Posts

Showing posts from 2008

Warsha: Utamaduni, Utandawazi na Maendeleo

Kati ya mambo ninayofanya ni kutoa ushauri kwa mashirika, taasisi, vyuo, vikundi na watu binafsi kuhusu masuala ya tofauti baina ya utamaduni wa Mwafrika na ule wa Mmarekani. Ninafanya hivyo kwa njia mbali mbali, kama vile kuandika makala na vitabu, kuendesha warsha, au kukutana watu binafsi ana kwa ana. Ninaposema utamaduni, namaanisha vitu kama hisia, tabia, maadili, namna tunavyofikiri na tunavyoongea. Vipengele hivi vyote vinatutofautisha watu wa tamaduni mbali mbali, na ni muhimu kuvielewa ili kuepusha migongano. Katika dunia ya leo, ya utandawazi, masuala ya tofauti za tamaduni yanahitaji kupewa kipaumbele, kwani yanaweza kuwa pingamizi kubwa, chanzo cha migogoro, au chachu ya hii migogoro. Nitaendesha warsha kuhusu masualaa hayo tarehe 4 Julai, 2009, kwenye kituo cha Meeting Point Tanga. Watu kutoka mashirika, makampuni, taasisi, na jumuia mbali mbali watapata fursa ya kuyatafakari masuala kadha wa kadha yanayojitokeza wakati huu ambapo watu wa tamaduni mbali mbali wanalazimi

Kijitabu Changu Kipya

Image
Miaka miwili iliyopita niliombwa kushiriki katika maonyesho ya utamaduni wa Mwafrika, soma hapa , yaliyofanyika kwa mara ya kwanza mjini Minneapolis katika jimbo la Minnesota, Marekani. Maonyesho hayo yalipangwa kujumlisha mambo mengi: historia ya Mwafrika duniani na harakati alizopitia, mafanikio na mchango wake, na hali yake ya sasa na baadaye. Wasanii, wabunifu wa mavazi, wanamuziki, na wengine walialikwa kutoa mchango wao. Mimi nilialikwa kuandaa vielelezo vya mambo muhimu katika historia ya Mwafrika, kuanzia chimbuko la binadamu Afrika hadi kusambaa kwa Waafrika sehemu mbali mbali za dunia, kama vile Marekani, Ulaya, na Asia. Nilifanya utafiti nikaandika habari hizo kwa mtindo wa insha fupi kumi. Kila insha niliiweka kwenye bango kubwa na kila bango liliambatana na picha kadhaa. Siku ya tamasha, niliyabandika mabango hayo kwenye kuta za ukumbi niliopangiwa. Watu walifika humo na kusoma kwa wakati wao, wakiangalia pia zile picha. Mama mmoja aliyehudhuria na kuanga

CCM: Ni chama cha Mapinduzi?

Sielewi kwa nini watu wanaamini kuwa CCM ni chama cha mapinduzi. Sijawahi kuelewa na bado sielewi kwa nini. Dhana ya mapinduzi ilielezwa vizuri na TANU, katika "Azimio la Arusha," "Mwongozo," na maandishi, hotuba na mahojiano mbali mbali ya Mwalimu Nyerere. Matokeo ya yote hayo ni kuwa Watanzania tulifahamu vizuri na kukubali dhana na maana ya mapinduzi katika nchi yetu. Yeyote ambaye hajasoma maandishi hayo, au kusikiliza hotuba hizo, ningemshauri afanye hivyo, ili aweze kufahamu msingi wa ujumbe wangu. CCM ilipoanza, ilijinadi kuwa ni chama cha mapinduzi. Lakini baada ya muda si mrefu, mwelekeo wake ulijionyesha kuwa si wa mapinduzi. Badala ya kuendeleza fikra na mwelekeo wa "Azimio la Arusha," "Mwongozo" na mengine yote niliyoyataja hapo juu, CCM ilitoa "Azimio la Zanzibar." Ingawa CCM haikutoa fursa iliyostahili kwa wananchi kuliangalia na kulijadili "Azimio la Zanzibar," habari zilizojitokeza ni kuwa Azimio hili liliki

