Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale. Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katika duka la vitabu la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kitabu hiki ni mkusanyo wa tenzi tatu za kale maarufu: Fumo Liyongo, uliotungwa na Muhamadi Kijumwa; Al Inkishafi, uliotungwa na Sayyid Abdalla bin Ali; na Mwanakupona, uliotungwa na Mwana Kupona binti Mshamu. Kitabu kimehaririwa na M.M. Mulokozi, profesa mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kilichapishwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili mwaka 1999.
Hizi ni kati ya tenzi maarufu kabisa katika ki-Swahili. Kwa msingi wa sanaa na maudhui, tenzi hizi zina hadhi kamili ya kuwemo katika orodha ambayo kwa ki-Ingereza huitwa "classics."
Fumo Liyongo ni hadithi inayomhusu shujaa Fumo Liongo, ambaye mimi, kutokana na utafiti wangu wa miaka mingi, napendelea kumwita Liongo Fumo. Huyu ni shujaa wa kale, labda miaka elfu moja iliyopita, na ndiye anayesifika kuliko wote tangu zamani katika jamii ya wa-Swahili.
Alikuwa pandikizi la mtu, mwenye vipaji kadhaa: kuwashinda maadui, shabaha katika kutumia upinde na mshale, ufundi wa kutunga nyimbo na mashairi. Juu ya yote, alikuwa muungwana sana, mfano wa kuigwa. Lakini alifanyiwa visa na ndugu yake ambaye alikuwa mfalme, hadi hatimaye akauawa na kijana mdogo, ambaye alikuwa mpwa wake.
Al Inkishafi ni utenzi wa tafakuri na falsafa kuhusu maisha, ambao umejikita katika kuuliza maana ya maisha ni nini. Mtunzi alilishughulikia suali hili kwa kuzingatia jinsi ustawi na utukufu wa wa-Swahili, hasa wa mji wa Pate, ulivyoanguka. Pate ulikuwa mji maarufu, wenye hadhi na mali, lakini kutokana na masaibu mbali mbali, ullipoteza hadhi hiyo na kuishia kuwa magofu.
Hii dhamira imeshughulikiwa tangu zamani na waandishi wengi wa pande za Arabuni, Uajemi, Ulaya na sehemu zingine duniani. Wanafalsafa pia wamehoji maana ya maisha, hasa wanafalsafa wa mkondo wa "existentialism."
Mwana Kupona ni utenzi uliotungwa na mama kumuusia binti yake kuhusu maisha ya ndoa, wajibu wake katika maisha hayo, na wajibu wake kwa watu kwa ujumla. Huu ni utenzi maarufu sana, ambao ni chimbuko la tungo za waandishi wengine, kama vile Shaaban Robert.
Mhariri amefanya kazi nzuri ya kuweka maelezo juu ya historia ya tenzi hizi, kuhusu watunzi, na kuhusu tafiti zilizofanywa juu ya tenzi hizi. Ametoa orodha ya maandishi ya wataalam mbali mbali, kumwezesha msomaji kufuatilia zaidi masuala hayo.
Kwa bahati nzuri, katika utafiti niliofanya kwa miaka mingi kuhusu tungo za kale za ki-Swahili, nimezitafiti tenzi hizi tatu, hasa Utenzi wa Fumo Liongo, ambao nimeutafiti kwa kina na kujipatia umaarufu kama mtafiti anayeongoza katika utafiti wa utenzi huu na masimulizi husika.
Watafiti bado wana majukumu makubwa ya kutafiti tenzi hizi na tenzi zingine. Kazi moja muhimu inayohitaji kufanyiwa bidii sana ni kuangalia miswada mbali mbali ya kila utenzi. Inahitajika juhudi na umakini kuangalia maneno yaliyotumika katika miswada hiyo, sentensi na lahaja, na kubaini tofauti zinazojitokeza.
Kuna tofauti za kila aina baina ya mswada na mswada, na ni juu ya watafiti kuzitambua na kuzitolea maelezo. Miswada ya tenzi zote za zamani za ki-Swahili inatofautiana katika vipengele mbali mbali.
