Saturday, March 26, 2016

Wasomaji Wangu: Akina Mama wa ki-Afrika, Marekani

Leo napenda kuendelea na jadi ya kuwakumbuka wasomaji wangu, kwa moyo wa shukrani. Kwa kuwa ninaandika katika magazeti, majarida, blogu zangu na za wengine, Facebook, na pia naandika vitabu, nina wasomaji wengi sehemu mbali mbali za dunia.

Hapa nimeamua kuwakumbuka wasomaji wa vitabu vyangu ambao ni wanawake wenye asili ya Afrika na nimefahamiana nao Marekani. Kwa kuwa nao ni wengi, na wengi siwafahamu, nitawataje wachache tu.


Huyu hapa ni Shannon, m-Marekani Mweusi anayeishi Minnesota. Ni profesa na mwandishi ambaye amekuwa akijijengea umaarufu. Kitabu chake cha kwanza, See No Color, kimewavutia wasomaji na wahakiki.

Shannon alikuwa mhakiki wa kwanza kuchapisha uhakiki wa kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Niliwahi kuandika habari zake katika blogu hii.





Huyu hapa ni Maimouna, mzaliwa wa Ivory Coast, anayeishi Minnesota. Yeye ni
mmoja wa wasomaji wa mwanzo kabisa wa Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nilifarijika sana aliponiambia kuwa amekipenda  kitabu hiki, na kwamba kitumiwe na wanafunzi wa ki-Marekani wanaokwenda Afrika. Kwa kuwa huyu mama na mume wake ambaye ni rafiki yangu ni wa-Islamu, kukipenda kwake kitabu changu kulinipa faraja ya pekee, kwani sikuwa na uhakika kuwa mambo ninayosema kitabu yameendana na maisha kama anavyoyafahamu yeye.







Huyu ni Latonya, m-Marekani Mweusi. Anaishi Minnesota. Tunakutana katika matamasha. Anapenda maandishi yangu, na aliwahi kunielezea hisia zake pale ninapoandika kwa ki-Swahili. Aliniuliza kwa nini ninawaweka kando ndugu zangu wa-Marekani Weusi. Nilijisikia vibaya, nikamwahidi kuwa nitajitahidi kuzingatia kauli yake.


Huyu ni Nalongue, mzaliwa wa Togo anayeishi Minnesota. Ni kati ya watu ambao wamekuwa wakifanya bidii sana kukitangaza kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Huyu ndiye ambaye niliwahi kumtaja katika blogu hii hapa, hapa na hapa.






Huyu hapa ni Rita, kutoka Sierra Leone. Anaishi Minnesota. Ni mwanzilishi na mkurugenzi wa jumuia ya wanawake iitwayo African Women Connect.

Baada ya yeye kusoma kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, tulikutana mjini Minneapolis tukakiongelea kwa karibu saa mbili. Alikuwa na hamu ya kuandika uhakiki wa kitabu hiki.


Huyu ni Leah, mzaliwa wa Kenya. Ni profesa, ambaye alipokuwa anafundisha katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Iowa, alikisoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, akaamua kukitumia alipowapeleka wanafunzi Rwanda na Tanzania mwaka 2008 katika safari ya masomo.







Huyu ni Eli, mzaliwa wa Togo. Anaishi Minnesota. Anavyo na amevisoma vitabu vyangu vya ki-Ingereza. Anaponikuta kwenye matamasha au mijumuiko mingine, anakuwa na dukuduku ya kujua kama nimeshaandika kitabu kingine.  Ninahamasika kwa moyo huu wa ufuatiliaji.





Huyu ni Julia, mzaliwa wa Kenya. Ni mwandishi katika magazeti hapa Minnesota anayejituma sana. Ni mmoja kati ya wasomaji wangu wa mwanzo, ambaye tangu mwanzo alijitosa katika kukitangaza kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Niliwahi kumtaja katika blogu hii, nilipoongelea juhudi za wa-Kenya katika masuala ya elimu na vitabu.


Huyu ni Nneka. Baba yake ni kutoka Nigeria na mama yake ni m-Marekani Mweusi. Nilifahamu jina lake kutokana na shughuli zake katika taasisi ya African Global Roots, inayoshughulika na utamaduni na elimu kwa waAfrika na wana-Diaspora wa ki-Afrika.

Wiki chache zilizopita nilikutana naye kwa mara ya kwanza, nikaelewa habari zake kama mtoto wa tamaduni mbili tofauti. Alipotambua kuwa ninashughulika na masuala hayo, aliniuliza masuali kadhaa. Baadaye nilimpelekea kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Baada ya siku chache aliniletea ujumbe akielezea jinsi alivyokipenda. Ninategemea kuendelea mawasiliano naye, angalau kumpa mwanga kuhusu masuala anayokabiliana nayo.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...