Posts

Showing posts from June, 2015

Mambo ya Tamasha la Vitabu Mankato

Image
Kila tamasha la vitabu au utamaduni ninaloshiriki huwa na mambo mengi ya kuelimisha na kuburudisha akili. Kukutana na watu na kuongea nao ni sababu muhimu ya ushiriki wangu katika matamasha hayo. Juzi katika tamasha la Deep Valley Book Festival,  binti yangu Zawadi nami, tunaoonekana pichani hapa kushoto, tulikutana na kuongea na watu mbali mbali. Kati ya hao alikuwepo mama mmoja ambaye si rahisi kumsahau. Alifika mezani petu, na wakati tunasalimiana alinyanyua nakala ya Matengo Folktales , Africans and Americans: Embracing Cultural Differences ,   Notes on Achebe's Things Fall Apart, na Africans in the World ,  akasema anavinunua. Wakati wote alikuwa anatuelezea kuwa alikuwa na binti yake ambaye aliishi China kwa miaka nane kisha akaenda Namibia, na kwamba ameipenda Namibia tangu  mwanzo. Alituambia tumwekee vitabu vyake, na kwamba binti yake angefika baadaye. Yapata nusu saa kabla ya tamasha kwisha, huyu binti alikuja. Tuliongea naye, akatuambia jinsi alivyoipenda Namibi

Tamasha la Vitabu Mankato Limefana

Image
Leo, nikiwa na binti yangu Zawadi, tulikwenda Mankato kushiriki tamasha la vitabu, Deep Valley Book Festival. Niliandika habari za tamasha hilo katika blogu yangu ya ki-Ingereza. Nilipeleka vitabu vyangu vinavyoonekana mtandaoni, pamoja kijitabu kiitwacho Africans in the World . Vile vile tulipeleka "t-shirt" kama hizo tulizovaa pichani, zenye nembo ya kampuni yangu ndogo Africonexion: Cultural Consultants. Tunajifunza mengi katika kukutana na watu wanaofika kwenye meza yetu. Hatujui nini kitamvutia mtu fulani na kwa nini. Lakini watu hujieleza. Tunasikia habari nyingi, nyingine za kushangaza, zinazomfanya mtu anunue hiki au kile. Inatufurahisha kuwaangalia watu wakipita kwenye meza mbali mbali kuangalia vitabu, kuongea na waandishi, wachapishaji na wengine wanaokutana nao katika tamasha. Nasi tunapata fursa ya kukutana na watu mbali mbali. Leo, kwa mfano, wamefika watu kwenye meza yetu ambao wametuambia wamefika Afrika: Botswana, Tanzania, na Namibia. Tunahisi walivu

Habari ya Malipo ya Mhadhara Chuoni Winona

Jumanne wiki hii, nilikwenda Chuo Kikuu cha Winona kutoa mhadhara, kama nilivyoandika katika blogu hii. Katika safari kama hii, kuna mambo mengi, na haiwezekani kuyaongelea yote. Hata hivi, naona ni vizuri tu kuelezea angalau yale yenye umuhimu Fulani kwangu na labda kwa wengine. Napenda kuongelea suala la malipo ya mhadhara ule. Wakati nilipoombwa kwenda kutoa mhadhara, mhusika aliniuliza malipo yangu ni kiasi gani. Huu ni utaratibu hapa Marekani, nami kama ilivyo kawaida yangu, nilimwambia kuwa siweki kipaumbele kwenye malipo, bali kutoa huduma itakiwayo. Kama wanaonialika wana uwezo wa kunilipa, kwangu ni sawa, kama wana uwezo kidogo, kwangu ni sawa, na kama hawana uwezo, kwangu ni sawa pia. Niko tayari kuitikia mwito kwa hali yoyote. Nilidhani suala lilikuwa limeishia hapo. Siku kadhaa baadaye, mhusika alinielezea tena habari ya malipo, akataja kiasi ambacho angeweza kunilipa, kutokana na bajeti yake. Nilimjibu kuwa sina tatizo, nikamshukuru. Alipoleta mkataba, ambao ulitaja

Uzinduzi wa Filamu ya "Papa's Shadow"

