Posts

Showing posts from July, 2014

Vitabu Nitakavyoonesha Katika Tamasha la Afrifest, Agosti 2

Image
Kila mwaka wakati wa tamasha Afrifest , ninakuwa na meza ambapo naonesha vitabu vyangu na machapisho mengine. Meza ya vitabu huwavuta watu waje hapo. Kwa kawaida, mbali ya kutaka kunifahamu na kufahamu shughuli zangu, watu wanaofika hapo huwa na hamu ya kujua vitabu vinahusu nini. Wengi huvishika wao wenyewe na kuangalia ndani. Kwa mawazo yangu, hiyo si fursa ya kuvipigia debe vitabu hivyo. Ninachofanya ni kujibu masuali niulizwayo. Kama suali linahusu kitabu au vitabu moja kwa moja, naelezea pia chimbuko la kitabu na uhusiano wake na shughuli zangu. Ninaposema shughuli zangu, ninamaanisha ufundishaji wa fasihi na lugha ya ki-Ingereza, utafiti katika masimulizi ya jadi, uandishi, utoaji wa ushauri kuhusu tofauti za tamaduni kwa wa-Marekani waendao Afrika. Pia naongelea kuhusu kuwaandaa wanafunzi na kuwapeleka katika safari za masomo Afrika. Kwa namna moja au nyingine, masuala ya aina hiyo yanajitokeza katika vitabu vyangu. Ni kawaida kwamba mtu anayekuja kwenye meza yangu anakuwa

Kitabu Kimefika Salama Dar es Salaam

Image
Leo nimefurahi kumsikia mwanablogu Bwaya akielezea kuwa amepata kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences , ambacho nilimpelekea Dar es Salaam, tarehe 14 Julai. Ameandika taarifa hii kwenye ukurasa wake wa Facebook na pia katika blogu yake, na sehemu zote mbili ameambatanisha picha inayoonekana hapa kushoto. Ni picha ya kitabu na pia bahasha ambayo nilitumia kitabu hiki. Nimefurahi kwamba kitabu kimefika salama, kwani jana nilianza kuwa na wasi wasi kuwa labda kimepotelea njiani. Namshukuru Ndugu Bwaya kwa kutoa taarifa hima alipopata, kama alivyoahidi. Kwa taarifa zaidi, pitia blogu ya Jielewe

Leo ni Kumbukumbu ya Kuzaliwa Hemingway

Image
Leo ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Ernest Hemingway. Alizaliwa tarehe 21 Julai, 1899, Oak Park, kitongoji cha Chicago. Hemingway ni mwandishi maarufu pengine kuliko wote walioandika ki-Ingereza katika karne iliyopita, na bado yuko juu sana. Anasifika kwa mengi, ikiwemo kuasisi mtindo wa uandishi ambao wengi wameufuata, hasa msisitizo katika uandishi wa sentensi fupi. Haiwezekani kwa mtu yeyote kukumbuka tarehe za kuzaliwa kwa kila mtu maarufu. Imekuwa bahati tu kuwa nimekumbuka kuwa leo, tarehe 21 Julai, ndio tarehe ya kuzaliwa Hemingway. Hemingway ni mwandishi ambaye maandishi yake nayasoma sana, pia maandishi ya wengine kumhusu yeye, na tahakiki mbali mbali za maandishi yake. Kitu kimoja kinachonivutia sana ni kauli mbali mbali za Hemingway kuhusu masuala kadha wa kadha ya maisha, uandishi, falsafa, na kadhalika. Ukizingatia kwamba Hemingway alipenda sana kunywa, hebu fikiria, kwa mfano usemi wake huu: "I drink to make other people more interesting." Alisema

