Posts

Showing posts from October, 2015

Shairi la "Kimbunga" (Haji Gora Haji)

Image
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasihi. Tofauti na inavyoeleweka katika jamii, kutafsiri ni suala pana kuliko kuwasilisha ujumbe kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine, bali ni kutunga upya kazi ya fasihi inayotafsiriwa. Hili suala linajadiliwa sana na wataalam wa lugha, fasihi, na falsafa. Pamoja na matatizo yote, ninapenda kuchemsha akili yangu kwa kutafsiri kazi za fasihi. Kwa mfano, nimetafsiri  hadithi za ki-Matengo,  na shairi la Mama Mkatoliki. Hapa naleta shairi la Haji Gora Haji, mshairi maarufu wa Zanzibar, ambaye niliwahi kukutana naye. Shairi hilo ni "Kimbunga" ambalo limo katika kitabu chake kiitwacho Kimbunga . Jisomee shairi hilo na ujionee nilivyopambana na lugha katika kutafsiri. Ni mapambano, na kuna wakati unajikuta umepigwa butwaa au mwereka. -----------------------------------------------------------------------------------------------------------

Maprofesa na Wajibu wa Kuandika

Image
Profesa ni mtu aliyefikia kiwango cha juu cha ufanisi katika ufundishaji, utafiti, uandishi, na kutoa ushauri kwa jamii katika masuala mbali mbali yanayohusiana na utaalam wake. Siwezi kuongelea hapa vipengele vyote vya suala hili, kama vile vigezo vinavyotumika katika kupima ufanisi wa mhusika hadi kumfikisha kwenye hadhi ya uprofesa. Ninakumbushia tu suala la wajibu wa profesa wa kuandika. Baadhi yetu wa-Tanzania tumeliwazia na kuliongelea suala hili kwa miaka mingi, kwa manufaa ya jamii, tukiliunganisha na masuala kama sera ya elimu, matatizo ya uchapishaji, na kukosekana kwa utamaduni wa kununua na kusoma vitabu. Kilichonifanya nirejeshe mada hii leo ni kwamba nimejikumbusha tamko la Rais Kikwete, "Maprofesa Wananisikitisha," ambalo lilijadiliwa katika blogu yangu hii na blogu ya Profesa Matondo. Mambo yaliyosemwa katika majadiliano yale ni muhimu na yataendelea kuwa muhimu. Wajibu wa profesa wa kuandika, kama njia mojawapo ya kufundisha na kuchangia maendeleo ya t

Shukrani kwa Wa-Tanzania Wadau wa Kitabu Changu

Image
Blogu yangu ni mahali ninapojiandikia mambo yoyote kwa namna nipendayo. Siwajibiki kwa mtu yeyote, wala sina mgeni rasmi. Leo nimewazia mafanikio ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Nimejikumbusha kuwa mtu hufanikiwi kwa juhudi zako pekee, hata ungekuwa hodari namna gani. Kuna watu unaopaswa kuwashukuru. Nami napenda kufanya hivyo, kama ilivyo jadi yangu. Nimewahi kuwaongelea na kuwashukuru wanablogu wa-Tanzania, na nimewahi kuwaongelea na kuwashukuru wa-Kenya. Ninapenda kuendelea kuwakumbuka wa-Tanzania. Mwanzoni kabisa, nilipokuwa nimeandika mswada wa awali kabisa wa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences , rafiki yangu Profesa Joe Lugalla, wa Chuo Kikuu cha New Hampshire, alipata kuusoma, akapendezwa nao. Yeye, kwa jinsi alivyoupokea mswada ule, alikuwa kati ya watu wa mwanzo kabisa kunitia hamasa ya kuuboresha. Tangu wakati ule hadi leo amekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha watu wakisome kitabu hiki.

Matamasha ya Vitabu: Tanzania na Marekani

Image
Nimehudhuria matamasha ya vitabu Tanzania na Marekani. Kwa usahihi zaidi, niseme nimeshiriki matamasha hayo, kama mwandishi, nikiwa na meza ya vitabu vyangu. Nimeona tofauti baina ya Tanzania na Marekani katika uendeshaji wa matamasha haya. Hapa napenda kugusia kidogo suala hilo, nikizingatia kwamba ni suala linalowahusu waandishi, wasomaji, wachapishaji na wauza vitabu. Tofauti moja ya wazi ni kuwa matamasha ya vitabu ni mengi zaidi, maradufu, Marekani kuliko Tanzania. Marekani kuna matamasha makubwa ya kitaifa na matamasha makubwa kiasi ya kiwango cha majimbo, na pia matamasha ya kiwango cha miji. Mtu ukitaka, unaweza kuzunguka nchini Marekani ukahudhuria matamasha ya vitabu kila wiki, kila mwezi, mwaka mzima. Angalia, kwa mfano, orodha hii hapa. na hii hapa. Kwa upande wa Tanzania, hali ni tofauti. Matamasha ya vitabu hayafanyiki mara nyingi. Tunaweza kuwa na tamasha la vitabu la kitaifa mara moja kwa mwaka. Lakini hatuna utamaduni wa kuwa na matamasha ya sehemu mbali mbali z

