Picha Yangu Kwenye Jalada la Kitabu
Jana jioni nilivyokuwa ninachapisha kitabu changu kipya mtandaoni, nilijipiga picha kwa ajili ya kuiweka kwenye jalada la nyuma la kitabu. Nilikuwa nimetumia masaa yapata manne katika kuweka marekebisho ya ziada ya mswada na pia katika hatua za kwanza za kuuweka mswada mtandaoni. Picha niliyojipiga inaonyesha dalili za uchovu niliokuwa nao baada ya kufanya kazi ya kufikirisha. Sikujali. Niliamua kuitumia picha hiyo hiyo, nikamalizia shughuli ya kuchapisha kitabu. Tukijiuliza kwa nini tunaweka picha kwenye jalada la kitabu, tutakumbana na masuala na masuali. Suali pana zaidi ni kwa nini tunajipiga picha. Picha kama hii niliyojipiga jana itakaa kwenye jalada hivyo ilivyo, pamoja na kwamba inaleta taswira yangu ilivyokuwa kwa sekunde ile moja ilipopigwa. Baada ya sekunde ile moja, uso wangu haukubaki hivyo. Huenda nilitabasamu au kununa. Baada ya muda, sikuwepo humu ofisini, na vitabu nyuma yangu, wala sikuvaa nguo zinazoonekana pichani. Tunaweza kusema kuwa picha ni udanganyifu.