Tunajiandaa kwa Tamasha la Afrifest, Agosti 2

Image
Kila mwaka, tangu mwaka 2007, nahudhuria tamasha la Afrifest , ambalo hufanyika hapa Minnesota, Marekani. Imewahi kutokea kwamba nilikuwa Tanzania wakati wa tamasha hilo. Binti zangu wananiwakilisha.Wanafahamu vizuri shughuli zangu, na wanawaeleza watu wanaoulizia kuhusu shughuli zangu na vitabu vyangu. Hizo "ti-sheti" tulizovaa zina nembo ya kikampuni changu kiitwacho Africonexion: Cultural Consultants, ambacho najaribu kukijenga. Hapa kushoto anaonekana Deta, binti yangu wa kwanza. Siku hiyo sikuwepo. Hapa kushoto anaonekana Zawadi, binti yangu wa mwisho, akiwa anangojea watu. Hapo ni wakati alipokuwa mdogo. Alianza kuipenda shughuli hii tangu alipokuwa mdogo sana. Alikuwa akifuatana nami kwenye matamasha ya utamaduni, akinisikiliza ninapoongea na watu. Tangu akiwa na umri ule mdogo, aliweza kuwaeleza watu kuhusu shughuli zangu na kuhusu vitabu vyangu. Kwa mfano, katika mji wa Faribault kulikuwa na tamasha la tamaduni, nami nikiwa Tanzania. Zawadi a

Ninasoma Vitabu Vitatu kwa Mpigo

Image
Siku hizi, nimekuwa nikisoma vitabu vitatu kwa mpigo. Kitabu kimojawapo ni A Moveable Feast cha Ernest Hemingway. Hiki ni kati ya vitabu vya Hemingway vilivyochapishwa baada ya kufariki kwake. Mswada wa kitabu hiki ulihaririwa kwanza na Mary Welsh, mke wake wa nne na wa mwisho, ukachapishwa mwaka 1964. Mimi ninasoma toleo jipya la mswada huu, ulivyohaririwa na Sean Hemingway, na kuandikiwa utangulizi na Patrick Hemingway. Toleo hili lilichapishwa mwaka 2009. Miaka ya 1921 hadi 1926 Hemingway aliishi Paris, na kitabu kinaelezea mambo ya wakati ule, yakiwemo mahusiano yake na waandishi mashuhuri kama Gertrude Stein, ambaye alichangia sana kumkomaza kijana Hemingway katika uandishi. Bado ninakisoma, isipokuwa habari zake nimezifahamu kwa miaka kadhaa. Kitabu kingine ninachosoma ni Nomad  (New York: Free Press, 2011), kilichotungwa na Ayaan Hirsi Ali. Kinahusu maisha yake. Huyu ni mama aliyezaliwa Somalia, akalelewa katika u-Islam. Baadaye aliacha dini hiyo, kitendo ambacho kilisababi

Madreva Wetu Katika Kozi ya "Hemingway in East Africa, 2013"

Image
Katika safari zetu, wanafunzi wangu nami, nchini Tanzania, mwezi Januari mwaka 2013, tulitumia kampuni ya utalii ya Shidolya, yenye makao yake Arusha. Hapa naleta picha ya madereva wetu, kutoka kwenye kampuni hiyo. Tulisafiri salama kila mahali: Arusha, Longido, Mto wa Mbu, Karatu, Ngorongoro, Serengeti, Manyara, Babati, na Tarangire. Tulikuwa na bahati; hatukupata tatizo. Nimeona ni jambo jema kuwakumbuka madereva. Kwa bahati mbaya sina picha ya wapishi wetu, ambao nao walituhudumia vizuri kabisa.

Leo Nimeongea Tena na Mzee Patrick Hemingway

Image
Leo, saa kumi na dakika hamsini na mbili, nilimpigia simu Mzee Patrick Hemingway. Niliona tu nimpigie, baada ya kimya cha miezi mingi, wakati nilipozidiwa na homa. Sasa, kwa vile najisikia nafuu sana, niliamua kumpigia Mzee Hemingway. Nilimweleza kuwa nimekuwa kimya kwa muda mrefu kwa sababu ya kuugua, ila sasa hali yangu ni nafuu sana na inaendelea kuimarika. Tumeongea hadi saa kumi na mbili na robo. Baada ya kusalimiana tu, Mzee alinifahamisha kuwa yeye na ndugu yake Sean Hemingway wamechapisha toleo jipya la kitabu cha Hemingway, The Sun Also Rises. Nami hapo hapo nikamwambia kuwa nimempigia simu leo baada ya kusikiliza, jana, mahojiano baina ya mtangazaji wa redio na Sean Hemingway, kuhusu kuchapishwa kwa toleo hili Mada hii tumeiongelea kwa muda mrefu, tukijumlisha pia mawazo na maandishi mengine ya Hemingway, kama vile True at First Light na Under Kilimanjaro . Tuliongelea kuhusu wahakiki wa Hemingway na jinsi Hemingway alivyokuwa hawapendi. Mzee Hemingway aliniambia kuwa ku

