Posts

Showing posts from November, 2014

Kuhusu "Macbeth"

Image
Makala hii nilianza kuiandika mara tu baada ya kuanza kusoma Macbeth , tamthilia ya Shakespeare, ambayo niliitaja hapa na hapa . Jana usiku nimefika mwisho wake. Inafurahisha kujisomea namna hii, bila msukumo kutoka popote. Hapa na pale katika Macbeth nimejikuta nikiyakumbuka maandishi mengine ya Shakespeare ambayo niliyasoma zamani, kama vile The Merchant of Venice , Othello , The Tempest , na Twelfth Night . Hii ni kwa sababu kuna mawazo ambayo yanajitokeza tena na tena katika maandishi ya Shakespeare. Wazo mojawapo ni kwamba dunia ni jukwaa ambapo sisi wanadamu ni waigizaji. Kuna misemo pia ambayo inajitokeza tena na tena. Kwa mfano, nilivyosoma katika Macbeth kauli ya mchawi kuhusu meli kukumbwa na dhoruba (I, III, 25-26) nimekumbuka The Tempest . Nilivyokutana na usemi huu wa mfalme kwa kapteni shujaa: "So well thy words become thee as thy wounds; They smack of honor both," (I, II, 47-48) nimekumbuka hotuba ya Portia katika The Merchant of Venice , ambamo anaelez

Kitabu Changu cha Ki-Swahili

Image
Kitu kimoja ninachojivunia kama mwandishi ni juhudi niliyofanya kwa miaka mingi katika kuandika kwa ki-Swahili. Aliyenihamasisha na kunisukumia katika uandishi wa ki-Swahili ni rafiki yangu Mugyabuso Mulokozi, ambaye sasa ni profesa mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Tangu tulipokuwa tunasoma wote "Mkwawa High School," aliona jinsi nilivyokuwa nimezama katika ki-Ingereza bila kujibidisha upande wa ki-Swahili. Hatimaye, hasa tulipokuwa chuo kikuu, ambapo yeye nami tulikuwa tunafundisha, nilijitosa katika ulimwengu wa ki-Swahili. Kwanza nilisoma maandishi ya ki-Swahili, kisha nikaanza kufanya utafiti na kuandika makala magazetini. Kati ya maandishi niliyochapisha ni mapitio ya tamthilia ya Kijiji Chetu , iliyotungwa na Ngalimecha Ngahyoma. Baadaye, nilianza utafiti kuhusu tungo za zamani za ki-Swahili, kama vile Utenzi wa Fumo Liongo , Al-Inkishafi na Utenzi wa Ras il Ghuli . Utafiti huu niliuendeleza nilipokuwa nasomea shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Wiscon

Tuna Likizo Fupi ya "Thanksgiving"

Leo hapa chuoni tunaanza likizo fupi itakayokwisha mwisho wa wiki. Ni wakati wa sikukuu maarufu hapa Marekani iitwayyo "Thanksgiving." Kwa mwaka huu, "Thanksgiving" ni keshokutwa, tarehe 27. Kwa upande wangu, nilianza hayo mapumziko jana mchana, baada ya kufanyisha mtihani katika somo langu la "South Asian Literature." Kwa hivi, kipindi hiki ambacho ni cha mapumziko sitapumzika, bali nitakuwa nasahihisha huo mtihani. Vile vile, wakati huu ambapo hatufundishi, ninaendelea kujisomea maandishi mbali mbali, hasa tamthilia ya Macbeth . Ninangojea kwa hamu kuandika ripoti yake wiki hii hii katika blogu hii. Pamoja na jukumu la kusahihisha mtihani, naona akili yangu imetulia vizuri, kiasi cha kuniwezesha kuitafakari tamthilia ya Macbeth na kuifaidi vilivyo. Nikirudi kwenye hii sikukuu ya "Thanksgiving," ningeweza kusema mengi kuhusu historia yake, pia malumbano na migogoro ya kiitikadi ambayo imeigubika sikukuu hii hasa miaka ya hivi karibuni.

Mwaliko wa Profesa Barbara Zust

Image
Asubuhi hii, nimefika ofisini na kukuta ujumbe kutoka kwa Profesa Barbara Zust wa Chuo cha Gustavus Adolphus , Minnesota. Ananiulizia iwapo naweza kwenda kuongea na wanafunzi wake tarehe 4 au 5 Januari, katika matayarisho yao ya kwenda Tanzania kimasomo. Nimempigia simu, tukakubaliana niende tarehe 5. Profesa Zust amenialika mara kwa mara anapoandaa wanafunzi wake kwa safari ya Tanzania. Nimewahi kuandika taarifa hizo, kwa mfano hapa , hapa , na hapa . Wanafunzi hao huwa wamesoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Mihadhara yangu huhusu masuala ninayoongelea kitabuni, nami hupenda sana kujibu au kujadili masuali wanayokuwa nayo. Nimefurahi kwa jinsi Profesa Zust alivyonieleza umuhimu wa mikutano yangu na wanafunzi hao. Nimefurahi pia kuwa yeye na wanafunzi wanaona ninachofanya kina faida kubwa kwao. Ni wazi kuwa, ingekuwa hawafaidiki, hawangekuwa wananialika tena na tena. Kwa hivi, siku yangu ya leo imeanza vizuri, nami nimeona niweke kum

