Sunday, March 8, 2015

Natamani Kuwatukana Akina "Anonymous"

Katika blogu kuna maudhi ya aina aina. Wanaoleta maudhi hayo ni hao wanaojiita "anonymous." Kwa kujificha namna hii, wanajisikia huru kusema cho chote, wakijua kuwa hakuna atakayewawajibisha.

Siku chache zilizopita, niliandika ujumbe katika blogu ya Michuzi, nikiulizia kuhusu taratibu za ibada ya mazishi ya ki-Katoliki. Sikujificha. Kama ilivyo kawaida yangu, nilijitambulisha kikamilifu.

Walitokea akina "anonymous" wakaongelea mambo ambayo hayakuonyesha nia ya kujibu suali nililouliza. Nilivyokuwa nasoma waliyoandika, niliona kuwa wananipotezea muda. Walikuwa wanakera. Kwa silika za kibinadamu, nilitamani kuwatukana, lakini niliamua kuachana nao, nikahamishia mada yangu katika blogu yangu.

Kwanza, sidhani kama ni uungwana kuingia katika blogu ya mtu na kuigeuza kuwa uwanja wa malumbano yasiyo na tija au ya kuwakera watu. Ni kama kukaribishwa nyumbani mwa mtu halafu uanze kufanya utovu wa heshima.

Miaka kadhaa iliyopita, Michuzi alilalamika kuhusu watu waliokuwa wanafanya utovu wa nidhamu katika blogu yake. Hadi leo, ameweka angalizo kuwa mchangiaji aangalie asichafue hali ya hewa wala kujeruhi hisia za mtu au watu.

Mimi mwenyewe nimekumbana tena na tena na akina "anonymous" wasio na uungwana. Kwa mfano, "anonymous" mmoja aliwahi kuniambia kwa kiburi kuwa ana uhuru wa kusema katika blogu yangu.

Napingana na "anonymous" huyu. Ingawa binafsi nimejiamulia kuifanya blogu yangu iwe huru kwa yeyote kutoa maoni yake, lakini sikubali kwamba yeyote ana haki ya kuandika katika blogu yangu.

Mtu anapokuja katika blogu yangu ninamwona kama mtu ninayemkaribisha nyumbani mwangu. Hawezi kudai kuwa ana uhuru kusema lolote atakalo katika nyumba yangu. Lazima atumie busara.

Mwenye nyumba ana haki ya kumtolea nje yeyote asiyeheshimu nyumba. Hivyo hivyo, nina haki ya kumzuia mtu yeyote kuweka maoni yake katika blogu yangu. Ninaweza kutumia njia iliyopo katika muundo wa blogu ya kuzuia maoni au kuondoa maoni.

Kwa hiari yangu, nimeamua kutotumia utaratibu huu wa kuzuia au kuondoa maoni. Lakini mtu asiniambie kwamba ana haki ya kutoa maoni katika blogu yangu.

Hii si mara yangu ya kwanza kuwaongelea akina anonymous wanaokera. Mara ya kwanza, niliandika makala hii hapa. Baadaye niliandika makala hii hapa.

Sijui wanablogu wenzangu wana maoni gani. Sijui wanaoandika au wanaowazia kuandika katika blogu wana maoni gani. Sijui wasomaji wa blogu wanasemaje.

4 comments:

PBF Rungwe Pilot Project said...

Naungana nawe Profesa kuwathibiti watu wasiotaka kujitambulisha na hapohapo wanatataka kutoa maoni yenye kuudhi. Kwa namna nyingine, yafaa kuweka utaratibu wa namna ya kuyapitia maoni hayo na kuyahakiki iwapo unakubaliana nayo au. Japo kwa jinsi hii unaweza kupunguza kasi ya mawazo kwenye blogu yako.

Mbele said...


PBF Rungwe Pilot Project,

Shukrani sana kwa mchango wako. Wazo lako la kuwa na utaratibu wa kuyapitia maoni na kuyahakiki naona ni wazo zuri.

Kuwaacha wakorofi wajiandikie wanavyotaka, kama ambavyo nimewaruhusu hadi sasa, ni suala ambalo nadhani ingekuwa bora nikaliangalia upya, kwani blogu ikiruhusu kero na ukorofi inakuwa imegeuzwa kuwa jalala la taka taka.

Labda niseme tu kuwa, yeyote, hata mkorofi, afanye juhudi ya dhati kujenga hoja. Kama ukorofi wake ni wa kuelimisha au kuendeleza mjadala kwa maana kwamba amejenga hoja, nitaendelea kuruhusu.

Lakini kama ni kuropoka matusi au maneno ya kukera yasiyo na msingi au umbo la hoja, itabidi nichukue uamuzi wa kuyaondoa, ili kulinda heshima ya blogu na heshima ya wasomaji.

Anonymous said...

samahani kama nitakuwa nje ya mada, naomba msome hii habari, halafu tutafakari kama ufisadi utakaa uishe nchii hii.
http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Daktari-bingwa-KCMC-/-/1597296/2647704/-/1h4mghz/-/index.html

Mbele said...

Ndugu anonymous, nimeguswa kwa namna ulivyolileta suala/suali lako. Kwa heshima yako, nimeamua kuliweka kama mada mpya katika blogu hii.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...