Image
Jana ilikuwa siku ya pekee kwangu. Nilihusika na matukio mawili muhimu sana, kama nilivyoripoti katika blogu hii. Napenda kuongelea tukio mojawapo: uzinduzi wa filamu ya "Papa's Shadow." Habari ya filamu hii nimezungumzia kabla katika blogu hii, lakini imeelezwa pia, vizuri kabisa, kwenye tovuti ya Ramble Pictures. Jana ilikuwa siku tuliyoingojea kwa hamu kubwa. Ilikuwa ni siku ya kuonyeshwa filamu ya "Papa's Shadow" hadharani, ingawa wote walikuwa waalikwa. Kwa kuwa mimi ni mhusika mkuu katika filamu hiyo kama mzungumzaji sambamba na Mzee Patrick Hemingway, uwepo wangu ulikuwa muhimu. Nilijikuta niko miongoni mwa kadamnasi iliyoniona maarufu. Nina hakika kuwa huu utakuwa mzigo maishani, kwani nitategemewa kujua mengi juu ya Hemingway kuliko inavyowezekana. Hiyo jana tu masuali magumu yalikuwa yanaelekezwa kwangu. Hata hivi, hii ni changamoto nzuri ya mimi kuendelea kujielimisha. Baada ya filamu kuonyeshwa, watu walikuja na kunishukuru sana kwa mengi

Imekuwa Siku ya Mafanikio Makubwa

Image
Leo imekuwa siku ya mafanikio makubwa. Kwanza nilienda Chuo Kikuu cha Winona na binti yangu Zawadi nikatoa mhadhara. Nilitumia hadithi za jadi kujadili namna wahenga wetu walivyozielewa dhana za uongozi na uwajibikaji. Baada ya kuelezea kwa ufupi jinsi Afrika ilivyokuwa chimbuko la binadamu, lugha, sayansi, tekinolojia, na falsafa, nilisimulia hadithi mbili zilizomo katika kitabu changu cha Matengo Folktales , kuthibitisha namna wahenga wetu walivyoyatafakari masuala ya jamii. Hadithi hizo ni "The Monster in the Rice Field" na "Nokamboka and the Baby Monster." Baada ya kurejea kutoka Winona, tulijiandaa kwenda Excelsior, kuhudhuria uzinduzi wa filamu ya "Papa's Shadow." Filamu hii inamhusu mwandishi Ernest Hemingway, na kwa kiasi kikubwa ni mazungumzo baina yangu na Mzee Patrick Hemingway, kuhusu maisha, uandishi, na fikra za Hemingway. Matokeo ya mazungumzo yetu yalivyo katika filamu yamewasisimua sana watazamaji. Nilitegemea hivyo, kutokana

Ernest Hemingway, a bridge between cultures

Image
HAVANA, JUNE 22, 2015 Ernest Hemingway, a bridge between cultures The 15th International Ernest Hemingway Colloquium was inaugurated in Havana on June 18, in the presence of researchers and followers of the life and work of the great U.S. writer ----------------------------------------------------------------------------------------------------- Author: Alain Valdés Sierra | alain@granma.cu june 20, 2015 01:06:26                  An excellent opportunity to learn why Ernest Hemingway fell in love with Cuba, was how Julián González, Cuban Minister of Culture, described the 15th International Colloquium dedicated to the author of The Old Man and the Sea , an academic event which began yesterday, June 18, in the presence of researchers and followers of the life and work of the great writer. The Minister spoke to the press regarding the number of U.S. scholars who attend each edition of the event and how their interest in the life of the winner of the Nobel Prize fo

El legado de Ernest Hemingway es celebrado en Cuba

Image
La vigencia del célebre autor también está en las películas basadas en sus obras / El evento resaltó la vida y obra del Premio Nobel de Literatura Caracas, 22 de junio de 2015. - Considerado el Dios de Bronce de la literatura norteamericana, expertos sostienen que la vigencia de sus obras no ha palidecido. Este domingo culminó el XV Coloquio Internacional Ernest Hemingway realizado en Cuba, con la participación de expertos de diferentes partes del mundo. Un estudioso cubano participante del evento resaltó la vida y obra del Premio Nobel de Literatura y manifestó que la personalidad del célebre autor ha creado una serie de mitos, sitios y plazas en los lugares donde él vivió. "La efigie de Hemingway (1899-1961) flota en un limbo, que va desde La Habana a Paris, Nueva York, España, Italia, el Caribe, desde Tanzania a Centroáfrica, y al parecer no va a desaparecer todavía" declaró un participante del Coloquio. En 1954, Hemingway le entregó la medalla del Premio No

