyakyusa na Tanzania kwa ujumla.

Natafuta maandishi mengine ya kuongezea ufahamu wangu. Kwa hilo naweza kusema nimeathiriwa na wa-Marekani. Wao, kabla ya kusafiri, wana hiyo tabia ya kusoma habari za sehemu waendako. Ni jadi nzuri. Kusafiri kunatupanua akili, lakini kusoma habari za tuendako kunautajirisha zaidi ufahamu wetu.

9 comments:

John Mwaipopo said...

Aah sijui nianzie wapi! Nilikisoma kitabu hiki choote mwaka 1994 au 1995. Nilikisoma wakati kizungu changu kina makorongo makubwa kuliko makorongo ya leo. Kilikuwa nyumbani kwetu. Nilimuazima jamaa yangu akiitwa Emanuel Mwambelo pale Mbeya (Day) Secondary School. Hakukirejesha hata leo. Ningetamani nikisome tena.

Mbali na hadithi na hekaya za wanyakyusa ndani ya kitabu hiki, pia kuna simulizi ndogo ya asili ya wanyakyusa na jina 'nyakyusa'. Kwa kifupi kulikuwa na mzee alikuwa na wake wengi. Miongoni mwa wake zake mmoja aliitwa 'kyusa'. Watoto wa mzee huyo, ambao walikuwa wengi kwa kuwa alikuwa na wake wengi, walitambuliwa kwa majina ya mama zao. Hivyo watoto wa mke aliyeitwa kyusa waliitwa ‘watoto wa kyusa', that is, abana ba kyusa/banya kyusa hence the name banyakyusa, simplified in kiswahili as 'WANYAKYUSA'. Kuna stori nyingi, ila nazikumbuka mbili ambazo zilinisisimua sana. Moja ikiitwa KAMPAPABUNGA THE IMPOSTOR, nyingine TWO CUNNING MEN.

Wazungu karibuni Mbeya, karibuni kwa wanyakyusa

Mbele said...

Ndugu Mwaipopo,

Ndaaga fiijo :-)

Teh teh teh teh :-)

Nilijua tu kuwa nikiandika makala hii, nitawatoa wa-Nyakyusa msituni walikojichimbia.

Huyu mwandishi, Christon Mwakasaka, tulifundisha wote Chuo Kikuu Dar. Yeye alianza kufundisha kwenye mwaka 1974, na mimi nilianza 1976. Kitabu hiki alikiandika wakati ule.

Lakini miaka michache baadaye alienda Zambia. Kwa miaka mingi sasa sijui habari zake.

Ni kweli kitabu chake kinagusa hisia za msomaji na ni muhimu. Sina hakina, lakini huenda nilikinunua Tanzania Publishing House. Labda kuna wadau Dar wanaweza kupita hapo kuangalia.

Wanyakyusa kaeni mkao wa kula. Wazungu nawaleteeni :-)

John Mwaipopo said...

kuna mtu ana taarifa za Christon Mwakasaka. ntamtafuta.

Christian Sikapundwa said...

Karibu sana Profesa Jijini Mbeya,Nimetoka huko Juzi nilikuwa na shughuli za Harusi ya Kijana wangu Mbalizi hata hivyo kulitokea na sintafahamu fulani haikufanikiwa.

Ni matumaini yangu ukienda na wanafunzi hao kuliona Ziwa Nyasa unaweza ukafika Nyumbani Litembo ?,mie niko nimerudi Songea.'Contact' zangu ni 0756 282368.Karbu sana Unyakyusani.Pia nakutakia safari njema,Karibu Tanzania.

Anonymous said...

Prof. Mbele

Hupeleki wazungu Mbeya.... kwani kule ni kwao - sema unawasindikiza au kuwarudisha kwako (lol). Sijabahatika kusoma kitabu cha Mwakasaka ila nikiwa binti mdogo nilisoma au kukipitia pitia kitabu cha Monica Wilson, nami kiingereza changu wakati huo kilikuwa cha kusuasua.

