Sunday, September 25, 2022

Mkutano na Mmiliki wa African Travel Seminars

Tarehe 22 Septemba, nilikutana na Georgina Martin Lorencz, mmiliki wa African Travel Seminars, kampuni ya utalii inayopeleka watu sehemu mbali mbali duniani. Huyu mama mwenye asili ya Ghana tunafanana kimtazamo kuhusu utalii. Tunataka utalii unaolinda heshima na utu, unaoboresha maelewano, na usio na hali yoyote ya udhalilishaji na ukoloni mamboleo. Tunataka manufaa ya utalii yaonekane katika jamii inayofikiwa na watalii.

Zaidi ya hayo, Georgina  ni kati ya wale wanaotumia kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences katika shughuli zao. Kuafiki kwao yale ninayosema kuhusu utamaduni wa waAfrika kunsnifanya nijisikie vizuri. Hiyo juzi nilimkabidhi kitabu changu kipya, Chickens in the Bus: More Thoughts on Cultural Differences.

Kuna mambo muhimu tumepangia kufanya, ikiwemo kufungua njia mpya za utalii Tanzania, kuongezea programu iliyopo Tanzania ya African Travel Seminars. Taarifa zitapatikana kadiri muda unavyokwenda. 

Sunday, September 18, 2022

Tanga Watafakari Changamoto za Tofauti za Tamaduni


Tarehe 11 Juni, 2022, nilikuwa mgeni rasmi katika mkutano wa kwanza wa kikundi cha watu wa mataifa mbali mbali kilichoanzishwa Tanga kwa lengo la kutafakari na kuchambua changamoto za tofauti za tamaduni. Kikundi kinajulikana kama Cross Cultural Dialogue.

Mratibu wa kikundi, Georgina, alikuwa amesoma kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, wakati niko bado Marekani, akaamua kunialika kuongea nao.

Safari yangu kutoka Marekani nilitua Nairobi, nikapitiliza hadi Mombasa. Kutokea Mombasa, nilishuka Tanga. Nilipumzika siku moja nikisubiri mkutano. Mkutano tulifanyia Hashtag Cafe, na ulifana sana. Wadau walifurahia kunisikiliza, tukabadilishana uzoefu na mitazamo. Nilikuwa nimeleta nakala za vitabu vyangu: Matengo FolktalesAfricans and Americans: Embracing Cultural Differences, na Chickens in the Bus: More Thoughts on Cultural Differences. Wadau walivinunua.

Kuanzishwa kwa Cross Cultural Dialogue ni jambo muhimu sana. Dunia inavyozidi kuwa kijiji, watu wa tamaduni mbali mbali, tupende tusipende, tunajikuta katika mahusiano ya kila aina ambayo huja na changamoto nyingi, ndogo na kubwa, kwa sababu ya tofauti za tamaduni. Tofauti hizi zinaweza kukwamisha au kuharibu mahusiano, iwe ni ya binafsi, biashara, diplomasia, na kadhalika.

Cross Cultural Dialogue wameendelea kukua. Nafurahi wanavyotumia vitabu vyangu kama dira na kichocheo cha tafakari. Mwamko wa aina ya Cross Cultural Dialogue unaleta matumaini kwa hatima ya Tanzania, katika ulimwengu wa leo wa ushindani mkubwa. Kwa wanaopenda, vitabu vinapatikana kwenye dula la A Novel Idea lililoko Slipway, Msasani, na pia katika TFA Center iliyopo Barabara ya Sokoine, Arusha.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...