Posts

Showing posts from September, 2015

Kampeni za CCM Mwaka Huu

Image
Najaribu kutafakari picha hii iliyopigwa katika moja ya mikutano ya kampeni za uchaguzi zinazoendelea Tanzania.  Ina maana kwamba mwenye uwezo wa kupiga "push-up" nyingi ndio anafaa kuwa kiongozi? Je, ili uukwae ubunge, unatakiwa upige angalau "push-up" ngapi? Udiwani je? Na ili uwe waziri, unahitaji "push-up" ngapi? Na kwa uwaziri, ni sahihi tuwe na "push-up" tu au na kuruka viunzi pia? Na kwa kuzingatia uzito wa cheo cha uwaziri, kwa nini tusiongezee pia uwezo wa kunyanyua matofali angalau manne ya zege? Kwa kweli, tukifanya hivyo, tutapata serikali imara kabisa.

Tumechangia Kanisa la Venezuela

Leo kanisani kwetu hapa mjini Northfield, kanisa Katoliki, tulikuwa na padri ambaye anatumikia kanisa fulani nchini Venezuela. Huyu padri ni m-Marekani, na kwa miaka yapata arobaini, mapadri wa-Marekani wamekuwa wamisionari katika kanisa hilo la Venezuela. Hata paroko wetu aliwahi kutumikia kanisa hilo kwa miaka mitano. Ananivutia kwa jinsi anavyoijua lugha ya ki-Hispania, na anawahudumia waumini hapa Northfield wanaotumia lugha hiyo. Huyu padri mgeni alitoa mafundisho mazuri, na katika kuelezea utume wake Venezuela alituhimiza kwa maneno matatu: "Pray, say, pay." Alifafanua kwamba tusali kuwaombea waumini wa kanisa lile la Venezuela, tuwaeleze wengine kuhusu hali halisi na mahitaji ya kanisa lile, na tutoe mchango kulisaidia kanisa lile. Niliguswa na maelezo yake, nikangojea muda wa kutoa mchango. Kilipopitishwa kijikapu cha mchango, nilikuwa tayari nimekwangua vijihela vilivyokuwemo katika pochi yangu nikavitumbukiza humo. Nilijisikia faraja na furaha kwamba vijihela h

Nimehojiwa Kuhusu Hemingway na "Papa's Shadow"

Image
Leo nimekuwa na mahojiano na mwandishi wa gazeti la Manitou Messenger linalochapishwa hapa chuoni St. Olaf. Ni gazeti la wanafunzi, ambalo limekuwa likichapishwa kila wiki kwa miaka 125. Mahojiano yetu yalikuwa juu ya filamu ya Papa's Shadow. Katika ujumbe wa kuomba mahojiano, mwandishi aliandika: ... we are doing a feature article this week on the documentary, Papa's Shadow and Ramble Pictures. We learned that you were instrumental in the inspiration for and production of this film, and we were hoping you could answer a few quick questions. Katika mahojiano, tumeongelea nilivyoanza kuvutiwa sana na mwandishi Ernest Hemingway, nilipoombwa na Thomson Safaris kuongoza msafara mkubwa wa wanafunzi, wazazi na walimu, katika safari ya Tanzania mwaka 2002. Hatimaye, baada ya miaka mitano ya kusoma maandishi na habari za Hemingway, nilitunga kozi Hemingway in East Africa, kwa ajili ya Chuo cha Colorado. Baadaye, niliona niunde kozi hiyo kwa ajili ya wanafunzi wa Chuo cha S

"Papa's Shadow" Yapongezwa na Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa

Image
Tarehe 20 mwezi huu nilipeleka ujumbe Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa kuhusu filamu ya Papa's Shadow. Sikuandika ujumbe mrefu, bali niliwatumia kiunganishi hiki. Bila kuchelewa, tarehe 22 nilipata ujumbe kutoka kwao, ukiwa umeandikwa na Ndugu Noel Kabanda. Uwakilishi unaafiki kuwa Papa's Shadow ni "fursa maridhawa ya kuitangaza Tanzania ulimwenguni" na unasisitiza kuwa "Serikali inatambua mchango wa sanaa katika kuitangaza Tanzania katika sekta mbali mbali ikiwemo utalii na utamaduni." Kwanza, kwa kuzingatia uwingi wa majukumu yanayowakabili wawakilishi wetu katika balozi zetu, nimeona ni muhimu kusema nilivyoguswa na jinsi Uwakilishi ulivyoushughulikia ujumbe wangu. Pili, ujumbe wa Uwakilishi unawatia moyo wahusika wa Ramble Pictures, ambao ndio watengeneaji wa Papa's Shadow. Timu nzima ya Ramble Pictures ni vijana wa ki-Marekani, na baadhi yao walikuja Tanzania mwaka 2013 kwenye kozi yangu ya Hemingway Katika Afrika Ma

