Posts

Showing posts from March, 2015

Chama cha Kijamaa na Uzalendo Tanzania (C.K.U.T.)

Image
Nimeona leo katika mtandao wa Facebook kuwa kuna chama kipya cha siasa ambacho kinawania usajili. Kinaitwa Chama cha Kijamaa na Uzalendo Tanzania (C.K.U.T.). Kama ni chama cha Kijamaa, kitanifurahisha, tofauti na CCM, chama ambacho kinahujumu ujamaa na mapinduzi kwa ujumla, kama yalivyoelezwa katika "Azimio la Arusha," "Mwongozo," na maandishi mengine. Kuanzisha chama au kujumuika na wengine katika chama kwa misingi ya amani ni moja ya haki za binadamu. Na mimi nina haki ya kuwa nilivyo, raia ambaye si mwanachama wa chama cho chote cha siasa, haki ambayo inahujumiwa na katiba ya Tanzania iliyopo kwa kuwa inaniwekea vikwazo nikitaka kugombea uongozi katika siasa. Pamoja na yote, ninapenda tu kusisitiza kuwa vyama vya siasa vijitegemee. Tutengue sheria ya kuvipa ruzuku, kama nilivyoandika katika blogu hii.

Vyama vya Siasa Vijitegemee

Image
Ninaandika ujumbe huu kwa wa-Tanzania wenzangu. Ninatoa hoja kuwa vyama vya siasa vijitegemee. Tuachane na utaratibu wa sasa wa serikali kuvipa ruzuku vyama vya siasa. Nimeweka picha yangu hapa kuthibitisha kuwa ninayeandika ujumbe huu ni mimi, si "anonymous." Fedha inayotolewa na serikali kama ruzuku kwa vyama vya siasa ni kodi ya walipa kodi wote, na wengi wao si wanachama wa chama cho chote cha siasa. Ruzuku hii ni hujuma dhidi ya hao walipa kodi ambao si wanachama wa chama cho chote cha siasa. Ni hujuma, ingawa imehalalishwa kisheria. Sheria na haki si kitu kile kile. Ukaburu ulikuwa halali kisheria, lakini ulikuwa ni hujuma dhidi ya haki. Fedha inayotolewa kwa vyama hivi ni nyingi sana, mamilioni mengi ya shilingi kila mwezi. Ni fedha ambazo zingeweza kununulia madawati na vitabu mashuleni, kulipia mishahara ya walimu au madaktari, kukarabati barabara, kuwanunulia baiskeli walemavu wanaotambaa chini, kujenga maghala ya kuhifadhia mahindi ambayo yanaoza katika mikoa k

Picha Nilizopigwa Katika Studio ya Afric Tempo, Machi 21

Image
Tarehe 21 Machi, nilifanyiwa mahojiano na Ndugu Petros Haile Beyene, mkurugenzi wa African Global Roots, katika studio ya Afric Tempo mjini Minneapolis. Aliomba tufanye mahojiano kuhusu kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences ambacho alikuwa amekisoma na kukipenda. Niliandika taarifa ya mahojiano hayo katika blogu hii. Hapa naleta picha mbili alizopiga Ndugu Malick, mmiliki wa studio, aliyerekodi kipindi kwa ajili ya televisheni. Amenitumia leo hii. Hapa kushoto anaonekana Ndugu Petros Haile akiwa nami, tayari kwa mahojiano, ambayo watakaoyaona katika televisheni watayafurahia. Kama wasemavyo mitaani, kaeni mkao wa kula. Nimeona niweke picha hizi hapa, nikizingatia kuwa wako ambao wangependa kuona sura yangu ilivyo kwa sasa, baada ya muda mrefu wa kuumwa. Ninaendelea kupona vizuri, ingawa pole pole. Hata safari kama hizi za Minneapolis, umbali wa maili 45, ninaendesha gari mwenyewe. Na majukumu yangu niliyozoea, kama vile kutoa mihadhara na kufu