Jukumu jingine ni kuzunguka katika maeneo ya wa-Swahili, kama vile mwambao wa Kenya, ambako nilifanya utafiti miaka ya 1989 hadi 1991. Huko nilikutana na mabingwa wa lugha na tungo za ki-Swahili, kama vile Mzee Ahmed Sheikh Nabhani wa Mombasa, na wazee wengine wa miji kama Witu na Lamu. Ni muhimu watafiti waende Pate, Siu, na kadhalika. Pia tunahitaji kufanya utafiti zaidi katika hifadhi za miswada ya ki-Swahili iliyopo katika maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha London, Berlin, na sehemu zingine.
Tenzi Tatu za Kale ni hazina kubwa kwa wasomaji wa kawaida, watafiti, na wanafunzi, hadi kiwango cha chuo kikuu. Kwa bahati nzuri kitabu hiki kinapatikana kirahisi Tanzania. Ninakipendekeza kwa yeyote anayetaka kujiongezea ufahamu wa lugha na fasihi ya ki-Swahili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
30 comments:
Asante kwa kazi nzuri tunaomba utuchambulie kwa Muhtasari maudhui yaliyomo katika Utendi wa FUMO LIYONGO
Ndugu David Kalonga, shukrani kwa mchango wako.
Nadharia za fasihi tulizofundishwa Tanzania miaka niliyosoma Chuo Kikuu Dar, kuanzia 1973, nami nikawa nazifundisha pale pale, kuanzia mwaka 1976, zilikuwa katika mkondo huu wa kuongelea fani na maudhui.
Nadharia zimebadilika na zinaendelea kubadilika. Hayo niliyafahamu vizuri wakati nasomea shahada ya uzamifu huku ughaibuni, Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, 1980-86.
Mtazamo huu mpya ndio niliokuja nao Chuo Kikuu Dar ule mwaka 1986, kuendelea na kazi yangu.
Kuhusu suala la muhtasari, hatari zake zimeelezwa vizuri katika makala mbali mbali, kama vile makala ya Cleanth Brooks iitwayo "The Heresy of Paraphrase."
Hakuna kazi ya sanaa ambayo imefungiwa maudhui ndani yake kama tunavyofungia bidhaa katika kifurushi.
Maudhui huzaliwa pale msomaji au msikilizaji anaposikiliza au kusoma. Hutofautiana kutokana na usomaji, msomaji, jamii hadi jamii. Jamii zenye itikadi tofauti au wasomaji wenye itikadi tofauti watasoma utendi na kuibuka na maudhui tofauti.
Kuna nadharia zingine za fasihi ambazo zinahoji uwezekano wa kazi ya fasihi kuwa na maudhui, uwezekano wa lugha kubeba ujumbe.
Nimeandika na kuchapisha makala kadhaa kuhusu utendi wa Liyongo, katika majarida kama "Kiswahili," "The Literary Griot," na "Research in African Literatures."
Ni bora kusoma makala hizo, ambazo hazimalizi suala, kwa maana kwamba hazihitimishi mjadala, bali ni hatua katika mchakato ambao bado unaendelea.
Bado ninautafakari utenzi huu, na ninaendelea kuuandikia makala. Nikileta muhtasari nitapotosha ukweli huo.
Shukran Bwana Ustadh.Kwa kweli uchambuzi wako umeniingilia sana na nimejikuta katika ile hali ya kutaka kujua zaidi kuzihusu tenzi hizi kwa sababu zina manufaa kwetu hasa katika jamii ya kisasa.Ustadh swali ninalo ni kuwa kwa unyenyekevu wangu wote nakuomba unielezee kupitia Tenzi Tatu za Kale kuhusu sura mbalimbali za kimuundo wa shairi wakati wa urasimi wa shairi
Ndugu Robert Ouko,
Shukrani kwa ujumbe wako. Masuala ya muundo wa shairi "wakati wa urasimi wa shairi," au wakati mwingine wowote ni nje ya ufahamu wangu. Utafiti na uandishi wangu umezingatia masuala mengine, kama vile dhana ya ushujaa na taswira ya mwanamke katika tungo hizo. Kuhusu masuala ya kimuundo, napendekeza usome kitabu cha Ibrahim Noor Shariff, "Tungo Zetu: Msingi wa Mashairi na Tungo Nyinginezo." Pia kuna makala kadhaa za ki-Ingereza kuhusu "Swahili prosody."
Asante sana kwa kazi yako nzuri. Naomba utusaidie kuonyesha jinsi mwanaume anavyodhalilishwa katika utenzi wa mwanakupona.