Kuku kwa Mrija

Watanzania wana uwezo mkubwa wa kubuni misemo na kudumisha uhai na utamu wa lugha ya kiSwahili. "Kuku kwa mrija" ni usemi moja ambao umepata hadhi ya pekee katika kiSwahili cha mazungumzo. Naamini kuwa wengi wanaweza kueleza maana ya usemi huu na matumizi yake, lakini napenda kuelezea machache, kwa kuchambua mantiki yake. Kuku kwa mrija ni usemi unaobeba dhana ya maisha ya raha, starehe, na vyakula tele. Kwa vile kuku ni nyama inayothaminiwa sana katika utamaduni wetu, kula kuku sana ni dalili ya kuishi maisha ya raha na mafanikio. Kwa ujumla, Watanzania wanaamini kuwa maisha hayo yanapatikana nchi za nje, hasa Ulaya na Marekani. Mtanzania anayeishi huko anahesabiwa na Watanzania walioko nyumbani kuwa anakula kuku kwa mrija. Maisha yake ni ya starehe na kuku ndio chakula chake kikuu. Mimi mwenyewe nilikuja Marekani mara ya kwanza mwezi Agosti 1980, kusoma katika chuo kikuu cha Wisconsin-Madison, nikitokea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo nilikuwa nafundisha. Wakati ul

Ubora wa huduma: msingi wa mafanikio

Ni muhimu kuelewa misingi ya mafanikio katika dunia ya leo, yenye ushindani mkubwa. Ushindani huu uko ndani ya nchi na kimataifa. Wapende wasipende, wafanya biashara na watoa huduma mbali mbali wanajikuta katika mazingira ya mashindano ambayo yanaongezeka kwa kasi na yanazidi kuwa magumu. Katika hali hii, ni muhimu kwa kila mhusika kujua siri za mafanikio. Siri mmoja ni ubora wa huduma. Kuna usemi kuwa mteja ni mfalme. Nimeona sehemu mbali mbali duniani ambapo dhana hii inazingatiwa sana. Wako watu wanaofahamu vema umuhimu wa mteja. Wawe ni wafanyabiashara au watoa huduma, wanaonyesha kumjali sana mteja. Hata kama mteja ni msumbufu wafanyabiashara na watoa huduma hao wako tayari kumsikiliza, kumvumilia na kumsaidia hadi aridhike. Sio rahisi kuwaona wafanyabiashara au watoa huduma hao wakimkasirikia mteja. Hapa Marekani, kwa mfano, mteja anaponunua kitu, anapewa risiti, na kama hataridhika na kitu alichonunua, ana uhuru wa kukirudisha na kurudishiwa hela yake, au kubadilisha alichonun

Mahojiano na Profesa Joseph Mbele

Niliwahi kuhojiwa na ndugu Deus Gunza, katika Radio Butiama, kuhusiana na kitabu changu kinachohusu tofauti za utamaduni wa Mmarekani na ule wa Mwafrika. Mahojiano yanasikika hapa: http://butiama.podomatic.com/entry/et/2006-09-02T06_26_37-07_00

Hadithi Zetu

Image
Kabla ya kuweko maandishi, wanadamu walikuwa wanahifadhi kumbukumbu, taaluma, mafunzo, urithi wa utamaduni wao kwa ujumla, kwa masimulizi ya mdomo. Masimulizi hayo yalikuwa ya aina nyingi, kama vile misemo, methali, vitendawili, nyimbo na hadithi. Mfumo mzima wa masimulizi hayo ilikuwa ni hazina iliyobeba taaluma, falsafa, kumbukumbu, mafundisho na kila aina ya ujuzi ambao wanadamu walihitaji katika maisha na maendeleo yao. Kwa karne na karne, ambapo vitabu wala maktaba hazikuwepo, watu walihifadhi ujuzi wao vichwani mwao. Uwezo wao wa kukumbuka mambo ulikuwa mkubwa kuliko uwezo tulio nao sisi, kwani maandishi yametupunguzia uwezo huo na kutujengea aina ya uvivu. Tunategemea maandishi kuliko vichwa vyetu. Tukienda kusikiliza mhadhara, tunahitaji karatasi ya kuandikia yale tunayoyasikia, tofauti na watu wa zamani, ambao walikuwa wanatumia vichwa vyao tu. Nilizaliwa na kukulia kijijini. Nilikuwa na bahati ya kusikiliza hadithi, nyimbo, na masimulizi ya aina aina, katika Kimatengo, amba

