Posts

Showing posts from November, 2010

Asante, Joseph Mbele

Jioni hii, katika kuzurura mtandaoni, mitaa ya Google, nimekumbana na makala kwenye blogu fulani, ambayo inanitaja. Soma hapa . Sikuwa nimeiona makala hii ambayo inataja ziara niliyofanya College of St. Benedict/St. John's University mwaka jana. Nilialikwa kutoa mihadhara. Katika darasa la Profesa Lisa Ohm, niliongelea hadithi na utamaduni, kufuatia maelezo yaliyomo katika kitabu cha Matengo Folktales , ambacho walikuwa wanakitumia. Soma hapa . Mhadhara wa pili niliutoa kwa wanafunzi na walimu waliokuwa wanajiandaa kwenda Tanzania na Afrika ya Kusini, lakini ulihudhuriwa na wengi wengine. Lengo lilikuwa kuwaarifu kuhusu tofauti za msingi baina ya tamaduni wa mw-Afrika na ule wa m-Marekani, kama nilivyoeleza katika kitabu cha Africans and Americans . Nakumbuka jinsi ukumbi ulivyojaa watu kwenye mhadhara huu, na kwenye meza nyuma ya umati walikuwa wameweka nakala nyingi za vitabu hivi viwili, kama ilivyo desturi hapa Marekani, wanapowaita waandishi kuzungumzia vitabu na uandishi.

Kuendesha Blogu Mbili

Nina blogu mbili: ya ki-Swahili na ya ki-Ingereza . Kuendesha blogu moja ni kazi, blogu mbili ni zaidi. Kwa nini naendesha blogu mbili? Nimewahi kuelezea kwa nini ninablogu . Labda nisisitize tu kuwa blogu yangu ya ki-Swahili inanipa fursa ya kujiongezea uzoefu wa kuandika kwa ki-Swahili, na pia kuwasiliana na wa-Tanzania wengi, wakiwemo wale wasiojua ki-Ingereza. Ninafahamu pia kuwa wako wasomaji wa blogu hii ambao si wa-Tanzania. Kuna hata wa-Marekani ambao wameniambia kuwa wanaisoma. Wanajikumbusha mambo ya Tanzania na pia lugha ya ki-Swahili. Katika blogu yangu ya ki-Ingereza siandiki sana masuala ya Tanzania. Kadiri siku zinavyozidi kwenda, napata hisia kuwa ninaandika kwa ajili ya walimwengu kwa ujumla. Naona jinsi ninavyozingatia masuala ya taaluma, hasa fasihi. Naamini natoa mchango kwa wale wapendao fasihi au wenye duku duku ya kuifahamu. Hapo nawafikiria sana wa-Tanzania. Katika kuongelea kazi za fasihi, siandiki makala ndefu, bali nagusia vipengele muhimu, na pia natoa

Kitendo cha CHADEMA Kususia Hotuba ya JK

Kitendo cha wabunge wa CHADEMA kususia hotuba ya JK Bungeni kimeibua mjadala mkubwa miongoni mwa wa-Tanzania. Wakati mjadala huu ukiendelea, nami nina la kusema. CHADEMA imesema kuwa, mapema kabisa, ilipeleka malalamiko kwenye tume ya uchaguzi (NEC) kuhusu mchakato wa utangazaji wa matokeo ya urais, na kuomba utangazaji ule usimamishwe ili kuchunguza dosari ambazo CHADEMA ilikuwa na taarifa nazo. Kwa msingi huu, ningependa kusikia taarifa ya NEC, niweze kufahamu kama kweli ililetewa malalamiko hayo. Kama iliyapata, napenda kujua iliyashughulikia vipi. CHADEMA inasema kuwa NEC haikuyajibu wala kuyashughulikia malalamiko yale. Kama hii ni kweli, basi naitupia NEC lawama nzito. CHADEMA imesema kwamba kutokana na kuupuziwa malalamiko yao na NEC, na kutokana na kwamba sheria inasema kuwa tangazo la NEC la mshindi wa urais haliwezi kupingwa mahakamani au penginepo, walilazimika kutafuta hatua zingine za kuelezea malalamiko yao. CHADEMA wanasema kuwa kususia hotuba ya JK ni njia waliyoamua

