Sunday, September 19, 2021

Msomaji Amejipatia "Chickens in the Bus"

 

Jana, tarehe 18 Septemba, nilimpelekea msomaji anayeonekana nami pichani nakala ya kitabu changu kipya, Chickens in the Bus: More Thoughts on Cultural Differences. Huyu mama, kutoka Togo, amekuwa msomaji wangu wa tangu zamani. Anavyo vitabu vyangu vya awali: Matengo Folktales na Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Mara aliposikia nimechapisha kitabu kingine, aliagiza nakala. 

Nina bahati ya kuwa na wasomaji makini namna hii. Huyu mama ni msomi na mzoefu katika idara ya ustawi wa jamii. Ninategemea kupata mrejesho adimu kutoka kwake atakapomaliza kusoma kitabu hiki.  

Saturday, September 11, 2021

Nimehudhuria Selby Ave JazzFest

Leo nimehudhuria tamasha liitwalo Selby Ave JazzFest mjini St. Paul, Minnesota. Sikuwahi kuhudhuria tamasha hili linalofanyika kila mwaka. Nilishindwa kufuatilia. 

Kuhudhuria kwangu leo kumetokana na mkurugezi wa In Black In kunifahamisha kuhusu kuwepo kwa tamasha hili, kisha kunialika na kuniambia kuwa nitakaribishwa kwenye banda la In Black Ink. Ndivyo ilibyofanyika leo.

Nimefurahi kukutana na watu wa kila aina, wengine ambao nimewafahamu tangu wakati uliopita hadi wapya machoni pangu. Pichani ninaonekana nikiwa na watu wawili ambao walisema wanatoka California. Wanafurahi baada ya maonezi na baada ya kujipatia vitabu walivyoshika.
 

Sunday, September 5, 2021

Msomaji wa Kwanza wa Kitabu Changu Kipya

Jana, tarehe 4 Septemba, 2021, nilipata nakala za kitabu changu kipya Chickens in the Bus: More Thoughts on Cultural Differences. Hima nilimpa nakala jirani yangu, Mama Merri, mwalimu mstaafu anayependa sana kusoma maandishi yangu na ni mfuatiliaji wa shughuli zangu za kuelimisha waMarekani kuhusu utamaduni wa Afrika na tofauti zake na ule wa Marekani. 

Ni bahati njema kwa mwandishi kuwa na wasomaji na wafuatiliaji wa aina ya huyu mama. Lakini kwa hapa Marekani, bahati hiyo ninayo sana. Nina wasomaji na wafuatiliaji wengi.

Mama Merri alifundisha kwa miaka mingi katika shule za waHindi Wekundu. Alivyosoma kitabu changu Africans and Americans: Embracing Cultural Differences aliandika maelezo kuhusu namna utamaduni wao unavyofanana na ule wa waAfrika nilioelezea kitabu. Ninashukuru kwa elimu anayonipa.


 

Wednesday, September 1, 2021

Kitabu Changu Kipya: "Chickens in the Bus."

Jana, tarehe 31 Agosti, nilichapisha kitabu, Chickens in the Bus, kama kitabu halisi, baada ya kuwa nimekichapisha kama kitabu pepe siku kadhaa kabla. Nilipotangaza kuchapishwa hiki kitabu pepe, niliahidi kuwa kitabu halisi kiko njiani.

Kitabu hiki ni mwendelezo wa kitabu changu cha awali kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences ambacho kimejipatia umaarufu na kusomwa na maelfu ya watu tangu nilipokichapisha, mwezi Februari, mwaka 2005.

Wasomaji kadhaa wa hiki kitabu cha awali walikuwa wananiuliza iwapo nilikuwa nawazia kuandika kingine cha kuendeleza mawazo yaliyomo, nami nikawa na nawazia kufanya hivyo kwa miaka na miaka.

Sasa nimetekeleza kwa kuchapisha Chickens in the Bus. Mwenye kutaka kujua angalau kijujuu nini ninaongelea katika kitabu hiki, anawaza kunisikiliza katika video hii.
 

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...