Migogoro ya kidini na hadithi zingine

Kuna hadithi nyingi duniani. Hadithi moja ninayoifuatilia ni ya migogoro ya kidini. Katika historia ya binadamu, kumekuwepo migogoro na vita baina ya watu wa dini mbali mbali, na migogoro hiyo bado inaendelea. India kumekuwepo migogoro baina ya Wahindu na Waislamu, na pia baina ya Wahindu na Wakristu. Ulaya kulikuwako vita maarufu za "Crusades." Ireland kumekuwapo migogoro baina ya Wakatoliki na Waprotestanti. Nigeria kumekuwapo migogoro baina ya Waislam na Wakristu. Hii ni mifano tu. Ni kawaida kwa migogoro hii kuitwa migogoro ya kidini. Suali ninalojiuliza ni je, hii migogoro ni ya kidini kweli? Mimi nadhani hapa pana tatizo kubwa kinadharia. Ninavyofahamu, dhana ya dini ni kumwamini Muumba na kufuata amri zake: katika ibada, katika maisha yetu binafsi, na katika kuishi kwetu na wanadamu wenzetu. Dhana ya dini inajumlisha yote hayo. Kwa msingi huo, mtu mwenye dini atakuwa mcha Mungu, mwema, mpole, mwenye haki, mwadilifu, mwumilivu, na mwenye huruma. Binadamu ni binadamu;

Mwalimu Nyerere na Elimu

Image
Mwalimu Julius Nyerere alikuwa mwalimu. Naamini ni sahihi kusema kuwa silika ya ualimu iliathiri siasa na matendo ya Mwalimu Nyerere kama kiongozi wa Tanganyika na hatimaye Tanzania. Aliiona nchi yake kama darasa, na daima alikuwa anafundisha. Ninachotaka kuongelea hapa ni mchango wa Mwalimu Nyerere katika uwanja wa elimu. Elimu ni suala mojawapo ambalo Mwalimu Nyerere alilishughulikia sana. Katika kuelezea suala la elimu, Mwalimu aliweka na kufuata misingi kadhaa muhimu. Tanganyika ilipopata Uhuru, Mwalimu Nyerere alikuwa ameshajizatiti kubadilisha mfumo wa elimu uliokuwepo wakati wa ukoloni, ambao ulikuwa mfumo wa kibaguzi. Kulikuwa na shule za wazungu, za Wahindi, na za watu weusi. Mara tulipopata Uhuru, Nyerere alifuta ubaguzi na kuwachanganya wanafunzi mashuleni. Tangu mwanzo, Mwalimu Nyerere aliamini dhana ya usawa wa binadamu. Mwalimu Nyerere aliamini kuwa elimu ni haki ya kila mtu. Alifanya kila juhudi kutoa elimu kwa watu wote, kuanzia watoto hadi watu wazima. Mwalimu alij

Watoto wa Marekani

Image
Ingawa kazi yangu kuu hapa Marekani ni kufundisha katika kiwango cha chuo kikuu, kufanya utafiti katika taaluma zangu, na kutoa mchango wa mawazo na uzoefu kwa walimwengu kwa ujumla, napenda sana kukutana na kuongea na watoto, kuwasilimulia hadithi za Afrika, na kuwaeleza kuhusu maisha ya Afrika na masuala mengine ya maisha kwa ujumla, katika nchi yao na duniani. Nimeshaongea na watoto kwenye miji mbali mbali, katika mikoa ya Colorado, Minnesota, Pennyslvania, na Wisconsin. Watoto ni watoto. Kitu kimoja wanachopenda ni hadithi. Nami nimekuwa na fursa nyingi za kuwasimulia hadithi za Kiafrika. Kitu kimoja kinachofurahisha ni jinsi watoto walivyo na akili ya kufuatilia hadithi na kuzichambua. Hata watoto wanaodhaniwa kuwa hawana akili sana au hawana moyo wa kupenda masomo, wanaonyesha msisimko wanaposimuliwa hadithi. Hapa kuna taarifa kuhusu nilivyokutana na watoto wa shule ya LeTort, Pennsylvania. Soma hapa Jambo hili limenifanya nikumbuke habari moja