Kitabu Kilivyopokelewa Ubalozi wa Kenya

Image
Mwaka 2007 mwanzoni, jumuia ya wa-Kenya wanaoishi Minnesota waliandaa mkutano kuhusu uwekezaji nchini kwao. Walihudhuria wa-Kenya wengi sana, wakiwemo maofisa wa serikali na taasisi mbali mbali waliofika kutoka Nairobi. Nilishiriki, nikiwa na meza ambapo niliweka vitabu vyangu na machapisho mengine. Nilikutana na wa-Kenya wengi, baadhi ambao tulifahamiana kabla na wengine kwa mara ya kwanza. Mmoja wa hao tuliofahamiana kabla alikuwa Julia Opoti , ambaye ni mwanahabari anayeendelea kujipatia umaarufu, na ni shabiki wa siku nyingi wa maandishi yangu. Alikuja kwenye meza yangu akiwa na bwana mmoja, akatutambulisha. Yule bwana alikuwa afisa katika ubalozi wa Kenya, Washington DC. Julia alikuwa amemwambia kuhusu kitabu cha Africans and Americans naye akakinunua. Tarehe 17 Aprili, yule afisa aliniandikia ujumbe huu: Kuhusu kitabu chako, hivi sasa nafikiri kimesomwa na watu kadri ya watano hapa ubalozi wetu na kimependwa sana. Ni matumaini yangu kuwa ukipata wasaa mzuri utaandika vitabu

Wabunge wa CCM Wanakera

Wabunge wa CCM wanakera. Tukianzia na wabunge hao walioapishwa safari hii, sitasahau kuwa hao ndio waheshimiwa waliotoroka midahalo wakati wa kampeni. Wote walitoroka midahalo, kitendo ambacho kimenikera. Mimi kama mwalimu, ninayetambua umuhimu wa midahalo, ninawashutumu hao waheshimiwa. Soma hapa . Kila nitakapokuwa naona sura za hao waheshimiwa wa CCM, nitakuwa nakumbuka kitendo chao hiki cha kutoroka midahalo. Nitakuwa naangalia kama watajirekebisha au kama kitendo kile ni ishara ya tabia na mwenendo watakaofuata kwa miaka mitano ijayo. Tukirudi nyuma, kwenye awamu iliyopita, wabunge wa CCM walikera. Ni nani atakayesahau yaliyotokea wakati Dr. Slaa alipoanza kutamka kuwa kuna ufisadi katika nchi yetu? Wabunge wote wa CCM walimpinga vikali na kumtupia shutuma nzito kwamba alikuwa mzushi. Dr. Slaa hakuyumba, bali aliendelea kutoa madai yake. Hatimaye, ilianza kuthibitika kuwa aliyokuwa anayasema ni kweli, kwamba tuna mafisadi. Baada ya wananchi kuanza kuona ukweli huo, ukawa haupin

Kwa Nini Wabunge wa CHADEMA Wamesusia Hotuba ya JK

Leo, Novemba 18, katika ukurasa wake katika mtandao wa Facebook, Dr. Slaa ameelezea kwa nini wabunge wa CHADEMA wamesusia hotuba ya JK Bungeni. Mimi ni raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Nina ugomvi wangu na CCM, kama ninavyoeleza mara kwa mara katika blogu hii na blogu zingine, katika makala mbali mbali, na hata katika kitabu cha CHANGAMOTO . Papo hapo, ninaheshimu midahalo, na nimeshaishutumu CCM kwa kukimbia midahalo wakati wa kampeni zilizopita. Naweka hapa kauli hii ya Dr. Slaa kwa vile ninawaheshimu watu wanaojitokeza na kujieleza kwa hoja: ------------------------------------------------------------------------ Wabunge wetu wamechukua uamuzi mgumu sana, uamuzi ambao unataka ujasiri na uthubutu wa vitendo. Ni lazima tuelewe kuwa mgogoro uliopo siyo na Kikwete kama Kikwete, la hasha bali na mfumo uliomuingiza madarakani safari hii, mfumo ambao tunautuhumu kuwa haukuwa huru na wa haki. Uamuzi huu haukuwa wa chuki binafsi au kisirani dhidi ya Kikwete kama Kikw

Mzee Kataraia Amekipenda Kitabu Hiki

Image
Blogu yangu hii ni kama kisebule changu binafsi. Naamua nini cha kukiweka hapa, na sidhani kama ninasukumwa na ukweli kwamba watu wanasoma ninayoandika. Yeyote anayepita hapa na kuchungulia, ni hiari yake. Niliwahi kujieleza hivyo katika makala hii hapa . Basi, leo napenda kuelezea nilivyokutana na Mzee Kataraia juzi, tarehe 14, mjini Minneapolis. Hatukuwa tumefahamiana. Lakini mara tulipotambulishwa, alianza kunielezea jinsi alivyokipenda kitabu changu cha Africans and Americans . Niliguswa, nikamsikiliza kwa unyenyekevu. Ingawa napenda kuandika makala na vitabu, na watu wengi wananielezea wanavyopendezwa na kufaidika na maandishi yangu, napata taabu kustahimili sifa. Ila huwa namshukuru Mungu kwa kunipa vipaji, niendelee kutekeleza wajibu wa kuwanufaisha viumbe wake. Hii ndio tafsiri yangu. Sifa zote na shukrani namrudishia Muumba. Nikiwa namsikiliza, Mzee Kataraia aliendelea kunieleza jinsi alivyosafiri sehemu zingine hapa Marekani, akawaonyesha wa-Tanzania kadhaa kitabu hiki, na

Tumesoma Masimulizi ya "Popol Vuh"