Nimenunua Kitabu cha Golding, "Lord of the Flies"

Image
Zimepita siku nyingi kidogo tangu niandike ujumbe kuhusu vitabu nilivyonunua, au nilivyojipatia kwa namna nyingine. Viko vitabu kadhaa, hasa riwaya, ambavyo sikuvielezea. Leo, baada ya kufundisha vipindi vyangu viwili, nilipita kwenye duka la vitabu la hapa chuoni. Niliangalia sehemu vinapouzwa vitabu kwa bei nafuu, nje ya duka, nikaona, kati ya vitabu vingi, kitabu cha William Golding, Lord of the Flies .  Hapo hapo nilikumbuka miaka ya ujana wangu. Tulisoma kitabu hiki tulipokuwa kidatu tano Mkwawa High School, mjini Iringa. Huku nikikumbuka hayo yote, nilikinunua hima, ingawa nina hakika ninayo nakala nyingine niliyonunua zamani, ila itakuwa vigumu kuigundua ilipo katika utitiri wa vitabu vyangu. Lord of the Flies ni riwaya niliyoipenda sana na ambayo ninaikumbuka sana. Ilinigusa kwa namna ya pekee kwa jinsi ilivyowachora wahusika, ambao ni watoto wa shule waliojikuta kwenye kisiwa peke yao baada ya ndege waliyokuwa wanasafiria kuanguka kisiwani humo na wao wakawa abiria peke

Tafsiri ya Sala ya Papa Francis

Image
Katika ujumbe wangu wa jana, niliweka sala ya Baba Mtakatifu Francis ya kuiombea dunia. Sala hii inagusia na kujumlisha mambo mengi, kama vile upendo kwa wanadamu wote na viumbe vyote bila mipaka, kuwajali wasiojiweza, kuyatunza na kuyaboresha mazingira. Sala hii inatuelekeza kumwomba Mungu atupe ufahamu wa thamani ya kila kiumbe, ufahamu na namna maisha yetu yalivyofungamana na maisha ya viumbe vyote. Aidha, sala inathimiza kumtegemea Mungu katika juhudi zetu za kutafuta haki, upendo, na amani. Katika sala hii kuna mafundisho muhimu ya dini mbali mbali, matarajio ya wanaharakati wa masuala mbali mbali ya jamii, na matarajio ya wanamazingira. Ni sala inayofundisha busara za zamani za jamii mbali mbali, kama vile wenyeji wa asili wa Amerika ("Native Americans"). Wazo lililomo katika sala hii la kuviangalia viumbe vyote kwa uchaji linanikumbusha falsafa ya mwandishi Shaaban Robert. Kati ya sentensi zinazonigusa kwa namna ya pekee katika sala hii ni, All-powerful God, you

Nimerejea Kutoka Kanisani

Image
Nimetoka kanisani kusali, na ninaona ni sawa tu kuandika habari hiyo hapa katika blogu yangu. Hii si mara ya kwanza kwangu kuandika habari ya namna hiyo. Kwanza napenda kuwajulisha ndugu, marafiki na wote wanaofuatilia habari zangu, kwamba afya yangu imeendelea kuwa bora. Zaidi ya huu mkongojo ninaotembea nao, uonekanao pichani, hakuna dalili ya tatizo. Naendesha gari mwenyewe, hata umbali mrefu. Natembea na mkongojo kwa kuwa daktari anataka nitembee nao. Nina kila sababu ya kumshukuru Mungu. Kama ilivyo kawaida, katika ibada ya misa ya leo tumewaombea watu wote. Tumewakumbuka waumini wenzetu wanaosali makanisani, misikitini, na katika nyumba za ibada za dini zingine, tukiombea amani ulimwenguni. Wa-Katoliki hatujiombei wenyewe tu, bali wanadamu wote. Kila Jumapili, tangu Baba Mtakatifu wa sasa, Papa Francis II, alipotoa waraka wake wa kichungaji, Laudato Si , tumekuwa tukisali sala yake ya kuiombea dunia: A prayer for our earth All-powerful God, you are present in the whole

