Monday, November 22, 2010

Kitabu Kilivyopokelewa Ubalozi wa Kenya

Mwaka 2007 mwanzoni, jumuia ya wa-Kenya wanaoishi Minnesota waliandaa mkutano kuhusu uwekezaji nchini kwao. Walihudhuria wa-Kenya wengi sana, wakiwemo maofisa wa serikali na taasisi mbali mbali waliofika kutoka Nairobi. Nilishiriki, nikiwa na meza ambapo niliweka vitabu vyangu na machapisho mengine.

Nilikutana na wa-Kenya wengi, baadhi ambao tulifahamiana kabla na wengine kwa mara ya kwanza. Mmoja wa hao tuliofahamiana kabla alikuwa Julia Opoti, ambaye ni mwanahabari anayeendelea kujipatia umaarufu, na ni shabiki wa siku nyingi wa maandishi yangu. Alikuja kwenye meza yangu akiwa na bwana mmoja, akatutambulisha.

Yule bwana alikuwa afisa katika ubalozi wa Kenya, Washington DC. Julia alikuwa amemwambia kuhusu kitabu cha Africans and Americans naye akakinunua. Tarehe 17 Aprili, yule afisa aliniandikia ujumbe huu:

Kuhusu kitabu chako, hivi sasa nafikiri kimesomwa na watu kadri ya watano hapa ubalozi wetu na kimependwa sana. Ni matumaini yangu kuwa ukipata wasaa mzuri utaandika vitabu zaidi katika fani hii ili upate kunufaisha watu juu ya swali hili muhimu la tafauti ya mila na utamaduni.


Ujumbe huu, ingawa ulinifurahisha, haukunishangaza, kwa sababu ninafahamu jinsi wa-Kenya wanavyothamini vitabu na elimu kwa ujumla. Nimefahamu jambo hilo tangu nilipoanza kutembelea Kenya, mwaka 1989, na katika kuwaona huku ughaibuni. Nimeshasema hivyo hata katika kitabu changu cha CHANGAMOTO. Jambo la pili ni kuwa nilivutiwa na wito kuwa niendelee kuandika, wito ambao nimeupata kutoka kwa wasomaji wengine pia. Naendelea kuandika.

7 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Ndugu Mbele kazi yako ya kuelimisha haina kifani. Moyo wako wa kutoa kila ulicho nacho na unachojua ni wa kupigiwa mfano.
Nilikuomba anwani yako nikutumie kitabu changu cha Saa Ya Ukombozi nawe unitumie chako utakachochagua. Lakini naona jii. Kama ulikuwa ukitania nijuze niwatumie wengine maana sina nakala nyingi. Samahani kwa kutumia sebule yako kama ubao wa matangazo.
Nkwazi Mhango Nkuzi.

Mbele said...

Shukrani kwa ujumbe wako. Nilikuletea anwani yangu ya posta tarehe 18, kwa njia ya barua pepe. Nilikuwa nangoja nipate anwani yako ya posta pia, ili tubadilishane vitabu.

Hata hivi, bora nikuletee tena hapa kijiweni pangu:

Joseph L. Mbele
English Department
St. Olaf College
Northfield, MN 55057
USA

Emmanuel said...

Dear Prof Mbele.

Hongera sana kwa kazi hii nzuri. Binafsi, lazima nikinunue hichi kitabu chako cha Africans & Americans. I am just growing up reader and hope to be a writter too. I am in the US for My Master's studies and I wish I will have time to follow up on your blog as I am used now. Thanks,

Emmanuel,
University of maryland,
College Park, MD
USA

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kaka kitabu chako nimekituma leo na kikifika nitaarifu.
Samahani kwa kuchelewa. Maana hata hiyo barua-meme au pepe uliyonitumia inaonekana iliingia mapepe haikufika.
Kila la heri,
Nkwazi

Mbele said...

Ndugu Mhango, shukrani. Nami nangojea anwani yako ya posta.

Ndugu Emmanuel, nafurahi kupata ujumbe wako, na kusikia kuwa unawazia kuwa mwandishi. Tunahitaji waandishi wengi, kwani kila binadamu ana mengi katika maisha yake, mtazamo, hisia, na mategemeo, ambayo yakiandikwa vizuri, yanakuwa ni hazina yenye manufaa kwa wanadamu. Nakutakia kila la heri.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kaka anwani yangu utapata. Ipo kwenye kitabu kilichotumwa.

Mbele said...

Ndugu Emmanuel,

Asante kwa ujumbe wako. Bahati mbaya sikuwa nimepita hapa kwa muda mrefu sana. Ukipata fursa ya kunipa maoni yako kuhusu kitabu changu, nitashukuru sana. Nakutakia kila la heri.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...