Wasomaji wa Maandishi Yangu

Image
Uandishi ni shughuli inayohitaji juhudi na ustahimilivu. Inaweza kuleta mema au mabaya katika jamii. Kwa hivi, mwandishi anapaswa kuwa makini. Uandishi unaweza kuwa na manufaa mengi, kwa mwandishi mwenyewe na kwa jamii. Kuandika kunatupa fursa ya kutumia akili katika kupanga mawazo na lugha. Ni zoezi la kuchangamsha na kuboresha akili. Kitu kimoja kinachonipa faraja sana na motisha pia, ni kufahamiana na watu mbali mbali, kwa njia ya maandishi yangu. Najifunza mengi kutokana na maoni ya wasomaji. Napenda kwenda sehemu mbali mbali kuwaonyesha watu maandishi yangu na kuongelea shughuli zangu za ufundishaji, utafiti, na uandishi. Napenda pia kuelezea ninavyojishughulisha katika kutoa ushauri kwa wageni mbali mbali, hasa Wamarekani, wanaokwenda Afrika, kama wanafunzi, watafiti, watalii, na washiriki katika shughuli za kujitolea. Baadhi ya picha zinazoonekana hapa zilipigwa Minneapolis, tarehe 4 Oktoba, 2008, wakati wa sherehe za kumbukumbu ya Uhuru wa Nigeria. Nilipata fursa ya kushiriki

Mwalimu Julius Nyerere

Image
Nimeona kuwa andiko la kwanza liwe juu ya Mwalimu Julius Nyerere. Mwalimu Nyerere ni mtu maarufu katika historia ya Tanzania. Katika ukumbi huu athari za mawazo na siasa za Mwalimu Nyerere zitajitokeza mara kwa mara, kwani alichangia kuiwezesha Tanzania kupitia hatua ilizopitia, akishirikiana na wazalendo wenzake, ambao nao watakuwa wanatajwa hapa ukumbini, kila itakapobidi. Mwalimu Nyerere anastahili kukumbukwa, kwa mchango wake mkubwa, sio tu kwa nchi yetu bali kwa dunia. Tunapaswa kusoma maandishi yake na kuyajadili, kuyatathmini, na kuyakarabati inapobidi, ili yaendelee kuwa mwongozo wetu. Mwalimu Nyerere alikuwa mtu wa fikra, ambaye daima alikuwa anaangalia maslahi ya nchi yetu, na jitihada alizofanya katika kubadilisha siasa, uchumi, utamaduni, na vipengele vingine vya nchi yetu ilikuwa ni kwa nia ya kuikomboa na kuijenga katika misingi ya uhuru, usawa, haki, na kujitegemea. Yako makosa ambayo alifanya, lakini alikuwa mzalendo, aliyeamini kuwa aliyokuwa anafanya ni kwa maslahi

Karibu, hapa kwetu

Karibu. Hapa ni kwetu--Watanzania, Waafrika, na wengine wanaotumia kiSwahili. Ninategemea kuwa huu utakuwa ukumbi wa masuala yanayotuhusu: katika siasa, uchumi, utamaduni, na jamii kwa ujumla. Namshukuru sana ndugu Freddy Macha, ambaye alinipa wazo la kuanzisha blogu. Freddy ni Mtanzania mwenye uwezo wa pekee katika fani mbali mbali, hasa muziki na uandishi. Anafanya kazi kubwa ya kuwaelisha na kuwaunganisha walimwengu. Namshukuru sana pia ndugu Jeff Msangi kwa kunihamasisha kwa namna mbali mbali. Jeff ni hodari katika kuelimisha umma kwa namna mbali mbali. Karibuni.