Posts

Showing posts from January, 2009

Raha ya Kununua Vitabu

Image
Tangu nilipokuwa kijana mdogo, nilipenda kununua na kusoma vitabu. Niliwahi hata kununua vitabu ambavyo vilikuwa vigumu mno kwangu kuvielewa. Nakumbuka, kwa mfano, kitabu kimoja cha falsafa, kilichoandikwa kiIngereza, ambacho nilinunua ila nilipata taabu sana kukisoma. Pamoja na kuwa somo la kiIngereza nilikuwa nalipenda na kuliweza kuliko masomo yote, kitabu hiki kilinishinda kwa wakati ule wa ujana wangu. Lakini nilifurahi kuwa nacho katika maktaba yangu ndogo. Nilinunua pia vitabu vya kiSwahili. Kwa mfano, nakumbuka vizuri kitabu cha Shaaban Robert, Maisha Yangu . Vile vile, nakumbuka kitabu cha Yusuf Ulenge , Nguzo ya Maji na Hadithi Nyingine . Wakati ule, sikujua kabisa kuwa Yusuf Ulenge alikuwa mdogo wa Shaaban Robert. Hayo nimekuja kujua mwaka 2008, baada ya kununua na kusoma kitabu kiitwacho Barua za Shaaban Robert 1931-1958 , kilichochapishwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili , Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa mara ya kwanza mwaka 2002. Nimefurahi sana kufahamu kuwa Yusu

Chakula Bora

Niliwahi kuandika makala, Kuku kwa Mrija . Leo nimeona nilete makala juu ya vyakula anavyokula Rais Mpya wa Marekani, Barack Obama, makala ambayo inasisitiza umuhimu wa kuangalia tunakula nini, na inaonyesha kuwa kiongozi anaweza kutoa mfano kwa wananchi. Kama nilivyosema katika ile makala ya Kuku kwa Mrija, kuna tabia mbaya inayojengeka miongoni mwa Watanzania, ya kushabikia vyakula ambavyo au havina faida kiafya au vina madhara kiafya. Lakini kutokana na kasumba, watu wanaona wanajipatia hadhi ya juu kwa kutumia vyakula hivi. Makala ninayoleta hapa imeandikwa kwa kiIngereza, na ingawa blogu yangu hii inatumia kiSwahili, nimeona nivunje utaratibu huu kutokana na umuhimu wa suala la chakula. Ninategemea kuwa wale ambao hawajui kiIngereza labda wataweza kupata msaada wa kutafsiriwa makala hii. Watanzania na wengine wote tunaweza kujifunza mengi kutokana na makala hii inayomhusu Rais Obama. Soma hapa .

Waafrika Wanamwenzi Obama?

Kesho, tarehe 20 January, 2009, Barack Obama anaapishwa kama rais wa 44 wa Marekani. Dunia nzima iko katika heka heka za furaha na matumaini yasiyo kifani kutokana na ushindi wa Obama katika kampeni za urais wa Marekani. Waafrika nao wamejawa na furaha, na wanajivunia, wakizingatia kuwa baba yake Obama ni Mwafrika mwenzao, kutoka Kenya. Waafrika wanaamini kuwa Rais Obama atajenga uhusiano bora na Afrika, kwani Afrika ni kwake. Lakini je, Waafrika wanaomshangilia Obama wanamfahamu Obama au wanashangilia tu kwa vile kwa asili yake ni Mwafrika? Ukweli ni kuwa, Waafrika wengi hawana fikra wala mtazamo kama wa Obama kwa mambo mengi. Kwa mfano, Obama amekuwa mstari wa mbele kwa shughuli za kujitolea kwa ajili ya jamii yake na binadamu kwa ujumla, amekuwa mtetezi wa wanyonge, na ameonyesha mfano mzuri wa kujibidisha katika elimu na kuwa binadamu bora. Ajabu ni kuwa hata Waafrika ambao ni wazembe, wanaoendekeza rushwa na ufisadi, wasiothamini elimu, wasiothamini suala la kujitolea, wote wa

Watanzania na Mkutano wa Sullivan

Mwanzoni mwa mwezi Juni, 2008, mji wa Arusha ulipata fursa ya kuwakaribisha wageni wengi kwenye mkutano mkuu wa nane wa Sullivan . Nilikuwa katika mkoa wa Arusha pamoja na Wanafunzi kutoka Chuo cha Colorado, ambao nilikuwa nawafundisha kuhusu maandishi na safari za Ernest Hemingway maeneo hayo. Kwa hivi, sikupata fursa ya kuhudhuria mkutano wa Sullivan. Hata hivi, nilipata fursa tele ya kuongea na Watanzania kuhusu mkutano huo. Lengo la taasisi ya Sullivan ni kuchangia maendeleo ya Afrika, kwa kujenga uhusiano wa kibiashara, kijamii, na kadhalika baina ya Afrika na hasa Marekani na Ulaya. Mwanzilishi wa taasisi alikuwa Mmarekani Mweusi, Rev. Leon Sullivan, na kwa sababu hiyo, taasisi hii imekuwa na mvuto mkubwa miongoni mwa Wamarekani Weusi. Hao wanaikaribisha kwa mikono miwili fursa ya kuwekeza barani Afrika na kuungana na Waafrika katika kutekeleza ajenda ya maendeleo. Basi, kwenye mkutano wa Arusha, Wamerekani Weusi walikuja wengi sana, wakiwemo watu maarufu katika nyanja mbali