Ndugu Anonymous uliyeandika December 11, 2015 at 3:37 AM, shukrani kwa ulizo lako. Napenda niliweke suali lako katika nadharia ya fasihi. Kazi ya fasihi ikishaandikwa na kuwafikia wasomaji, inakuwa na tabia ya kuleta tafsiri mbali mbali kwa kila msomaji, na pengine kwa kila jamii. Inategemea uwezo na uzoefu wa msomaji katika kusoma fasihi, akili, imani na itikadi ya msomaji, utamaduni wa jamii, na kadhalika.
Kwa maana hiyo, utenzi wa Mwana Kupona unaweza kueleweka kwa namna mbali mbali na watu au jamii mbali mbali, katika tamaduni mbali mbali, na katika vipindi mbali mbali vya historia. Unaweza kueleweka namna tofauti kwa mwanamme na mwanamke, muumini wa dini na asiye muumini wa dini, mwanaharakati wa masuala ya jinsia kama vile "feminist," na kadhalika.
Kwa kuzingatia yote hayo, suali lako ni tata, huenda haliwezi kujibika kwa jibu moja, na huenda halijibiki kabisa. Lakini huu ndio utamu wa somo la fasihi. Linatupa fursa ya kuzama katika tafakari, kuchemsha bongo, na hata kuchanganyikiwa. Kuchanganyikiwa ni matokeo ya kufikiri kwa dhati, na ni jambo jema kuliko kukaa tukiwa tumeridhika kwamba masuala ni wazi na rahisi, na kwamba majibu tunayo.
Naomba msaada wa mambo muhimu katika kuhakiki utenzi huu wa mwana kupona
Ndugu Junaynat Dama
Shukrani kwa ulizo lako. Kama nilivyojaribu kuelezea masuali niliyoulizwa hapa juu, ninasita kutoa majibu ya kujenga hisia kuwa ndio majibu sahihi. Taaluma hii ya fasihi ninaiona ina changamoto nyingi na utata mwingi.
Kutokana na mtazamo wangu huu, hata nikiulizwa kutaja mambo muhimu katika utungo kama huu wa Mwana Kupona, sielewi namna ya kujibu. Nimesoma nadharia nyingi, na zingine zinadai kwamba hatuna vigezo vinavyokubalika na kila mtu vya kuamulia nini ni muhimu na nini si muhimu katika kazi ya fasihi.
Tafadhali vuka mipaka tuliyoizoea katika kuiangalia na kuijadili fasihi. Tumekuwa na jadi ya kurahisisha mambo na kujiaminisha kuwa kuna majibu ya uhakika ya masuali yetu, au kuna wenye majibu sahihi.
Sikatai kuwa tukiulizwa tumtaje aliyetunga kitabu cha "Kusadikika," tunalo jibu kwamba ni Shaaban Robert. Lakini tukiulizwa tutaje na kujadili mambo muhimu katika "Kusadikika," ndipo ninaposema ni pagumu sana.
Kila anayesoma maongezi hayo nadhani anaweza kujionea ninasimama wapi. Ninahisi wako wasomi wa taaluma ya fasihi ambao wanafuatilia mjadala huu. Ingekuwa bora iwapo wangetuletea mchango wao.
Habari na hongera kwa shughuli nzuri umefanya. Napenda kufahamishwa kua nikiasi gani matumizi ya lugha,lahaja na misamiati katika tenzi tatu zakale zinatofautiana na hizi tenzi zakileo
Ndugu Azizi Salim
Shukrani kwa suali lako. Nilitegemea kuwa wengine wangejitokeza na kusema chochote, kwani mimi sijafanya utafiti wowote kuhusu mada unazoongelea, yaani lugha, lahaja na msamiati katika tenzi. Hata hivi, napenda niseme mambo mawili matatu kuhusu suali lako.
Ninavyoona, suali lako ni pana mno. Halijibiki kwa namna ya kuridhisha, labda liandikiwe kitabu au vitabu baada ya utafiti wa kina. Masuali ni mengi. Kwa mfano, unapambanua baina ya tenzi tatu za kale na tenzi za leo. Je, unamaanisha kuwa lugha, lahaja na misamiati ni ile ile katika hizi tenzi tatu za kale? Tunaweza kuhisi kuwa kwa kuwa tenzi za Mwana Kupona na Liyongo zilitungwa na watunzi wa Lamu, labda lahaja iliyotumika ni ki-Amu. Lakini kinachohitajika ni uthitibisho, ambao unahitaji uchambuzi wa kina wa lahaja katika tenzi hizi mbili.