Nilivyohojiwa na Radio Butiama Kuhusu Kitabu Changu

Image
Nimewahi kuandika kuwa kama mwandishi, najikuta nikialikwa kuongelea maandishi yangu, na pengine kuongelea kitabu maalum. Hayo niliandika katika blogu hii Wakati mwingine, mwandishi unaalikwa kwenye mahojiano katika vyombo vya habari. Nami nimewahi kuhojiwa katika redio, blogu, na magazeti. Hapa naleta mahojiano niliyofanyiwa mwaka 2006 na m-Tanzania Deus Gunza, ambaye alikuwa anamiliki na kuendesha Radio Butiama, kule Columbus, Ohio. Mahojiano hayo ya papo kwa papo yalihusu kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Yasikilize mahojiano haya hapa: http://butiama.podomatic.com/entry/2006-09-02T06_26_37-07_00

Ninasoma Vitabu Kiholela

Image
Jana, baada ya kufundisha darasa langu la South Asian Literature, nilikuwa ofisini kwa muda, nikawa napekuapekua bila lengo maalum katika makabati ya vitabu vyangu. Niliamua, kiholela tu, kuchukua tamthilia ya Macbeth ya Shakespeare, nikarudi nayo nyumbani na kuanza kuisoma. Nilikuwa na hamu ya kujikumbusha enzi za ujana wangu, nilipokuwa nasoma sekondari hadi chuo kikuu. Nilipenda kusoma vitabu vya waandishi mbali mbali, kama vile Shakespeare na Charles Dickens. Leo asubuhi, nilipoamka, niliendelea kusoma Macbeth , lakini nikakumbuka kuwa kuna vitabu kadhaa ambavyo nilianza kuvisoma au nilikuwa navisoma siku kadhaa zilizopita, au wiki kadhaa zilizopita, au miezi kadhaa iliyopita, ambavyo sikuvimaliza. Mifano ni A Moveable Feast na Islands in the Stream , vilivyoandikwa na Ernest Hemingway; Lost For Words , kilichoandikwa na J.W. Patrick Creber, na Nomad , kitabu cha Ayaan Hirsi, yule dada m-Somali anayetishiwa maisha yake kwa vile anaukosoa u-Islam. Hiyo ni mifano tu ya viporo.

Naulizwa Malipo ya Mihadhara Yangu

Hapa Marekani, mtu unapoalikwa kwenda kutoa mhadhara, nawe ukakubali, huwa unaulizwa malipo yako ni kiasi gani. Hapo unawatajia kiwango cha malipo unayotegemea. Unazingatia umaarufu wako, na wale wanaokualika wanategemea uwatajie kiwango chako bila maneno zaidi. Hata siku chache zilizopita, nilipoletewa mwaliko wa kwenda kutoa mhadhara mjini Zumbrota, niliulizwa malipo yangu ni kiasi gani. Miaka yapata mitano iliyopita, kwa nyakati tofauti, nilipata wasaa wa kuongea na wa-Marekani wawili wenye wadhifa katika jamii kuhusu suala hili. Tulikuwa katika mazungumzo kuhusu shughuli zangu za uandishi na utoaji mihadhara katika jumuia na taasisi mbali mbali. Ndipo wakaja na hili wazo la malipo. Ingawa waliongea nami kwa nyakati tofauti, wote walisema kuwa kufuatana na umaarufu niliokuwa nao wakati ule, nilikuwa na haki ya kutegemea kiasi cha dola 2,500 au 3,000 kwa mhadhara. Kwangu, huu umekuwa ni mtihani miaka yote. Sijaweza kutaja hata siku moja nilipwe kiasi gani. Ukiniuliza sababu zangu