Mwandishi Grace Ogot Amefariki

Image
Wikiendi hii, habari zimetapakaa kuwa mwandishi Grace Ogot wa Kenya amefariki. Habari hizi zimenishtua na zimenikumbusha mengi kuhusiana na mwandishi huyu. Nilipokuwa kijana, miaka ya sitini na kitu, ndipo nilianza kusikia habari zake. Nilikuwa nasoma masomo ya sekondari katika seminari ya Likonde. Shule ilikuwa na maktaba nzuri sana, chini ya usimamizi wa Padri Lambert, OSB, ambaye alikuwa mwalimu wetu wa ki-Ingereza na historia. Nilikuwa msomaji makini wa vitabu, na nilikuwa nafuatilia kwa karibu uandishi katika Afrika Mashariki, Afrika, na sehemu zingine za dunia. Ndipo nilipoanza kuyafahamu maandishi ya Grace Ogot. Riwaya yake, The Promised Land, ilikuwa na maana sana katika ujana wangu, kwani ilichangia kunifanya niipende zaidi fasihi. Hadithi fupi ya "The Rain Came" ilinigusa kwa namna ya pekee. Miaka ya mwishoni mwa sabini na kitu, wakati nafundisha katika Idara ya "Literature" ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nakumbuka nilifundisha kitabu cha Gikuyu F

Siendi Mahali Kuuza Vitabu

Image
Mimi ni mwalimu, mwelimishaji, darasani na katika jamii. Ili kufanikisha majukumu yangu, ni mtafutaji wa elimu bila kuchoka. Ni mwanafunzi muda wote ili kujiimarisha katika ualimu na uelimishaji. Nafundisha na kujufunza kwa kuongea na watu ana kwa ana, iwe ni darasani au nje ya darasa. Nafundisha na kujifunza kwa mawasiliano ya masafa marefu, iwe kwa barua pepe au kwa simu. Hivi karibuni, nimeanza pia kutumia Skpe. Hizi zote ni njia za kuelimisha sambamba na kujielimisha. Lakini vile vile, mimi ni mwandishi wa makala na vitabu. Kwa kawaida uandishi wa nakala huchukua muda mwingi, na vitabu ndio zaidi, kwani kitabu kinaweza kuchukua miaka kukiandaa na kukiandika. Kwa ujumla unaandika katika upweke. Nakubaliana na kauli ya Ernest Hemingway, "Writing, at its best, is a lonely life." Kwangu mimi kama mwalimu naona uandishi wa aina ya vitabu ninavyoandika kuwa ni mwendelezo wa ufundishaji. Ninapokwenda na vitabu vyangu kwenye tamasha au maonesho, ninakwenda kama mwalimu.

Leo Nimehojiwa na "African Global Roots"

Image
Nimerejea mchana huu kutoka Minneapolis, kwenye mahojiano na African Global Roots (AGR). Wiki mbili hivi zilizopita, Ndugu Petros Haile, mkurugenzi wa AGR alikuwa ameniomba tufanye mahojiano hayo. Ndugu Haile nami tumefahamiana kwa miaka kadhaa. Nimewahi kushiriki katika program zake kwa kupeleka vitabu vyangu. Vile vile, alivyovyofahamu kuwa nimepeleka wanafunzi Tanzania kwenye kozi ya Hemingway, aliniomba niandike makala, ambayo aliichapisha. Kwa mahojiano ya leo, Ndugu Haile alitaka tuongelee kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences , ambacho alishakisoma miaka iliyopita. Alitamani, kwa kutumia mawasiliano ya AGR kusambaza ujumbe katika jamii ya wa-Afrika hapa Marekani na ulimwenguni na kwa watu wengine, kuhusu umuhimu wa kuyaelewa masuala ninayoongelea katika kitabu changu. Kwa kuwa nilijua kuwa Ndugu Haile alitaka kunihoji kuhusu dhughuli zangu za kuelimisha umma, nilichukua pia nakala ya kitabu changu cha Matengo Folktales , ambacho n