Maelezo ya John Mwaipopo kuhusu asili ya Wanya-Kyusa (au watoto wa Kyusa) ni sahihi kabisa. Nikiwaeleza wenzangu kuwa "I'm the mother of the Nyakyusa tribe" hawaamini, yaani Wanyakyusa were named after my great great great great... grand mother!

Nakuonea ghele mno maana huu ni wakati wa mavuno ya mpunga (chele wa Kyela), na msimu wa mbasa kwa wingi.

Bila shaka utatembelea Matema Beach Enjoy your stay.

UK
London

Mbele said...

Ndugu Mwaipopo, hii hadithi ya Kampapabunga the impostor imo, na hii ya Two Cunning Men, na nyingine kadha wa kadha. Kwa vile nimefanya kazi ya kutafsiri hadithi za kiMatengo kwa miaka kadhaa, ninaposoma tafsiri hizi za Mwalimu Mwakasaka natambua kuwa aliiweza vizuri kazi hii.

Katika lugha zetu za ki-Bantu, kuna mtindo na hata mtiririko fulani ambao unajitokeza kwenye hadithi. Ukiwa na uzoefu wa hizi hadithi, hata ukisoma tafsiri ya lugha usiyoijua, unapata hisia kuwa imetafsiriwa ipasavyo.

Hizi tafsiri za Mwakasaka zinavutia. Labda ndio maana jamaa alipokisoma kitabu chako, alitokomea nacho mitini :-)

Mzee Sikapundwa, nashukuru kwa ujumbe wako, na namba ya simu. Nitaenda hadi Litembo, na itakuwa vizuri tukikutana hapa Songea.

Dada anonymous wa UK, shukrani. Nashukuru kusikia ni wakati wa mavuno, maana ni lazima niondoke na kigunia cha mchele kuelekea Dar.

Matema Beach nimepangia kwenda. Halafu, maadam tunaongelea mambo haya ya masimulizi, nimepata wazo kuwa niwatafute watu wanaoweza kuimba nyimbo zilizomo katika kitabu cha Mwakasaka, hasa zile za hadithi. Kwa mfano, kuna hadithi ya "Kandangasali," yenye wimbo unaorudiwa rudiwa. Itakuwa vizuri sana kuzirekodi nyimbo hizi, kwani nami hupenda kuwasimulia wa-Marekani hadithi za makabila mbali mbal ya kwetu.

Renatus Mgusii said...

Mzee Mbele karibu Mbeya, Mimi nilikuwa naishi Mbeya hadi 2006 na sasa nimehamia DSM. Wewe ni balozi mzuri wa Tanzania. Baada ya kusoma comments za synonimous niliona ni muhimu nikatafuta machapisho yako. Nimepata kile kitabu na Africans and Americans Embracing Cultural Differences na Hadithi za Kimatengo (Matengo Folktales). Nimekipenda sana. Ingawa sitegemei katika maisha yangu kuja kuishi Marekani lakini kwa kusoma nimepata picha nzuri sana kuhusu tofauti ya utamaduni wetu na wa wenzetu. Mwenzetu aliyesoma na kuona ni chakawaida kabisa inawezekana ameshindwa kuwa na mtizamo wa ndani wa nini kinachozungumzwa. Ni kweli ukisoma unaweza kuona ni cha kawida sababu mambo yanayoelezwa ni ya kawaida ila katika kuyatafakari na kuyaeleza katika maandishi yanaweka wazi na vizuri sana tofauti hizo na tafsiri halisi ya mazingira yanayoleta tofauti hizo. Nimesikia unakuja natamani kukuona na kukusalimia tu. Utaniwia radhi kwamba kwa asili nimetokea kuwahusudu sana walimu hasa wanaotumia muda wao kuwasiliana na watu wengine kwa ajili ya masuala ya kijamii.Kitabu kizuri nakufagilia sana na nikimaliza nitasoma na hadithi za kimatengo na baadae nikikipata Changamoto nitakisoma pia. Udumu mzee.
Asante sana ,
Renatus Mgusii

Mbele said...