Mwandishi Unapoitwa Kuongelea Kitabu Chako

Image
Siku hizi, mara kwa mara, nawazia jukumu linaloningoja, la kwenda mjini Zumbrota, Minnesota, kutoa mhadhara. Mada ni "Incorporating Immigrants into our Culture and Worship," kama nilivyoeleza katika blogu hii . Mwaliko wa kutoa mhadhara huu umetokana na kitabu nilichoandika, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Sikualikwa nikaongelee kitabu hiki, lakini kwa hali yoyote, baadhi ya yaliyomo kitabuni yatajitokeza katika mhadhara na katika kipindi cha majibu na masuali. Napenda kusema machache kuhusu jukumu la kutoa mhadhara kuhusu kitabu ulichoandika. Mara nyingi, hutokea kwamba watu utakaozungumza nao wanakuwa wameshakisoma kitabu. Ni lazima utafakari kabla kwamba utaongelea nini, na jambo hilo hutegemea aina ya kitabu. Kama ni riwaya, watu hutegemea utawaeleza mambo kama vile nini kilikuwa chanzo cha wewe kuandika, yaani nini kilichokufanya uandike, njia uliyopitia katika kuandika, maandishi au waandishi waliokuathiri, matatizo uliyokumbana nayo, na mam

Kuhusu Kunyanyaswa kwa Jaji Warioba

Kati ya mambo yaliyonishtua sana mwaka huu ni kunyanyaswa kwa Jaji Warioba. Kadhia hii imetokana na kazi murua aliyofanya Jaji Warioba na tume yake ya kukusanya mawazo ya wananchi kuhusu Katiba Mpya. Kumekuwa na mlolongo wa matukio kadhaa ya unyanyasaji huo, ambao, kwa kadiri ninavyofahamu, mwanzilishi wake ni Ikulu. Tukio la kupigwa Jaji Warioba mkutanoni, ambalo limeripotiwa sana, ni kilele cha utovu huu. Wengi tunaamini kuwa Jaji Warioba ananyanyaswa kwa sababu ya uwazi na uwakilishi wa mawazo ya wananchi, jambo ambalo ni mwiba kwa mafisadi. Nimeshtushwa vile vile na kauli ya Rais Kikwete kuhusu tukio hili la vurugu na kupigwa Jaji Warioba. Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, Rais Kikwete aliishia tu kusema kuwa anaomba yasimkute yaliyomkuta Jaji Warioba. Sikuona popote kama aliongelea suala hili kwa undani na mapana kama linavyostahili. Yeye kama Rais, nilitegemea kwanza atambue kuwa vurugu zile ni aibu kwa nchi anayoiongoza. Nilitegemea awakemee walioleta vurugu zile

Nimealikwa Kutoa Mhadhara

Siku chache zilizopita, nilipigiwa simu kutoka Faribault, kwenye Kanisa la First English Lutheran Church. Wananiuliza iwapo nitaweza kwenda kutoa mhadhara katika Cannon River Conferenc utakaofanyika mwezi Aprili mjini Zumbrota, Minnesota. Mada ya mkutano itakuwa "Incorporating Immigrants Into our Culture and Worship," na mhadhara wangu unatarajiwa kuwa dira ya mkutano. Miaka kama sita hivi iliyopita, nilialikwa First English Lutheran Church, Faribault, kutoa mihadhara kuhusu yale niliyoandika katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Nimefurahi kuwa mihadhara yangu ile inakumbukwa, tena mama aliyenipigia simu alinikumbusha kuwa anaikumbuka baadhi ya michapo yangu na pia kitabu changu. Hata hivi, kwenye mkutano kama huu wa Zumbrota, mada sio niliyoandika katika kitabu changu, ingawaje nitakitumia kama msingi mojawapo wa kuijadili mada niliyopewa. Patakuwepo pia na muda wa masuali na majibu.  Huu mkutano wa Zumbrota utawaleta pamoja wana

Nililazwa Tena Hospitalini

Kwa siku kadhaa, sikuandika chochote katika blogu zangu: hii na ile ya ki-Ingereza . Inapokuwa hali ni hiyo, wasomaji hujiuliza kuna nini. Nilikuwa nimelazwa tena, kwa wiki moja, katika hospitali ya Allina Abbott Northwestern, kule Minneapolis. Baada ya kuachiwa, nimekuwa nikipumzika. Kesho nategemea kuanza tena kufundisha. Chuo ambacho ni mwajiri wangu , kwa maelekezo ya daktari, kimenipunguzia sana majukumu, kuliko hata nilipoachiwa kutoka hospitalini miezi kadhaa iliyopita. Nitakuwa nafundisha kozi moja tu, "South Asian Literature." Mungu ni mkubwa na madaktari wanajua wanachofanya. Wananiambia kuwa hatimaye, hata kama ni baada ya miezi kadhaa, wana imani watayatatua matatizo ya afya yangu. Baada ya kurekebisha  matatizo mengine, sasa wanashughulikia figo. Wamenihimiza niendelee kufundisha, wakati wao wanashughulikia matatizo hayo. Kama kawaida, nawashukuru wote wanaonikumbuka katika maombi na salaam. Nimeona nilete taarifa hii, kuelezea hali yangu, na kwa kuzing