Filamu ya "Papa's Shadow:" Fursa ya Kuitangaza Tanzania

Image
Nina furaha kuandika kuhusu filamu ambayo imeandaliwa iitwayo "Papa's Shadow," inayomhusu mwandishi maarufu Ernest Hemingway. Katika filamu hiyo, ninaonekana nikiongea na Mzee Patrick Hemingway, ambaye ni mtoto pekee wa Ernest Hemingway aliye hai. Ana umri wa miaka 87. Tunaongelea maisha, safari, maandishi na fikra za Hemingway, hasa kuhusu Afrika. Sehemu nyingi hapa duniani ambako Hemingway alipita au kuishi na akaandika habari zake, zimejipatia umaarufu. na zinafaidika hasa katika utalii. Mifano ni Cuba na mji wa Pamplona nchini Hispania. Watu wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla tuna bahati hiyo, kwani Hemingway alikuja na kuishi kwetu mara mbili, mwaka 1933-34 na 1953-54, akaandika vitabu, hadithi, insha na barua kuhusu aliyoyaona. Filamu ya "Papa's Shadow" ilitokana na kozi niliyofundisha Tanzania mwezi Januari mwaka 2013 juu ya Hemingway. Kozi ile ilimhamasisha Jimmy Gildea, mmoja wa wanafunzi wangu, kutengeneza filamu hiyo. Alianzisha kamp

Wazo Kuhusu Kuchagua Kiongozi

Image
Tunavyoelekea kwenye uchaguzi, mwezi ujao, nchini Tanzania, tunaona malumbano yanashamiri. Tunataka kujua nani anafaa kuwa kiongozi. Napenda kuchangia kifupi malumbano haya. Mchango wangu unasimama katika taaluma na utafiti. Suala la uongozi linaingia moja kwa moja katika utafiti juu ya akili na saikolojia. Miaka yetu hii, watafiti wamekuwa wakituambia kuwa kuna aina nyingi za akili. Kuna maandishi mengi juu ya suala hilo, ambalo kwa ki-Ingereza linajulikana kama "multiple intelligence" au "multiple intelligences." Kwa mujibu wa utafiti huo, uongozi unahitaji aina ya akili iitwayo "emotional intelligence." Ni akili inayomfanya mtu awe na mvuto kwa watu kwa haiba na mwenendo wake, uwezo wa kuunganisha watu, uwezo wa kuwafanya wafuate njia fulani kwa kutumia ushawishi, si vinginevyo. Mtu mwenye "emotional intelligence" kubwa ndiye anayefaa kuwa kiongozi. Katika malumbano yanayoendelea miongoni mwa wa-Tanzania wakati huu wa kuelekea uchaguzi,

Vijana Wameonana Na Mzee Patrick Hemingway

Image
Leo nimepata ujumbe na picha kutoka kwa Jimmy Gildea, anayeonekana kushoto kabisa pichani hapa kushoto, kwamba walikuwa mjini Bozeman, Montana, wakingojea kuonana na Mzee Patrick Hemingway na mkewe Mama Carol. Jimmy alikuwa ni mmoja wa wanafunzi wangu katika kozi ya Hemingway in East Africa ambayo nilifundisha Tanzania mwezi Januari mwaka 2013. Kutokana na kozi ile, na pia safari tuliyofunga kwenda Montana kuonana na Mzee Patrick Hemingway, Jimmy ametengeneza filamu iitwayo Papa's Shadow, ambayo kwa kiasi kikubwa inatokana na kozi ile. Katika filamu hii, ambayo si ya maigizo, Mzee Patrick Hemingway na mimi tunaongelea maisha na maandishi ya baba yake, Ernest Hemingway, na tunaongelea kwa undani zaidi maisha na mizunguko yake Afrika Mashariki, miaka ya 1933-34 na 1953-54, na pia falsafa yake kuhusu masuala ya maisha na uandishi. Katika kutengeneza filamu hiyo, Jimmy ameshirikiana na hao vijana wanaoonekana pichani, na wengine ambao hawamo pichani. Nimetamani sana kama nami