Kitabu Kinapouzwa Amazon

Image
Nina jadi ya kuandika kuhusu vitabu katika blogu hii. Ninaandika kuhusu vitabu ninayonunua na ninavyosoma, uandishi, uchapishaji, na uuzaji wa vitabu. Ninaandika ili kujiwekea kumbukumbu na pia kwa ajili ya wengine wanaotaka kujua mambo hayo, iwe ni wasomaji na wadau wa vitabu, waandishi, au wanaotarajia kuwa waandishi. Leo napenda kuongelea kidogo juu ya vitabu vinavyouzwa katika tovuti ya Amazon. Nimewahi kuandika kuhusu mada hii. Lakini nimeona si vibaya kuirudia, ili kuelezea kama yale niliyoyasema mwanzo yamebaki vile vile au kama kuna lolote jipya. Ninaongea kutokana hali halisi ya vitabu vyangu Amazon. Kwanza kabisa, mambo ya msingi niliyosema mwanzo yamebaki vile vile. Vitabu vyangu viliingia Amazon bila mimi kuvipeleka kule. Vinauzwa kule kuliko sehemu nilipovichapisha au kwenye duka langu la mtandaoni. Ninajionea mwenyewe kuwa Amazon ni mtawala wa himaya ya uuzaji wa  vitabu mtandaoni. Kila niendako, kwenye matamasha ya vitabu au katika kukutana na watu popote, liki

Michango ya Papa's Shadow Imekamilika

Image
Kwa mwezi mzima kumekuwa na kampeni ya kuchangisha fedha kwa ajili ya filamu ya Papa's Shadow, kama nilivyoelezea katika blogu hii. Leo, shughuli imekamilika, masaa sita kabla ya kipindi cha michango kwisha. Mafanikio haya yamefungua njia kwa mambo makubwa siku zijazo. Papa's Shadow sasa itapatikana kwa wadau, pindi taratibu za malipo zitakapokamilika. Kwangu ni furaha kubwa, kama mchangiaji mkuu wa filamu hiyo, sambamba na Mzee Patrick Hemingway, wa maelezo na uchambuzi juu ya mwandishi Ernest Hemingway. Ninafurahi pia kwamba filamu hii itaitangaza Tanzania kwa namna ya pekee, kama nilivyoelezea katika blogu hii. Umaarufu wa Ernest Hemingway ulimwenguni ni wa pekee. Pamoja na kuelezea uhalisi wa maisha ya binadamu, kama walivyofanya waandishi wengine maarufu, pamoja na kuzipa umaarufu kwa maandishi yake sehemu alizotembelea hapa duniani, Hemingway alianzisha jadi mpya kimtindo katika uandishi wa ki-Ingereza. Hilo limesemwa tena na tena na wataalam wa fasihi. Ninaamini

Kama Mwandishi, Ninawaenzi wa-Kenya

Image
Mimi kama mwandishi, ninawaenzi wa-Kenya. Naandika kutokana na uzoefu wangu. Tena na tena, mwaka hadi mwaka, nimeshuhudia wa-Kenya wakifuatilia vitabu vyangu. Wamekuwa bega kwa bega nami kama wasomaji wangu. Tangu nilipochapisha kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences , wa-Kenya walikichangamkia. Ndugu Tom Gitaa, mmiliki wa gazeti la Mshale aliandaa mkutano kuniwezesha kukitambulisha kitabu hicho, kama ilivyoelezwa katika taarifa hii. Kati ya watu waliohudhuria alikuwepo Julia Opoti, m-Kenya mwingine, ambaye alishajipambanua kama mpiga debe wa kitabu hiki. Siku hiyo alimleta rafiki yake m-Kenya, Dorothy Rombo, naye akapata kunifahamu na kukifahamu kitabu changu. Julia hakuishia hapo. Siku moja ulifanyika mkutano mkubwa wa wa-Kenya hapa Minnesota, ambao uliwakutanisha wana-diaspora wa Kenya na viongozi mbali mbali waliofika kutoka Kenya ili kuongelea fursa zilizopo nchini kwao katika uwekezaji na maendeleo kwa ujumla, na namna wana-diaspora wanavyoweza

Nimepata Toleo Jipya la "Green Hills of Africa"

