Elimu ya Kijijini
Makala hii ilichapishwa katika gazeti la KWANZA JAMII Profesa Joseph L. Mbele Mara kwa mara nakumbuka elimu niliyopata kijijini, kabla ya kuanza shule. Wengi wetu tulipitia njia hiyo. Ni elimu gani hiyo? Tangu utotoni, tulipata maelekezo kutoka kwa wazazi kuhusu mambo mbali mbali, kufuatana na umri, kuanzia namna ya kuvaa hadi namna ya kula kwa adabu na kuwasalimia watu. Baadaye wavulana tulijifunza kuchunga mbuzi na ng’ombe, na kutandika nyasi kwenye zizi la ng’ommbe, na kukamua maziwa. Wasichana walifundishwa kazi za jikoni na kulea watoto. Kama ilivyo kwa watoto wengine, baba na mama walikuwa wananituma kufanya shughuli hii au ile. Hata majirani walikuwa wanatutuma sisi watoto kuwasaidia shughuli mbali mbali. Yote hii ilikuwa ni sehemu ya elimu yetu. Nilipokua kidogo nilianza kushiriki katika kilimo. Nilijifunza kulima, kupanda, kupalilia, na kuvuna mazao. Nilijifunza kuchuma kahawa na kuishughulikia baada ya hapo. Shughuli hizi ziliniwezesha kufahamu zaidi habari za udongo, n