Neema Komba Ashinda Tuzo ya Uandishi

Image
Neema Komba ni mwandishi chipukizi wa ki-Tanzania. Kama wewe ni mfuatiliaji wa uandishi wa Tanzania wa siku hizi, huenda tayari unafahamu habari zake. Mbali na uandishi, Neema ni mhamasishaji wa uandishi na sanaa husika kupitia jukwaa liitwalo la Poetista. Mwaka 2011 Neema alichapisha kitabu cha mashairi yake, See Through the Complicated . Nilikisoma muda si mrefu baada ya kuchapishwa. Mwishoni mwa mwezi Julai, 2012, nilipokuwa Tanzania, tulikutana Lion Hotel, Dar es Salaam, tukaongelea uandishi wake. Pamoja na mashairi, Neema ni mwandishi wa insha. Hivi karibuni nilianza kufahamu kuwa anaandika pia hadithi, niliposoma kuwa hadithi yake "Setting Babu on Fire" imeteuliwa kuwemo kati ya hadithi tatu zilizoteuliwa kushindania tuzo ya "Flash Fiction" ya Etisalat. Hayo yalikuwa mashindano makubwa ya uandishi barani Afrika. Hatimaye, "Setting Babu on Fire" imeshinda tuzo ya kwanza. Ushindi huu ni sifa kubwa kwa Neema mwenyewe na kwa Tanzania. Nik

Darasa la "Hemingway in East Africa 2013" Kando ya Ziwa Babati

Image
Mwezi Januari, 2013, nilikuwa Tanzania na wanafunzi kutoka Chuo cha St. Olaf katika kozi ya "Hemingway in East Africa." Niliitunga kozi hii mwaka 2006, kwa ajili ya Chuo cha Colorado. Kwa miaka kadhaa, kabla ya kutunga kozi hiyo, nilisoma maandishi ya Ernest Hemingway aliyoandika kufuatia safari zake mbili Afrika Mashariki, miaka ya 1933-34 na 1953-54. Lengo la kozi lilikuwa kuwafundisha wanafanuzi kwa kusafiri nao katika baadhi ya maeneo alimopita Hemingway, huku tukisoma maandishi yake kuhusu safari zake katika maeneo haya. Maandishi hayo ni pamoja na kitabu cha Green Hills of Africa na Under Kilimanjaro , hadithi ya "The Short Happy Life of Francis Macomber," barua, na insha kadhaa katika magazeti. Pichani wanaonekana wanafunzi na madereva wetu pembeni mwa Ziwa Babati. Katika Green Hills of Africa , Hemingway aliandika kuhusu Babati na Ziwa Babati:      We left, soon after midnight, ahead of the outfit, who were to strike camp and follow in the two l

Vitabu Nilivyonunua Jana na Leo

Image
Kila mtu ana mambo anayoyapenda sana, na yuko tayari kuyapata au kuyafanya kwa gharama yoyote. Vitabu ni kati ya vitu ninavyovipenda sana, na niko tayari kutumia gharama yoyote kuvipata. Imekuwa hivyo tangu nilipokuwa shule ya msingi. Mara kwa mara, katika blogu hii, nimeandika taarifa ya vitabu nilivyonunua. Siandiki taarifa ya kila kitabu, kwani wakati mwingine nasahau. Lakini leo nimekumbuka. Naandika kuhusu vitabu nilivyonunua jana na leo. Nilitoka zangu ofisini, nikaelekea kwenye duka la vitabu. Nje ya duka kulikuwa na "seli" ya vitabu. Kulikuwa na vitabu vingi sana vikiuzwa kwa bei nafuu. Hapo hapo nilijiunga na wengine waliokuwa wanavichambua vitabu hivyo na kuvinunua. Jungu kuu halikosi ukoko. Niliviona vitabu vinne vilivyonivutia kwa namna ya pekee, nikavinunua. Kimojawapo ni Wine to Water: How One Man Saved Himself While Trying to Save the World. Hilo jina tu lilinivutia, nikakumbuka hadithi ya muujiza wa Yesu wa kugeuza maji kuwa divai. Katika kukiangalia