Image
Leo ni siku ya furaha kwangu. Nimepata nakala ya toleo jipya la Green Hills of Africa , kitabu cha Ernest Hemingway, kilichochapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1935. Taarifa kwamba toleo hili lilikuwa linaandaliwa nilielezwa na Mzee Patrick Hemingway, kama nilivyoandika katika blogu hii. Kwa hivi, nilipogundua kwamba limechapishwa, niliagiza nakala hima. Katika Green Hills of Africa ,  Hemingway anaelezea mizunguko yake katika nchi ya Tanganyika, mwaka 1933-34, akiwa na mke wake wa pili Pauline Pfeiffer. Anaelezea uzuri wa nchi, watu wa makabila, tamaduni, na dini mbali mbali, na wanyama katika mbuga alimowinda, kama vile Serengeti na eneo la Ziwa Manyara. Anaelezea miji alimopita, kama vile Mto wa Mbu, Babati, Kondoa, Handeni, na Tanga. Toleo hili la Green Hills of Africa lina mambo ambayo hayakuwemo katika toleo la mwanzo, kama vile maandishi ya awali ambayo hayakutokea kitabuni, picha, na hata "diary" aliyoandika Pauline alipokuwa safarini na mumewe. Nilijua kuwa &q

Wanafunzi Wangu wa Ki-Ingereza

Image
Ni yapata mwezi sasa tangu tuanze muhula mpya wa masomo hapa chuoni St. Olaf. Ninafundisha kozi mbili, South Asian Literature na "First Year Writing." Hii ya kwanza ni kozi ya fasihi ya ki-Ingereza kutoka India, Pakistan, na Sri Lanka. Ya pili ni kozi ya uandishi wa ki-Ingereza. Picha hii kushoto, ya darasa la ki-Ingereza (FYW), tulipiga leo. Mwanafunzi mmoja hayumo. Niliweka picha ya darasa kama hili katika blogu hii. Nilipenda ualimu tangu utotoni. Ninawapenda wanafunzi. Ninawaambia hivyo tangu siku ya kwanza ya masomo, nao wanashuhudia hivyo siku zote. Wanajionea ninavyojituma kuwaelimisha kwa uwezo wangu wote na kwa moyo moja. Sina ubaguzi, dhulma, wala upendeleo. Hiyo imekuwa tabia yangu tangu nilipoanza kufundisha, mwaka 1976, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ninajivunia jambo hilo. Kwa miezi mingi, hasa mwaka jana, afya yangu haikuwa njema, na nilichukua likizo ya matibabu. Ingawa nimeanza tena kufundisha, inatokea mara moja moja kwamba sijisikii vizuri. Juzi ilit

Uzushi wa Abdulrahman Kinana

Siku kadhaa zilizopita, niliiona mtandaoni makala iliyoandikwa na Abdulrahman Kinana, katibu mkuu wa CCM. Ilikuwa ni makala kali. Kinana anazitahadharisha nchi za magharibi kwamba mgombea urais Edward Lowassa na umoja wa vyama vya siasa ninavyomwunga mkono, yaani UKAWA, wakishinda uchaguzi, Tanzania itageuka kuwa ngome ya magaidi. Makala yake imejibiwa na watu wengi, lakini nimeona nilete hapa uchambuzi wa Ahmed Rajab huu hapa.  Ahmed Rajab amethibitisha vizuri uwongo na uzushi uliomo katika makala ya Kinana, nami sina sababu ya kurudia uchambuzi wake. Ninapenda kuongezea mawili matatu. Kwanza, ni jambo la kushangaza kwamba Kinana anazielekea nchi za magharibi kama vile ni marafiki zetu wa kuaminiwa, au kama vile ni nchi zenye maslahi sawa na yetu. Ukweli ni kwamba nchi hizo zinafuata maslahi yao. Nchi kama Marekani imethibitisha katika historia yake kwamba haisiti kuwageuka wale waliojiaminisha kuwa ni marafiki wake. Mfano ni Saddam Hussein. Kinana angezingatia hilo. Ni mradi g

Kwa Wanadiaspora: Fursa ya Kuitangaza Tanzania

Image
Naandika ujumbe huu kwako mwanadiaspora mwenzangu, kuelezea mradi ambao nimehusika nao, wa kitaaluma na wenye fursa ya kuitangaza Tanzania. Mradi huo ni filamu juu ya mwandishi maarufu Ernest Hemingway, ambaye aliwahi kutembelea nchi yetu na Afrika Mashariki kwa ujumla mwaka 1933-34 na 1953-54. Kutokana na safari hizo, Hemingway aliandika vitabu, hadithi, insha, na barua. Maandishi hayo ni hazina, kwa jinsi yanavyoitangaza nchi yetu, iwapo tutaamua kuwa makini katika kuyatumia. Mfano ni hadithi ambayo wengi wamesikia angalau jina lake, "The Snows of Kilimanjaro." Nilifanya utafiti wa miaka kadhaa juu ya mwandishi huyu, hatimaye nikatunga kozi, Hemingway in East Africa. Nilisafiri na wanafunzi wa ki-Marekani kwenda Tanzania, tukatembea katika baadhi ya maeneo alimopita Hemingway, huku tukisoma maandishi yake. Kozi hii imemhamasisha Jimmy Gildea, mmoja wa wanafunzi hao, kutengeneza filamu, Papa's Shadow. Sehemu kubwa ya filamu hiyo ni mazungumzo baina yangu na Mzee