Niliyoyaona Maktabani Brookdale, Minnesota

Image
Jana, kama nilivyoandika katika blogu hii, nilihudhuria mkutano Brooklyn Park, ambao tulifanyia katika maktaba ya Brookdale. Hapa kushoto ni picha ya upande wa Mbele wa maktaba hii, inavyoonekana kabla hujaingia ndani. Jana ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kufika hapa, na niliona jinsi jengo lilivyo tofauti na majengo ya maktaba zingine ambazo nimeingia hapa Minnesota. Nilivyoingia ndani, nilijikuta sehemu hii inayoonekana kushoto, ingawa ni kubwa na pana zaidi ya hii inayoonekana pichani. Wakutubi wengi wapo katika eneo hilo, tayari kuwasiaida wateja, na sehemu ya maulizo ambayo ni kubwa pia, iko eneo hili. Unapokuwa sehemu hii, kwa mbele yako na pembeni kuna maeneo yenye vitabu, majarida, kompyuta nyingi na hifadhi mbali mbali za taarifa, kama vile CD, DVD na na kaseti. Niliulizia kilipo chumba cha mkutano, nikapita katikati ya makabati ya vitabu vya kila aina hadi mwishoni kabisa. Baada ya mkutano, nilirejea tena sehemu hii na kuchungulia katika makabati mbali mbali, has

Msomaji Amenilalamikia

Image
Leo alasiri nilikwenda Brooklyn Park, Minnesota, kuhudhuria mkutano wa bodi ya Afrifest Foundation ambayo mimi ni mwenyekiti wake. Tulifanyia mkutano wetu katika maktaba ya Brookdale. Baada ya mkutano, nilipotoka nje kuelekea sehemu nilipopaki gari, alinikimbilia dada Latonya anayeonekana katika picha hapa kushoto, ambayo tulipiga miaka mitano iliyopita kwenye tamasha la Afrifest. Ni m-Marekani Mweusi kutoka Chicago, ila anaishi Minneapolis. Tulifahamiana miaka ile kwa kuwa naye alikuwa katika bodi ya Afrifest Foundation. Hatukutegemea kama tungeonana leo, ghafla namna ile. Kwa hivi tulifurahi sana. Lakini hakupoteza muda, alianza kunihoji kwa nini siandiki sana katika blogu yangu ya ki-Ingereza kama zamani. Alisema, akimaanisha maandishi yangu ya kiSwahili, "Tunaona unaandika sana, na tunajua unaandika mambo ya maana, ila hatujui unachoandika. Inakuwa kama unatusahau marafiki zako wa-Marekani Weusi." Kwa kweli, ingawa mazungumzo yalikuwa ya kirafiki, na hata kiutani

Mteja Nimefurahia Huduma

Image
Leo nilipeleka gari langu kwenye kituo cha Car Time hapa mjini Northfield kubadilishiwa "oil." Kwa hapa Marekani, inashauriwa kubadili "oil" kila baada ya kuendesha gari maili 3000. Sijui utaratibu wa Tanzania. Kama ilivyo kawaida, nilipokewa vizuri, nikakaa sehemu ambapo wateja hungojea huduma. Baada ya dakika kama ishirini hivi, mtu aliyenipokea sehemu ya mapokezi alifika nilipokaa akachuchumaa kwa heshima zote na kuniambia kuwa mafundi walikuwa wamegundua kuwa gari langu linahitaji pia "tire rotation." Kwa kuogopa kuwa labda ingekuwa gharama ambayo sikujiandaa kuimudu, nilimwuliza kwa utaratibu iwapo itakuwa gharama kiasi gani. Alinijibu kuwa hiyo "tire rotation" haitanigharimu. Nilimjibu kuwa nashukuru kwa huduma hiyo. Dakika kama kumi tu baadaye. huyu jamaa aliiniita, kuniambia kuwa gari lilikuwa tayari. Alinikabidhi ufunguo na bili yangu, nikalipia, kisha nikashukuru na kuondoka zangu. Huu ndio utamaduni niliouona hapa Marekani wa