Image
Leo katika darasa langu mojawapo tumemaliza kuongelea masimulizi ya kale ya Popol Vuh . Ni masimulizi ya zamani sana ya taifa la wa-Maya wa Amerika ya Kati. Wa-Maya wa zamani waliishi maeneo ambayo leo yanahusisha nchi za Mexico, Guatemala, Belize na Honduras. Walikuwa maarufu kwa mafanikio waliyofikia katika nyanja mbali mbali, kama vile ujenzi wa miji, ugunduzi wa hati ya kuandikia lugha yao, utafiti wa sayari, na utengenezaji wa kalenda. Nilisikia juu ya Popol Vuh kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 1982 kutoka kwa Profesa Harold Scheub, nilipokuwa nasomea shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu Cha Wisconsin-Madison . Hata hivi hatukusoma kitabu hiki. Sasa nimefurahi kuwa katika darasa langu tumefanikiwa kukisoma na kukijadili, ingawa mambo yake mengi si rahisi kueleweka kwetu watu wa leo, wa tamaduni tofauti kabisa na ule utamaduni wa wa-Maya wa zamani. Popol Vuh ni masimulizi kuhusu mambo mengi yahusuyo jinsi dunia ilivyoumbwa, na matukio mbali mbali yaliyofuatia, yakiwahusisha miung

Huduma ya Vitabu Gesti

Image
Tarehe 29 Oktoba nilikuwa Chicago, kuhudhuria mkutano wa washauri wa programu ya masomo iitwayo ACM Botswana . Vyuo vingi hapa Marekani vinaendesha programu za kupeleka wanafunzi nchi mbali mbali, nami ni mshauri katika programu kadhaa . Nilifikia katika hoteli ya Best Western River North . Nimeshalala hapo mara kadhaa, ninapohudhuria mikutano ya ACM Botswana na ACM Tanzania . Safari hii niliona hoteli hii imeanzisha huduma ya vitabu. Nilivyoingia chumbani, niliona tangazo kwenye meza ndogo ya taa, pembeni mwa kitanda. Nilipoliangalia karibu zaidi, niliona kuwa ni tangazo la huduma ya vitabu. Nilifuatilia. Nikateremka chini, kuelekea sehemu ya mapokezi. Wakati nashuka kwenye lifti, baada ya kufika chini kabisa, nikaona kuwa ukutani pana tangazo kuhusu huduma ya vyakula katika hoteli hii, na pia hii huduma ya vitabu, pamoja na uwepo wa hoteli hii katika mtandao wa Facebook, pia kuwa hoteli ina blogu yake. Hoteli imeanzisha huduma ya vitabu katika

Mdahalo wa Dr. Slaa, ITV, Utumike Mashuleni

Mimi ni mwalimu, mwenye uzoefu wa kufundisha tangu mwaka 1976, nilipoanza kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na hatimaye kutoa mihadhara katika vyuo vikuu sehemu mbali mbali duniani. Kutokana na wadhifa wangu, napenda kusema kuwa ingekuwa bora iwapo mdahalo wa Dr. Slaa ITV ungesambazwa mashuleni, kwani una mambo muhimu ya kuwafundisha vijana wetu. Jambo la kwanza ni kuwa mdahalo ule unatoa changamoto kuhusu masuala ya nchi yetu, ni kichocheo cha fikra. Jambo la pili ni kuwa vijana wetu wakiona jinsi Dr. Slaa anavyoyakabili masuali, kwa ufasaha, ufahamu, na kujiamini, wataona mfano wa kuiga na kigezo cha kujipima. Wataelewa kuwa wana wajibu wa kujielimisha sana. Wengi tunafahamu jinsi kiwango cha elimu kilivyoporomoka nchini, kiasi kwamba hata kwenye mahojiano ya kutafuta ajira, wa-Tanzania wanapata taabu. Kwa mfano, taarifa zimezagaa kuwa wa-Tanzania wanaogopa kushindana na wa-Kenya. Sisi miaka tulipokuwa tunasoma hatukuwa tunawaogopa wa-Kenya, wala wa-Ganda, wala wengine

Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM

Ingawa alikuwa mwanzilishi wa CCM, kwa nia njema ya kuendeleza mapinduzi katika nchi yetu, miaka ilivyozidi kwenda Mwalimu Nyerere alishuhudia jinsi CCM ilivyobadilika na kuwa mzigo kwake na pia tishio kwa usalama wa Taifa. Mwaka 1993 Mwalimu alichapisha kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (Harare: Zimbabwe Publishing House, 1993). Pamoja na mambo mengine katika kitabu hiki, Mwalimu alisema kuwa kuna kansa katika uongozi wa CCM. Nanukuu baadhi ya maneno yake: Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama cho chote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa Nchi yetu unataka yasemwe . (Ukurasa 61) Mwalimu hakuishia hapo, bali aliongezea namna hii: Nilisema awali kwamb