Vitabu Nilivyonunua Leo

Image
Leo mchana, wakati binti yangu Deta ananirudisha kutoka hospitalini, tulisikia katika redio ya garini mahojiano na Sean Hemingway, mjukuu wa Ernest Hemingway. Mahojiano yalihusu toleo jipya la kitabu cha Ernest Hemingway, The Sun Also Rises . Ilikuwa ni mwanzo kwangu kusikia kuwa Sean amehariri  toleo jipya la kitabu cha The Sun Also Rises. Sikushangaa kusikia kuwa kampuni ya Scribner ndiyo imechapisha. Nimefahamu tangu zamani kuwa Scribner ni kampuni kongwe ambayo ilichapisha vitabu vya Hemingway tangu zamani. Niliposikiliza mahojiano hayo, niliamua hapo hapo kwenda kutafuta nakala ya hili toleo jipya. Tulipita kwenye duka la vitabu la chuo cha St. Olaf na nikaambiwa kuwa tayari wanacho kitabu hiki. Niliwaambia waniwekee, ili nije kununua. Wakati huo huo, niliamua kutafuta nakala ya toleo la mwanzo la The Sun Also Rises . Katika kusoma maandishi ya Hemingway, kwa miaka, nilifahamu kuwa The Sun Also Rises ni kitabu kilichompa Hemingway umaarufu miaka yake ya mwanzo kama mwandis

Karatu: Baada ya Darasa Kumalizika

Image
Hapa ni Karatu, Tanzania, mwezi Januari, mwaka 2013.  Ilikuwa mara tu baada ya kumaliza kipindi katika kozi yangu ya "Hemingway in East Africa." Hapa wanaonekana wanafunzi, mimi, na wenyeji watatu waliokuja kujumuika nasi. Sote tulifurahi kujumuika nao. Huyu bwana aliyeshika kitabu changu ni mwanasheria. Aliweza kuongea na baadhi ya wanafunzi, wakamweleza manufaa ya kitabu hiki kwao. Ninayo video inayowaonyesha wakiongea. Hao akina mama wawili, mmoja mwenye khanga na mwingine mwenye "jeans" ni mahakimu.

Hemingway: "True at First Light"

Image
Tulipomtembelea Mzee Patrick Hemingway, kule Montana , alituzawadia nakala za kitabu cha Ernest Hemingway, True at First Light . Tayari nilikuwa na nakala mbili hivi za kitabu hiki, na nilikuwa nimekisoma. Pia ni kitabu kimojawapo ambacho nilikitumia katika kozi yangu ya "Hemingway in East Africa." Hata hivi, zawadi hii kutoka kwa Mzee Patrick Hemingway ilinigusa sana. Jalada lake tu lilinivutia kwa namna ambayo siwezi kuelezea. Pili, ilikuwa ni bahati ya pekee kupata nakala kutoka kwa mhariri wa kitabu. Ernest Hemingway aliandika mswada mrefu sana kutokana na safari yake ya pili Afrika Mashariki. Alisafiri na kuishi kule miezi kadhaa, kuanzia mwaka 1953 hadi 1954. Hakuuchapisha mswada huu, bali aliuhifadhi Cuba, ambako aliishi miaka mingi. Alisema kuwa ni urithi kwa watoto wake. Miaka ya hivi karibuni, mswada huu ulitayarishwa na kuchapishwa kitabu, Under Kilimanjaro . Ni kitabu kikubwa sana, ila nilikuwa nimekisoma. Humo, Hemingway anaelezea vizuri hali ilivyokuwa mie