Ndugu Mgusii, shukrani kwa ujumbe. Wewe ni m-Tanzania wa pekee, kati ya wale wachache sana wanaothubutu kununua na kusoma vitabu ambavyo si vya udaku.

Ni kweli, huenda usifike Marekani. Lakini katika dunia ya utandawazi wa leo, utakumbana nao kwa namna moja au nyingine, au rafiki na majirani zako watakumbana nao. Kwa mfano, wa-Marekani wengi wanakuja huko Tanzania, kwa shughuli mbali mbali, kama vile utalii, masomo, kujitolea. Wengine wameoa au kuolewa huko. Na huenda mtoto wa ndugu yako au rafiki yako akaja huku Marekani, iwe ni kwa masomo au kazi, au biashara.

Au kuna mawasiliano ya mtandao, baina ya wa-Marekani na wa-Swahili. Katika mazingira yote hayo, masuala niliyoelezea katika kitabu yanajitokeza.

Nitoe mifano hai ya watu ambao kitabu hiki kinawasaidia hapa Tanzania. Kuna kikundi cha vijana pale Mto wa Mbu ambao wanajishughulisha na utalii. Hao wanakipenda kitabu hiki, kama walivyoelezea hapa.

Pale Arusha, kuna kampuni ya utalii ya J.M. Tours. Mmiliki wake ni mama mzungu ambaye ameolewa na m-Tanzania. Huyu mama alipokisoma tu kitabu hiki, miaka madhaa iliyopita, alifanya uamuzi wa kuwapa madreva wake wasome. Wanakitumia. Ukiwakuta, watakueleza kinavyorahisisha shughuli zao za kuongoza watalii, kwa sababu wanaelewa hizo tofauti za tamaduni ambazo zamani zilikuwa kama kero au kipingamizi.

Mamia ya wa-Marekani wa kanisa la kiLuteri wanakuja huko Tanzania kwa mpango wa uhusiano baina ya makanisa yao na makanisa ya Tanzania. Hao wanakitumia kitabu hiki, na hapa Tanzania ukiwasiliana na Askofu Owdenburg Mdegela wa jimbo la Iringa, ambaye ni mmoja wa waasisi wa program hiyo, atakueleza jinsi kitabu hiki kinavyowafaa kwa shughuli zao. Yeye ni kati ya wa-Tanzania ambao wanashughulika na wa-Marekani muda wote. Kwa hivi, anajua anachosema.

Huwa napokea maombi kutoka kwa waTanzania wanaoendesha shughuli za utalii na pia za kuwaleta wageni wa kujitolea. Wananiambia niwaletee wageni. Ningefurahi kufanya hivyo, lakini mimi ningependa kwanza waTanzania hao waonyeshe moyo wa kujielimisha kwa yale ninayoongelea, iwe ni kwenye vitabu au kwenye warsha. Ajabu ni kuwa nimejaribu kuendesha warsha mwaka jana, hapa Tanga na Arusha, na taarifa ziliwekwa hadi kwenye blogu ya Michuzi, lakini waTanzania hawakujitokeza. Nami sioni sababu ya kuwaletea wageni watu ambao hawaonyeshi utashi wa kutafuta elimu hii ya tofauti za tamaduni, elimu ambayo naamini ni jambo la msingi sana.

Mungu akipenda, tutaonana hivi karibuni hapa Dar es Salaam. Nakutakia kila la heri.

Mbele said...

Nashindwa kuamini kuwa baada ya mawasiliano haya hapa juu na mdau Mgusii, kweli na ni jambo la kushukuru kuwa tulipata fursa ya kuonana pale Dar es Salaam, kama nilivoelezea hapa.