Halafu, kuhusu hizi tenzi tatu za kale, tukizingatia kuwa mambo yanayoongelewa katika kila utenzi ni tofauti na yale ya tenzi zingine mbili, haiwezekani misamiati isitofautiane. Lakini je, utahesabu maneno yote yaliyomo katika kila utenzi na kisha kulinganisha misamiati? Labda kwa kuwa siku hizi tunazo kompyuta tunaweza kuhesabu maneno yote na kulinganisha. Lakini, kama nilivyogusia, kutofautiana kwa mambo yanayozungumziwa katika tenzi hizi lazima kunasababisha misamiati kutofautiana.
Katika suali lako, unaongelea pia tenzi za kileo. Hii nayo ni dhana pana mno, kwani tenzi za kileo ni nyingi, na zimetungwa na watu wengi, kama vile Salim A. Kibao, Zuberi Hamadi Leso, Jumanne M. Mayoka, George Mhina, Ramadhani Mwaruka, Haji Gora Haji, Mohammed Saif Khatib, na Henry Muhanika. Sasa mtu ataanzia wapi na ataishia wapi katika kujibu suali lako?
Binafsi, napendekeza mtu ajipe jukumu la kutafiti mada finyu iwezekanavyo, si pana kama hii uliyoileta. Ninamaanisha nini? Kwa mfano, mtu atafiti miswada ya utenzi mmoja, kama vile "Utenzi wa Mwana Kupona" au "Utenzi wa Ras il Ghuli." Ninazingatia ukweli kwamba ingawa kimechapishwa kitabu cha "Utenzi wa Mwana Kupona," kuna haja ya kuichunguza miswada ya utenzi huo, si kuridhika tu na kitabu kilichopo.
Vile vile utenzi kama huu wa "Ras il Ghuli." Si vizuri tuendelee kuridhika na kitabu kilichopo, kilichohaririwa kwa umakini sana na Padri Leo van Kessel. Tunapaswa kuwa na moyo wa kiutafiti wa kuichunguza miswada mingine ya utenzi huu, au vipande vya miswada hiyo, na kulinganisha na kitabu kilichopo.
Nikirejea kwenye suala la tenzi tatu za kale, napenda niseme, kama mfano, kwamba utenzi wa Liyongo tunaousoma, ulitungwa na Muhammad Kijumwa kwenye mwaka 1913. Alitunga utungo wake huo kutokana na nyimbo na masimulizi yaliyorithiwa tangu zamani katika jamii ya wa-Swahili. Huu, kwa hakika, ndio ukale wa utenzi wa Liyongo. Tukizingatia kuwa mwaka wa 1913 kama mwaka ulipotungwa utenzi huu, dhana ya ukale wake inaweza kuwa na utata.
Kama nilivyotamka hapo juu, mimi sijafanya utafiti wowote wa lugha, lahaja, na misamiati katika tenzi za kale, wala za leo. Utafiti wangu umekuwa katika masuala mengine ya tenzi za kale. Ila nimeona nitoe duku duku zangu, angalau kifupi.
Asante sana bwana kwa ufafanuzi wako kwenye Mada tofauti, je unaweza kunipa barua pepe yako kwa kuniunga :mwalimu. Shafi@yahoo.com
Ndugu Mwalimu Shafi
Shukrani kwa kutembelea hapa na kuacha ujumbe. Anwani yangu moja ni josephmbele@yahoo.com na nyingine ni africonexion@gmail.com
Ninaona jinsi wasomaji wanavyofurika kwenye mada hii ya Tenzi Tatu za Kale. Hakuna mada yoyote katika blogu hii inayotembelewa zaidi ya hii. Ni faraja kwangu kuona kuwa nilichoandika kinawavuta watu kiasi hiki.
Ninapenda kusema kuwa hiki nilichoandika hapa ni chembe ndogo sana ya uandishi wangu na ni mfano mdogo sana wa namna ninavyoandika. Ili kupata ufahamu mpana zaidi, ni bora msomaji asome machapisho yangu mengine, kama yaliyoorodheshwa katika tovuti hii.
mimi NAKUpongeza mwalimu umejaribu kutufumbua macho juu ya urithi huu adhimu katika lugha ya kiswahili nami nanena
jack nalimwaga chozi,kaburini mwa mwalimu
yule NYERERE Mjuzi,nampatia salamu
daima tutamuenzi,alifanya la muhimu
kukifanya kiswahili kuwa lugha yetu mama.