Matawi ya CCM Nje ya Nchi

Kwa miezi mingi sasa, kumekuwa na habari za kuanzishwa matawi ya CCM nje ya Tanzania. Naamini kila Mtanzania anaweza kuwa na maoni yake kuhusu jambo hili, na mimi ninayo pia, ingawa mimi ni Mtanzania ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Niliishi nje ya Tanzania kwa mara ya kwanza miaka ya 1980-86, nikiwa masomoni Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, Marekani. Nilipofika hapo, nilipokelewa vizuri na Watanzania waliokuwa wanasoma hapo. Walinipa kila msaada na ushauri niliohitaji ili kuzoea maisha yale mapya. Jumuia hii ya Watanzania, ingawa haikuwa kubwa, ilikuwa kama familia huku ugenini. Wakati wa shida na raha tulijumuika. Na mara kwa mara tulikuwa tunakutana kwa maongezi na kustarehe pamoja. Kama mtu alishindwa kuja kwenye mikutano hii, ilikuwa ni sababu ya labda kuzidiwa na shughuli au kuwa safarini. Lakini hatukuwa na mtu aliyekuwa hatakiwi au aliyejiona hatakiwi au hahusiki katika mikutano hiyo. Ningependelea Watanzania wanoishi nje waendeleze jadi hiyo. Mazingira ya

Mfano Bora wa Ujasiriamali

Neno ujasiriamali linasikika sana miongoni mwa Watanzania. Wengi wanajitahidi kuanzisha shughuli mbali mbali za kutoa huduma, kuuza bidhaa, na kadhalika, kama njia ya kujiongezea kipato na kujiendeleza kimaisha. Lakini, wengi hawana ufahamu wa siri ya mafanikio na maendeleo katika shughuli hizo. Kutokana na hilo, wengi wanashikilia imani za ushirikina. Matokeo yake katika jamii yetu yamekuwa mabaya sana, kama vile mauaji ya watu wengi. Hali hii inatisha. Kwamba watu wanaamini kuwa vitendo hivi vya kishirikina ndivyo vinaleta mafanikio ni ishara ya kukosekana elimu katika jamii yetu, ikiwemo elimu ya kuendesha miradi mbali mbali. Napenda kuleta taarifa kuhusu mjasiriamali mmoja ninayemfahamu, ambaye naamini anaonyesha mfano wa kuigwa na wajasiriamali wa Tanzania. Anaendesha mgahawa uitwao Tam Tam, katika mji wa Minneapolis, Minnesota. Ni mtu anayejibidiisha kufahamu biashara yake, wateja, na mambo mengine kadha wa kadha. Anajua kuwa elimu ni ufunguo wa mafanikio. Taarifa hizi zimeandi

Maongezi na Wanafunzi Wamarekani Waendao Tanzania

Image
Leo nilikwenda kwenye mji wa Apple Valley, Minnesota, kuongea na wanafunzi wa Chuo cha Gustavus Adolphus kilichoko St. Peter, Minnesota. Mkutano wetu tulifanyia katika ukumbi wa kanisa la Shepherd of the Valley . Maongezi yangu yalikuwa sehemu ya maandalizi ya wanafunzi hao kwa ajili ya safari ya kwenda Tanzania kwa masomo ya mwezi moja. Safari yao inawafikisha Iringa, katika Chuo Kikuu cha Tumaini , na vijiji vya Tungamalenga na Ilula . Nilikuwa nimeombwa na profesa wao nikaongee nao kuhusu masuala ya tofauti ya utamaduni wa Mwafrika na ule wa Mwamerika. Katika kujiandaa kuonana nami, wanafunzi hao walikuwa wameshasoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences , ambacho wanafunzi wa vyuo vingi hapa Marekani wanakitumia pia, katika kujiandaa kwenda Afrika. Baadhi ya wanafunzi hao wa Gustavus Adolphus wanasomea masuala ya afya. Nilitumia fursa ya leo kuwaeleza jinsi nilivyoingia katika shughuli ya kutafakari masuala ya tofauti baina ya utamaduni wa Mma

Kwa Kina na Prof. Joseph Mbele

Machi 28, 2008, yalitolewa mahojiano baina yangu na Bongo Celebrity . Kwa vile bado ninayo mawazo niliyotoa wakati ule, naona ni vema niyalete hapa pia, kama changamoto. Soma hapa