Namshukuru Msomaji

Image
Napenda kuweka kumbukumbu nyingine katika hii blogu yangu, kama ilivyo desturi. Wikiendi hii nimeona ujumbe kuhusu kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Ujumbe huu, ulioandikwa na Ruth Ann Baker kwenye mtandao wa Amazon, unasema: Learned some things I don't think I could find elsewhere. There is Lots of info on relationships and social etiquette. Nimenakili ujumbe kama ulivyoandikwa. Nimefurahi kusikia maoni ya mtu ambaye amekisoma kitabu. Namshukuru kwa kutumia muda wake adimu kuandika maoni yake, katika ukumbi ambapo watu duniani kote wanaweza kuusoma. Ni faraja kwangu ninapoona kuwa mtu baada ya kutumia fedha zake kukinunua kitabu, na muda wake katika kukisoma, anaona hajapoteza fedha wala muda. Ningejisikia vibaya sana iwapo hali ingekuwa kinyume, kama msomaji angeona amepoteza fedha zake na muda wake. Nimeona niandike hayo, kwani ni jadi yangu kufanya hivyo, kuwahakikishia wasomaji wa vitabu vyangu kwamba ninawaheshimu na ninawa

Nimepata Kitabu "Infidel" cha Ayaan Hirsi Ali

Image
Leo nimepata kitabu Infidel cha Ayaan Hirsi Ali ambacho nilikinunua mtandaoni tarehe 3 Juni. Ayaan alizaliwa Somalia, akakulia Somalia, Saudi Arabia, Ethiopia na Kenya. Kisha alihamia u-Holanzi, ambako aliwahi hata kuwa mbunge. Katika kukua kwake alianza kuhoji malezi ya ki-Islam aliyoyapata, na hatimaye alijitoa katika dini hii na kuwa mtu asiye na dini. Hayo amekuwa akisimulia katika vitabu na mihadhara yake. Kitabu chake cha kwanza, ambacho sina, ni The Caged Virgin: An Emancipation Proclamation for Women and Islam , ambacho Salman Rushdie amekielezea hivi: This is an immensely important book--passionate, challenging, and necessary. It should be read as widely as possible, because it tells the truth--the unvarnished, uncomfortable truth. Mtazamo wa Ayaan Hirsi Ali umemletea matatizo makubwa tangu mwanzo. Anatafutwa kuuawa. Alikuwa chini ya ulinzi u-Holanzi na hatimaye alihamia Marekani. Bado anaandika, anatoa mihadhara na anafanya mahojiano. Baada ya kusikia habari zake

Nimenunua "Muhammad:" Kitabu cha Deepak Chopra

Image
Jana nilipita kwenye duka la vitabu hapa Chuoni St. Olaf nikanunua kitabu kiitwacho Muhammad kilichotungwa na Deepak Chopra. Nilikiona juzi, nikawa nakiwazia, na jana nikaenda kukinunua. Deepak Chopra ni mwandishi maarufu, ambaye mawazo yake na mtazamo wake huwagusa watu sana. Ni mhamasishaji na mtoa ushauri kuhusu masuala mbali mbali ya maisha. Ninajua hayo, ingawa sina na wala sijasoma kitabu chake hata kimoja. Katika kukiangalia kitabu hiki cha Muhammad, nimeona kuwa Deepak Chopra ameandika pia kitabu juu ya Yesu na Buddha. Nikizngatia umaarufu wa mwandishi huyu, naona nijitahidi kusoma angalau hiki nilichonunua. Ninacho kitabu kingine kiitwacho Muhammad: A Biography of the Prophet , kilichotungwa na Karen Armstrong. Nilikipenda, na niliwahi kuandika juu yake katika blogu hii. Nikiona kitabu hiki cha Deepak Chopra kimenifaa, nitakiongelea pia. Blogu yangu hii ni uwanja huru kwa yoyote kutoa maoni yake. Ni uwanja huru kwa mijadala ya mada yoyote. Mara kwa mara ninaandika