Udini Katika Kampeni za Urais

Image
Katika kipindi hiki cha kampeni za urais nchini Tanzania, tunashuhudia mengi. Kwa mfano, kwa siku mbili tatu hivi tumekuwa tukisikia shutuma nyingi dhidi ya mgombea wa UKAWA, Edward Lowassa kwamba anafanya udini. Chanzo cha shutuma ni kauli anayoonekana akitoa katika video alipokuwa anaongea na waumini wa ki-Luteri. Anasikika akiomba wamwunge mkono, awe m-Luteri wa kwanza kuwa rais. Kauli hiyo imewasha moto miongoni mwa wapinzani wake, kwa mfano CCM. Wamekazana kupaaza sauti wakisema kuwa mgombea huyu hafai; anatugawanya kwa msingi wa dini, na atatuletea maafa akiwa rais. Binafsi, sioni kama watu hao wana hoja ya msingi. Lowassa hana tabia hiyo inayosemwa. Tumemshuhudia kwa miaka anavyojumuika na waumini wa dini mbali mbali katika shughuli zao. Tumemwona akiongoza harambee za kuchangia misikiti na makanisa ya madhehebu mbali mbali sehemu mbali mbali za nchi. Kwa kufahamu alivyo na ushawishi mkubwa, viongozi na waumini wa dini mbali mbali wanafurahi kumwalika kwenye shughuli zao

Gazeti la "MwanaHalisi" Lafunguliwa

Image
Nimefurahi kuona taarifa kuwa mahakama kuu ya Tanzania imeamuru kufunguliwa kwa gazeti la MwanaHalisi ambalo serikali ya CCM ililifungia mwaka 2012. Ni ushindi kwa mmiliki wa MwanaHalisi , Saed Kubenea, na timu yake. Ni ushindi kwa watetezi wa uhuru wa vyombo vya habari. Nilikuwa mmojawapo wa watu waliopinga wazi wazi  hatua ya serikali ya kulifungia gazeti la MwanaHalisi . Ninasimamia uhuru wa kutoa mawazo, uhuru wa waandishi, kama ilivyofafanuliwa katika tangazo la kimataifa la haki za binadamu. Taarifa tulizozipata leo ni kwamba mahakama imetamka kwamba ni juu ya Saed Kubenea kuamua kuendelea kuchapisha gazeti lake au kutoendelea. Vile vile, mahakama imeacha mlango wazi kwa Saeed Kubenea kuishtaki serikali na kudai fidia kwa kipindi chote ambapo gazeti lake lilikuwa limezuiwa. Ni wazi kwamba, endapo Saed Kubenea atadai fidia, ambayo ni haki yake, walipa kodi wa Tanzania watabeba mzigo mkubwa. Labda watajifunza hasara ya kuiweka madarakani serikali isiyo makini, isiyoheshimu

Hotuba ya Dr. Wilbroad Slaa Kuacha Siasa

Kuhusu hotuba ya Dr. Slaa kwa waandishi wa habari akitangaza kuondokana na siasa, mengi muhimu yamesemwa na wenye upeo na tafakari nzito kunizidi. Ila nami kama raia mwingine yeyote, nina uhuru kamili wa kuongelea suala hili, kama mwananchi anavyoongea mtaani, ambayo ni haki yake. Napenda nianze kwa kujikumbusha kwamba kwa miaka mingi, CCM wamekuwa wakimbeza Dr. Slaa, kwamba ni mzushi na mropokaji. Alipoanza kusema kuna ufisadi, CCM walimkatalia katakata, wakasema ni mzushi. Baadaye, vijana wa UVCCM wakawa wanafanya kibarua cha kumtukana Dr. Slaa. Sasa, baada ya huyu mzushi na mropokaji kutema cheche juzi, mbele ya waandishi wa habari, nasubiri kuwasikia CCM wanasemaje. Wakisema tumpuuze kwa vile ni mzushi na mropokaji, basi ina maana kuwa UKAWA hawana sababu ya kukosa usingizi wala kujibishana naye. Kwa nini mtu ukose usingizi kwa sababu ya maneno ya mtu anayefahamika wazi kuwa ni mzushi na mropokaji? Nitawashangaa CCM iwapo watashangilia mashambulizi ya Dr. Slaa dhidi ya Lowass