Video ya Kumbukumbu ya Miaka Kumi ya Kitabu

Jana, binti yangu Zawadi na mimi tulirecodi video ya kumbukumbu ya miaka kumi tangu nilipochapisha kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Hatukuwazia tungefanya shughuli hiyo jana. Tulijishitukiza bila maandalizi. Tulitayarisha kompyuta nami nikaanza kuongea. Zawadi alifanya shughuli yote ya kiufundi hadi kuiweka video katika mtandao wa You Tube. Katika kumbukumbu hii ya miaka kumi ya kitabu changu, napenda kuwashukuru wasomaji wangu, familia, na marafiki na wengine wote walionihamasisha kwa namna moja au nyingine. Kwa mwezi huu wote, yeyote anayetaka kitabu hiki, popote duniani, ataweza kukipata kutoka kwangu kwa bei nafuu ya dola 12. Awasiliane nami kwa barua pepe, africonexion@gmail.com au simu (507) 403 9756. Mwisho wa fursa hii ni tarehe 31.

Mdau Anauliza Kama Ufisadi Utaisha Nchini

Image
Mdau anonymous ameomba tusome makala ifuatayo na ameuliza iwapo ufisadi utaisha Tanzania. Makala aliyoleta inamhusu Dr. Fulgence Mosha, anayeonekana pichani, daktari bingwa mstaafu wa hospitali ya KCMC, ambaye amekuwa akihangaikia mafao yake ya ustaafu kwa miaka kumi bila mafanikio. Makala aliyoileta mdau ni hii hapa.

Natamani Kuwatukana Akina "Anonymous"

Katika blogu kuna maudhi ya aina aina. Wanaoleta maudhi hayo ni hao wanaojiita "anonymous." Kwa kujificha namna hii, wanajisikia huru kusema cho chote, wakijua kuwa hakuna atakayewawajibisha. Siku chache zilizopita, niliandika ujumbe katika blogu ya Michuzi, nikiulizia kuhusu taratibu za ibada ya mazishi ya ki-Katoliki. Sikujificha. Kama ilivyo kawaida yangu, nilijitambulisha kikamilifu. Walitokea akina "anonymous" wakaongelea mambo ambayo hayakuonyesha nia ya kujibu suali nililouliza. Nilivyokuwa nasoma waliyoandika, niliona kuwa wananipotezea muda. Walikuwa wanakera. Kwa silika za kibinadamu, nilitamani kuwatukana, lakini niliamua kuachana nao, nikahamishia mada yangu katika blogu yangu. Kwanza, sidhani kama ni uungwana kuingia katika blogu ya mtu na kuigeuza kuwa uwanja wa malumbano yasiyo na tija au ya kuwakera watu. Ni kama kukaribishwa nyumbani mwa mtu halafu uanze kufanya utovu wa heshima. Miaka kadhaa iliyopita, Michuzi alilalamika kuhusu watu walio

Kofia Katika Mazishi ya Ki-Katoliki

Image
Niliona taarifa za msiba na mazishi ya Kapteni John Komba mitandaoni. Ni jambo la kushukuru kwamba waandishi na wapiga picha walituwezesha tulio mbali kuelewa mambo yalivyokuwa. Nilivyoona picha inayoonekana hapa kushoto, ya jeneza likiteremshwa kaburini, niliamua kuandika ujumbe katika blogu ya Michuzi nikisema kuwa nimekerwa na kitendo cha wahusika kuwa wamevaa kofia wakati wa shughuli hiyo. Niliuliza iwapo jambo hili linaruhusiwa kwa mujibu wa ibada za mazishi ya ki-Katoliki. Akina "anonymous" kadhaa wamejitokeza na kuandika hili au lile, katika sehemu ya maoni. Nami katika sehemu ile ya maoni, nimejaribu kuelezea zaidi suala langu, nikisema, kwa mfano, kuwa kwa askofu kuvaa kofia ya kiaskofu wakati wa kuendesha ibada ni sehemu ya mavazi yake rasmi ya ibada. Sikuona kama duku duku yangu imejibiwa. Badala yake, niliona watu wanazua mambo ambayo hayahusiani na ulizo langu, ulizo ambalo lilitokana na nia njema, yaani kujiridhisha kuwa tunaheshimu ibada na tunamheshimu