Siku ya Mhadhara Chuo Kikuu Winona Inakaribia

Image
Siku hazikawii. Zimebaki siku kumi na moja tu kufikia siku ya mhadhara wangu Chuo Kikuu cha Winona, utakaotokana na utafiti wangu juu ya falsafa zilizomo katika masimulizi ya jadi kama inavyodhihirika katika kitabu changu cha Matengo Folktales . Niliandika taarifa ya awali ya mhadhara huu katika blogu hii. Leo nimeamka nikiwa nauwazia mhadhara huu kwa dhati. Nimejikuta nikijikumbusha mambo muhimu. Ninataka kwenda kutoa mhadhara madhubuti, wa kusisimua na kuelimisha. Hili huwa ni lengo langu kila ninapokubali mwaliko kama huu wa kwenda kutoa mhadhara popote. Ninatambua wajibu wangu wa kuitendea haki taaluma. Ni wajibu wangu kama mtafiti na mwalimu kuitendea haki taaluma. Ni wajibu wangu kuwa mfano wa kuigwa na vijana wanaotafuta elimu, kama hao vijana watakaonisikiliza Chuoni Winona. Ninatambua wajibu wangu wa kuwathibitishia wanaonialika kwamba hawakukosea kwa kunialika. Ninataka wasikilizaji wangu wakiri kuwa uamuzi wa kunialika ulikuwa sahihi. Sitaki wanaonialika na wanaonis

Kesi ya Raif Badawi: Mwanablogu wa Saudi Arabia

Image
Raif Badawi ni mwanablogu wa Saudi Arabia ambaye anafahamika sana duniani kutokana na kuhukumiwa kifungo cha miaka kumi gerezani na viboko 1000. Alihukumiwa kwa kile kilichoitwa kuitukana dini ya u-Islam. Amekaa gerezani miaka miwili na tayari alishapigwa viboko 50 nje ya msikiti mjini Jeddah. Adhabu hiyo si nyepesi; inaweza kusababisha kifo. Watu wengi duniani wanalaani hukumu hiyo. Wengi hawaoni ni kwa vipi Raif Badawi ameutukana u-Islam. Wengi wamechukizwa na hukumu hiyo kwa kuwa ni hujuma dhidi ya uhuru wa kutoa mawazo.  Mawazo ya Raif Badawi yaliyosababisha hukumu dhidi yake ni ya kawaida sana kwa vigezo vyetu wa-Tanzania na wengine duniani. Lakini wahusika nchini Saudi Arabia wameendelea kusisitiza kuwa Raif Badawi anastahili hukumu hiyo. Kuna tetesi kuwa huenda akashtakiwa upya ili apewe hukumu kali zaidi, kukatwa kichwa, hukumu ambayo hutekelezwa sana Saudi Arabia. Kesi ya Raif Badawi imeibua masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Saudi Arabia. Kuna mengi ya

"Song of Lawino:" Utungo wa Okot p'Bitek

Image
Sisi tuliosoma sekondari miaka ya mwishoni ya sitini na kitu na kuendelea tunaukumbuka utungo wa Okot p'Bitek, Song of Lawino , ambao ulichapishwa na East African Publishing House, mwaka 1966. Ni utungo uliotusisimua sana kwa namna mhusika wake mkuu, Lawino, alivyozielezea tofauti baina ya utamaduni wa asili wa kabila lake la Acholi, akifananisha na utamaduni wa ki-zungu ambao mume wake anaukumbatia. Lawino ana mtazamo wa aina yake, na anatumia lugha ya ucheshi na kejeli. Tuliosoma somo la"Literature" katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka ya sabini na kitu tulikuwa na bahati ya kufundishwa utungo huu na mwalimu Grant Kamenju wa Kenya, ambaye ufundishaji wake ulikuwa wa kusisimua fikra. Alitumia nadharia za akina Karl Marx, Frantz Fanon, Eldridge Cleaver, na wengine wa kimapinduzi katika kuchambua ujumbe wa Lawino. Alitujengea msimamo wa kuutambua ukoloni mamboleo kama alivyouelezea Fanon, hasa katika The Wretched of the Earth na  Black Skin, White Masks . Kit