Naulizwa Kama Nafundisha ki-Swahili Hapa Marekani

Image
Mara kwa mara, ninapokutana na wa-Tanzania wasionifahamu vizuri, au wasionifahamu kabisa, wasikiapo kuwa nafundisha kwenye chuo fulani Marekani, wanauliza iwapo nafundisha ki-Swahili. Suali hili linaweza kuonekana kuwa rahisi, lakini kwangu ni suali tata. Kifupi ni kuwa mimi nafundisha katika idara ya ki-Ingereza ya Chuo cha St. Olaf , hapa Minnesota. Idara hii ilinialika kuja hapa kuanzisha kozi katika somo la "Post-Colonial Literature," na pia kufundisha uandishi wa ki-Ingereza. Nilichukuliwa, mwaka 1991, kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam , ambapo nilikuwa nafundisha katika idara ya "Literature." Hakuna kozi ya ki-Swahili katika chuo hiki cha St. Olaf . Mbali ya ki-Ingereza, lugha zinazofundishwa hapa ni ki-Jerumani, ki-Japani, ki-China, ki-Spaniola, ki-Norway, ki-Latini, na ki-Griki cha kale. Ninapotafakari suala la kufundisha ki-Swahili, najutia kwa nini sina ujuzi utakiwao, nikizingatia kuwa hii kwangu ni lugha karibu sawa na lugha mama. Nimeifahamu na

Mandhari ya Mto wa Mbu na Ziwa Manyara

Image
Mwezi Januari, 2013, katika mizunguko yangu Tanzania na wanafunzi wa Chuo cha St. Olaf , tukiwa tunafuatilia safari na maandishi ya Ernest Hemingway, niliamua tusimame kwenye mlima juu ya Mto wa Mbu, pembeni ya barabara iendayo Karatu. Mkisimama hapo, mnauona mji wa Mto wa Mbu kule bondeni, na kwa mbali kule mbele mnaliona ziwa la Manyara. Hata miaka iliyotangulia, wakati nasafiri na wanafunzi kutoka Chuo cha Colorado , tulifika mahali hapa. Mimi kama mwalimu naona ni muhimu kwa wanafunzi kufika sehemu hiyo na kuangalia sehemu hizi ambazo Hemingway alizielezea vizuri katika kitabu chake cha Green Hills of Africa . Inavutia kusoma maelezo ya Hemingway wakati mpo mahali hapa, anavyouelezea mji, mto unaopita hapo, duka la m-Hindu na uzuri wa Ziwa Manyara. Nina imani kuwa sina haja ya kueleza kuwa anayeonekana hapo kushoto ni mimi.

Ngorongoro

Image
Hapa ilikuwa ni mwezi Januari, 2013. Niko katika bonde la Ngorongoro, mmoja ya vivutio vikubwa vya utalii Tanzania. Nimebahatika kufika sehemu hiyo mara kadhaa. Kila wakati naguswa na uzuri na upekee wa mahali hapo. Mara ya kwanza kufika hapo nilikuwa kiongozi wa wanafunzi na wazazi wao kutoka shule ya Shady Hill, Boston. Nilikuwa nimeombwa na kampuni ya Thomson Safaris kuongoza msafara huu. Miaka iliyofuata nimefika hapo na wanafunzi kutoka vyuo vya Marekani vya Colorado na St. Olaf , tukiwa katika kozi ya "Hemingway in East Africa," ambayo niliitunga. Nimeandika makala kadhaa kuhusu kozi hiyo, na makala ya hivi karibuni kabisa ni hii hapa Kila wakati naguswa na uzuri na upekee wa mahali hapo. Kuna wanyama wa aina aina, kama vile samba, pundamilia, twiga, tembo, vifaru na nyati. Mara zote, tulitembelea pia hifadhi za Serengeti, Manyara, na Tarangire. Zote hizo ni utajiri mkubwa wa nchi yetu, kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.