Utamaduni wa Kuwasomea Watoto Vitabu

Nimeandika mara kwa mara kuhusu suala la elimu, sio tu katika blogu hii, bali pia katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii , kitabu ambacho nilitegemea kitasomwa na wa-Tanzania wenzangu, lakini mambo yamekuwa kinyume. Kati ya mambo ambayo nimekuwa nikiyaongelea ni umuhimu wa kuwasomea watoto vitabu, jambo ambalo limejengeka katika utamaduni wa wa-Marekani. Nimekumbuka yote hayo leo baada ya kusoma makala hii hapa kama uthibitisho na changamoto. Hili ni kati ya mambo ambayo wa-Tanzania tunapaswa kujifunza. Nimethibitisha mwenyewe kuwa watoto wa Tanzania wanapenda vitabu, bali, kadiri wanavyokua, mapenzi hayo huzimishwa na watu wazima na jamii kwa ujumla. Kama wahenga walivyosema, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Baada ya muda, watoto wa ki-Tanzania hufuata utamaduni wa jamii wa kutothamini vitabu, na Taifa linaendelea kuzorota kielimu., wakati wenzetu wa-Marekani wanawalea watoto wao katika kupenda vitabu. Mwalimu Nyerere alikuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha

Nimeulizwa Inakuwaje Siuzi Vitabu Vyangu Tanzania

Leo katika mtandao wa Facebook kuna mdau kaniuliza inakuwaje siuzi vitabu vyangu Tanzania. Nimemshukuru kwa ulizo lake, nikajaribu kulijibu. Napenda kuandika machache kuhusu suali hili. Napenda kuanza kwa kusema kuwa vitabu hivyo vinapatikana mtandaoni, kama vile kwenye tovuti ya lulu na tovuti ya Amazon. Yeyote mwenye kadi ya "credit" kama vile VISA au MasterCard, anaweza kuvinunua. Haijalishi kama yuko Chake Chake, Dar es Salaam au Tukuyu. Ataletewa. Kama ana kifaa kama "kindle," ananunua bila tatizo. Ninafahamu kuwa ni wa-Tanzania wachache walioko Tanzania wanaoweza kununua vitu mtandaoni. Lakini kuna maelfu ya wa-Tanzania katika nchi kama Marekani wenye hizo kadi. Kama kuna nia ya dhati ya kununua kitabu, haikosekani njia. Mimi mwenyewe nimekuwa tayari kufanya mipango na wa-Tanzania wenye nia ya kuuza vitabu vyangu, kwa kuwapelekea. Nimewahi kufanya hivyo na Cultural Tourism Program (Longido), Bougainvillea Lodge (Karatu), na Cultural Tourism Program (M

Imekuwa Wiki ya Mafanikio

Wiki hii inayoisha imekuwa ya mafanikio makubwa kwangu. Napenda kwanza nifafanue kuwa dhana yangu ya mafanikio ni tofauti na ya wale wanaowazia fedha. Mimi ni mwelimishaji, darasani na katika jamii. Ni mtoa ushauri katika masuala ya tofauti za tamaduni na athari zake, hasa katika dunia ya tandawazi wa leo. Ushauri huo natoa kwa njia mbali mbali, hasa maandishi na mazungumzo na watu binafsi au vikundi. Dhana yangu ya mafanikio imejengeka katika shughuli hizo. Kwanza, nilijiandaa kwa ziara ya chuo cha South Central, mjini Mankato, ambako nilifanya mazungumzo na darasa la wanafunzi wanaojiandaa kwenda Afrika Kusini kimasomo, na halafu nikatoa mhadhara kwa wanajumuia hapo chuoni, ambao mada yake ilikuwa "Writing About Americans." Maandalizi ya mazungumzo hayo yote yalikhusu kukusanya fikra zilizokuwa akilini mwangu na kuziweka pamoja ili kukidhi mahitaji ya mazungumzo yale. Ilikuwa rahisi kujitayarisha kwa maongezi na wanafunzi waendao Afrika Kusini. Nmaongezi ya aina hiyo