Nimerekebisha Kitabu Changu

Image
Kwa zaidi ya wiki moja, nimekuwa nikikipitia kitabu changu cha Matengo Folktales kwa ajili ya kukiboresha. Rekebisho moja nililofanya ni kuongeza ukubwa wa herufi ili kitabu kisomeke kwa urahisi zaidi. Nilikuwa pia naangalia kama kuna kosa lolote katika uandishi wa maneno. Nimerekebisha dosari zilizoziona katika maneno yapata matano Ingawa nimetumia masaa mengi katika shughuli hiyo, kwangu si kitu, nikifananisha na kazi niliyofanya kwa miaka yapata ishirini na tatu katika kukiandaa kitabu hiki, tangu kuzitafuta na kuzirekodi hadithi, kuziandika kwa kuzitafsiri kwa ki-Swahili, kuzitafsiri kwa ki-Ingereza, kuzichambua, kusoma nadharia mbali mbali ili kutajirisha uchambuzi, na kurekebisha tafsiri na uchambuzi tena na tena. Bahati ni kwamba miaka ya sabini na kitu, nilianza pia kufundisha somo la fasihi simulizi ("Oral Literature") na nadharia ya fasihi (Theory of Literature") katika idara ya "Literature" ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Katika kufundisha ni

Mhadhiri wa Algeria Amefurahi Kupata Kitabu

Image
Jana, niliporejea kutoka kanisani, nilikuta ujumbe katika ukurasa wangu wa Facebook kutoka kwa Samir Zine Arab, mhadhiri wa "African Literature and Listening Skills" katika chuo kikuu cha Hassiba Ben Bouali Chlef, Algeria. Alikuwa anashukuru kupata nakala ya kijitabu changu, Notes on Achebe's Things Fall Apart ambayo nilimtumia siku kadhaa zilizopita. Ujumbe wake, ulioambatana na picha inayoonyesha kitabu pamoja na bahasha niliyotumia, kama inavyoonekana hapa kushoto, ameusambaza kwa marafiki zake wa Facebook ambao mimi ni mmoja wao. Amenigusa kwa namna alivyoandika: Dear friends, brothers and sisters! Today I'm the happiest man on earth! This morning I received a lovely book from a great professor Joseph Mbele! Thank you so much dear!! Pamoja na ujumbe huu, Mwalimu Samir ameniandikia pia ujumbe binafsi ambao nao umenigusa sana. Kwake na kwangu imekuwa ni furaha. Ninavutiwa na watu wa aina ya huyu mwalimu, ambao wana duku duku ya kutafuta elimu. Aliposikia t

Nimetoka Kanisani Kusali

Image
Ni Jumapili, saa sita na kidogo mchana. Nimetoka kanisani kusali. Mimi ni m-Kristu wa kawaida, m-Katoliki. Namwabudu Mungu na ninaamini kuwa yeye ndiye anayeongoza maisha yangu. Katika raha na matatizo, ninamtegemea yeye. Ninamshukuru kwa kunipa uhai siku hadi siku. Namshukuru Mungu kwa kunipa akili na utashi nitafakari mambo na kujiamulia. Ninamshukuru kwa jinsi anavyotuneemesha, kwa kuwaumba wanadamu wa kila aina, wenye dini mbali mbali, tamaduni na lugha mbali mbali. Dunia inapendeza kwa tofauti hizo, sawa na maua yanavyopendeza, kwa uwingi wa tofauti za rangi. Namshukuru Mungu kwa yote aliyoyaweka duniani: nchi kavu, bahari, milima, mabonde, mito, miti, majani na maua. Ametuwekea wanyama wa kila aina, ndege na wadudu, jua, mwezi na nyota, mvua na upepo, vitu vinavyoonekana na visivyoonekana. Vyote ni mazao ya uumbaji wa Mungu. Ninaomba niwe na moyo wa kuwapenda wanadamu wote na vyote alivyoumba Mungu. Ninaomba niwe mtu mwema, mwenye kutambua na kuzingatia kila siku kuwa Mungu