MIMI ni jackson thomasy mwanafunzi wa BAED\kisw/hist
amucta
Ndugu Jackson Thomasy,
Shukrani kwa ujumbe wako, na utungo. Nashukuru kwamba kujaribu kwangu kuiongelea mada hii ya fasihi kumekuwa na manufaa. Tuendelee kutafuta elimu, kwani haina mwenyewe, wala haina mwisho. Nakutakia kila la heri.
Ingekuwa bora ungechanganua baadhi ya maidhui yayojitokeza katika tenzi hizi...
Maudhui ya utenzi wa AL-Inkishafi in yapi
Ndugu anonymous uliyeandika tarehe 24 November, 2016 at 12:06 AM na ndugu purity murathi, naomba mfuatilie kwa makini maelezo niliyotoa katika majibu yangu hapa juu. Kazi ya kuchambua fasihi haina majibu ya mkato. Ni tofauti na mafundisho ya dini kanisani au msikitini, ambako padri au mchungaji, au imam wanajibu masuali. Fasihi inatutaka tutafakari sisi wenyewe, kila mtu na upeo wake, na majibu hutofautiana na huenda yakabadilika kutokana na kukua kwa fikra na elimu ya kila msomaji. Siwezi kuwa kama padri, mchungaji, au imam. Itakuwa siitendei haki taaluma ya fasihi.
Ninaweza kuelezea maudhui, lakini haitakuwa ndio ukweli wa mambo, kama msahafu. Itakuwa ni mtazamo tu, katika mazingira yangu na ufahamu wangu wa sasa, na ninaweza kubadili mtazamo wakati wowote.
Hongera sn ndg kwa kaz mzr, lkn ingependeza sn km ukatuwekea makala inayochambua utendi huu wa liongo fumo km unavomuita mwnywe,naomb kuwasilisha.
Kazi hii yaridhisha
Swali langu ni,vielelezo vya kigeni vina athari gani katika ushairi wa kiswahili
Shukran. Naomba unielezee jinsi waandishi hawa wa zamani walvyojikita kwenye
1.dini
2.utawala
3Utamaduni
4.Biashara
Katika kutunga kazi zao
ukurasa huu ume jibu maswali yangu mengi sababu mimi ni mshairi nae chipukia
Ndugu Albert John Solyambingu, kama umevutiwa na mawazo yangu, bila shaka utafaidika zaidi ukisoma vitabu vyangu ambamo ninajieleza kwa ufasaha zaidi nikijumlisha masuala ya fasihi na utamaduni. Vitabu hivyo vinapatikana mtandaoni, kama unavyoona pembeni mwa ukurasa huu wa blogu yangu, lakini vile vile vinapatikana katika duka la Kimahama lililoko Arusha na duka liitwalo A Novel Idea, liliko eneo la Slipway kule Msasani, Dar es Salaam.
Shukrani za dhati gwiji kwa ufafanuzi wako wa kina. Ulizo langu ni aliloandika mwandishi wa Al-Inkishafi unaashiria vipi maisha yetu ya kisasa na ya siku zijazo kama jamii?
Hongera kwa kazi yako nzuri ningeomba unielezee maudhui mbalimbali yanayojitokeza katika utenzi wa fumo liyongo
Kazi kuntu hongera
Ahsante kwa kazi nzuri , Naomba kujua kipengele cha wahusika katika utenzi wa Al-inkishafi
prof. asante sana kwa mawazo yako yanayojenga. nimesoma na nimepat vitu vizuri sana na vinavyotujenga kama wasomaji, wahakiki na watafiti wa kazi za fasihi. Ubarikiwe
stella Fautine, ukumbi huu ungekuwa ni wa kitaaluma hasa, ningeandika mengi zaidi na kwa uangalifu zaidi. Hata hivi, najaribu kuwaonjesha wasomaji na kuwavutia kwenye uwanja wa fasihi.
Naomba ufafanuzi wa sifa za kimtindo na maudhui yanayojitokeza katika Utenzi wa Al-inkishafi.
Post a Comment