Ninaombwa Tafsiri ya Kitabu Changu

Image
Mara kadhaa, wa-Marekani wameniuliza iwapo kitabu changu Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kimetafsiriwa kwa ki-Swahili au wameniomba nikitafsiri. Hao ni watu ambao wameishi au wanaishi Afrika Mashariki, hasa kwa shughuli za kujitolea. Tangu nilipoanza kupata maulizo au maombi hayo, nimekuwa na wazo la kukitafsiri kitabu hiki. Mwanzoni kabisa, kwa kuzingatia uwingi wa wa-Somali walioingia na wanaendelea kuingia hapa Minnesota, ambao nimekuwa nikiwasaidia katika kuufahamu utamaduni wa Marekani, niliwazia kumwomba mmoja wa marafiki zangu wa ki-Somali atafsiri kitabu hiki kwa ki-Somali. Ninao marafiki kadhaa wa ki-Somali ambao, sawa na wa-Afrika wengine, wamekisoma na wanakipenda kitabu hiki. Lakini bado sijalitekeleza wazo hilo. Jana nimepata ujumbe wa aina hiyo kutoka kwa mama mmoja m-Marekani, ambaye simfahamu. Ninanukuu sehemu ya ujumbe wake, na nimeweka nukta nne mahali ambapo kuna maneno ambayo sijayanukuu: ....I hope one day that you will translate your

Kitabu "Africans and Americans" Kiko Manyara

Image
Kitabu changu Africans and Americans: Embracing Cultural Differences  ambacho kinafahamika kwa wasomaji wa blogu hii na blogu yangu ya ki-Ingereza, sasa kinapatikana Burunge Visitors Center(BVC) mkoani Manyara. BVC ilianzishwa kwa ajili ya kuratibu uhifadhi wa mazingira na kuendesha shughuli za utalii kwa manufaa ya jamii. BVC inatoa elimu kwa jamii na wageni kuhusu mazingira, historia, na utamaduni. Kwa mujibu wa shughuli zangu kama mtoa ushauri na mwelimishaji wa masuala ya utamaduni, ushirikiano na BVC ni jambo lenye mantiki ya wazi. Kwa hivi, tumechukua hatua hii ya BVC kujipatia vitabu vyangu ninavyovichapisha kwa jina la  kampuni yangu ya Africonexion: Cultural Consultants ili kiviuza katika duka lao. Watu walioko Tanzania wanaohitaji vitabu hivi wanaweza kutuma barua pepe: info@burungevisitorscentre.or.tz au imborutours@gmail.com  au kupiga simu zilizoorodheshwa kwenye tovuti:   http://www.burungevisitorscentre.or.tz/

Nadharia ya Uandishi

Image
Uandishi ni nini? Je, kila uandishi ni uandishi wa kweli? Uandishi wa kweli ni nini? Naona haya ni masuali ya msingi. Ningependa tuyatafakari. Waandishi wengi maarufu wameandika kuhusu masuala hayo. Katika kitabu chake,  Letters to a Young Novelist , Mario Vargas Llosa, mwandishi maarufu kutoka Peru, aliandika: The defining characteristic of the literary vocation may be that those who possess it experience the exercise of their craft as its own best reward, much superior to anything they might gain from the fruits of their labors. That is one thing I am sure of amid my many uncertainties regarding the literary vocation: deep inside, a writer feels that writing is the best thing that ever happened to him, or could ever happen to him, because as far as he is concerned, writing is the best possible way of life, never mind the social, political, or financial rewards of what he might achieve through it. Nitafsiri kwa ki-Swahili: Utambulisho mahsusi wa wito wa uandishi labda ni kwamb

Blogu Zangu Zimenisaidia

Hapa Chuoni St. Olaf kuna utaratibu unaomtaka kila mwalimu kuandika ripoti ya shughuli alizofanya katika mwaka wa shule unaoisha. Hizo ni shughuli za kitaaluma, yaani vitabu ulivyochapishwa, makala ulizochapisha, ushiriki wako katika mikutano ya kitaaluma, kazi ulizofanya katika uongozi wa vyama vya kitaaluma, kozi ulizotunga na kufundisha, uhariri katika majarida ya kitaaluma. Vile vile unaorodhesha huduma ulizotoa katika jamii nje ya chuo, kama vile ushauri ("consultancy"), na mihadhara katika mikutano ya vikundi na jumuia. Nimekuwa na jadi ya kuandika mambo ya aina hiyo katika blogu hii ya hapakwetu na blogu ya ki-Ingereza. Katika kuandika ripoti yangu ya mwaka unaoisha, blogu zangu zimekuwa hazina ya kumbukumbu na taarifa nilizohitaji. Huu ni uthibitisho wa manufaa ya shughuli ninayofanya ya kublogu. Ninakumbuka kuwa niliwahi kuelezea namna blogu ilivyonisaidia darasani. Watu wengine wanaandika kumbukumbu zao katika "diary." Lakini mimi kwa vile sina mazo