Posts

Showing posts from January, 2017

Kitabu Nilichonunua Leo: "The Highly Paid Expert"

Image
Leo nilikwenda Minneapolis na wakati wa kurudi, nilipita Mall of America, kuangalia vitabu katika duka la Barnes & Noble. Nilitaka hasa kuona kama kuna vitabu vipya juu ya mwandishi Ernest Hemingway. Niliangalia scheme vinapowekwa vitabu vya fasihi, nikakuta kitabu kipya juu ya Ernest Hemingway, Everybody Behaves Badly: The Backstory to 'The Sun Also Rises.' kilichoandikwa na Lesley M.M. Blume. Kwa kuwa nimezama sana katika uandishi wa Hemingway, maisha na falsafa yake, na kwa kuwa nimeshasoma  The Sun Also Rises , nilitamani kukinunua kitabu hiki, ambacho, kwa maelezo niliyoyaona, kinazungumzia yaliyo nyuma ya pazia. Sikuwa na hela za kutosha, kwa hivyo nikaamua kuangalia vitabu vingine. Nilitumia muda zaidi katika sehemu ya "Business/Management." Huwa ninapenda sana kununua na kusoma vitabu vya taaluma hii, kwani vinanifundisha mengi kuhusu mambo ya ujasiriamali na biashara. Taaluma hii inanisaidia katika kuendesha shughuli za kampuni yangu ya Africonexi

Ukabila wa Tanzania

Image
Kuna dhana kuwa hakuna ukabila Tanzania, kwa maana ya ubaguzi au uhasama miongoni mwa makabila. Kwa ujumla dhana hiyo ni ukweli, hasa tukifananisha na baadhi ya nchi zingine.  Lakini, ni wazi kuwa wa-Tanzania wengi wameamua kubuni namna ya kuifanya nchi yetu ifurahie matunda ya ukabila. Kwa kuwa ubaguzi na uhasama wa makabila umeshindikana, wamegundua kuwa ubaguzi na uhasama unawezekana kwa njia ya vyama vya siasa. Mimi ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa ninaangalia mambo wanayofanya wa-Tanzania wenye vyama, na ninaona jinsi yanavyofanana na yale yanayotokea katika nchi zenye ukabila. Kwa mfano, katika nchi moja jirani, ukabila ulivyokolea, wahusika walikuwa wanaitana majina ya kudhalilisha, hasa ya wadudu au wanyama. Hiyo ilikuwa ni sehemu ya itikadi ya uhasama.  Hali hiyo tayari imeshamiri Tanzania. Watu hawaitwi binadamu, bali nyumbu, fisi, na kadhalika. Kule Rwanda, kabla ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, katika propaganda dhidi ya wale waliokusudiwa kuu

Maandamano Makubwa Dhidi ya Rais Trump

Jana hapa Marekani yamefanyika maandamano makubwa dhidi ya rais Donald Trump, ambaye aliapishwa juzi. Maandamano haya yaliyoandaliwa na kukusudiwa kwa wanawake, yanasemekana kuwa makubwa kuliko yote yaliyowahi kufanyika katika historia ya Marekani kwa siku moja. Maandamano haya yamefana sana, kwa mahudhurio na hotuba mbali mbali, na yametoa ujumbe wa wazi kuwa serikali ya Rais Trump isitegemee kuwa itatekeleza ajenda yake bila vipingamizi. Marekani ni nchi inayoheshimu uhuru wa watu kujieleza. Katiba inalinda uhuru huo. Ndio maana maandamano ya kumpinga Rais Trump yalifanyika nchi nzima bila kipingamizi. Polisi walikuwepo kwa ajili ya kulinda amani, si kuzuia maandamano, wala kuwakamata wahutubiaji waliokuwa wanamrarua Rais Trump. Polisi wana wajibu wa kuhakikisha kuwa waandamanaji wanayo mazingira muafaka na fursa kamili ya kutekeleza haki yao ya kuandamana na kuelezea mawazo yao. Ninajua kuna wengine walioshiriki maandamano ya jana ambao si wa-Marekani. Kuna wakimbizi na wahamiaj

Nimejipatia Vitabu Vingine vya Bure

Image
Jana niliandika  katika blogu hii kuhusu vitabu nilivyovipata jana hiyo hiyo. Nilisema kuwa nilivipata hapa chuoni St. Olaf. Leo nilipita tena hapo, nikaviona vitabu vingi vya soshiolojia, na vichache vya taaluma zingine. Nilichukua vitatu. Kimoja ni Who Speaks for Islam?: What a Billon Muslims Really Think ,  kilichoandikwa na John L. Esposito na Dalia Mogahed. Ni matokeo ya utafiti uliofanywa miongoni mwa wa-Islam kutoka nchi nyingi, ili kubaini mitazamo yao juu ya masuala kadhaa, kama vile mahusiano baina ya nchi za ki-Islamu na mataifa ya Magharibi, wanawake katika jamii za ki-Islam, na jihad. Kitabu kingine ni Student Learning Abroad: What Our Students Are Learning, What They're Not And What We Can Do About It. kilichohaririwa na Michael Vande Berg, R. Michael Paige, and Kris Hemming Lou. Nimekisikia kitabu hiki kwa miaka miwili au mitatu, na nilitaka kukinunua. Imekuwa kama muujiza kuwa nimeiona nakala, nikajuchukulia. Kutokana na nilivyofahamu, kitabu hiki ni muhimu

Vitabu Nilivyojipatia Leo

Image
Leo, baada ya wiki nyingi kidogo, nimeona nirejee tena kwenye mada ambayo nimekuwa nikiiandikia tena na tena katika blogu hii. Ni juu ya vitabu ninavyojipatia, iwe ni kwa kununua, au kwa namna nyingine. Leo asubuhi, kama kawaida, nilienda chuoni St. Olaf kufundisha. Nilipoingia katika jengo la maktaba, ambamo pia ni makao ya idara yangu ya ki-Ingereza, nilipita kwenye meza ambapo huwekwa vitabu na makabrasha kwa ajili ya yeyote anayehitaji. Niliona meza imejaa vitabu kuliko siku nyingine yoyote iliyopita, nikaamua kuviangalia. Niliona kuwa vyote vilikuwa vitabu vya taaluma, hasa masuala ya wanawake na jinsia. Niliamua kujichukulia vitatu, baada ya kuangalia ndani na kuona maelezo ya vitabu hivi. Kitabu kimojawapo ni Sex & Power , kilichotungwa na Susan Estrich. Niliona maelezo kuwa mwandishi alikuwa profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Harvard na baadaye profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha California ya Kusini. Ameandika vitabu kadhaa na makala mbali mbali. Alikuwa

Erica Huggins Ahutubia Chuoni St. Olaf

Image
Leo mwanaharakati Erica Huggins amehutubia chuoni St. Olaf. Alialikwa kuhutubia kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya Martin Luther King Jr. Erica Huggins alikuwa mwanaharakati maarufu katika Black Panther Party, na ameendelea kuwa mwelimishaji wa jamii, kama inavyoelezwa katika tovuti yake. Ameelezea historia yake katika Black Panther Party, jinsi mume wake alivyouawa na idara ya upelelezi ya FBI, na jinsi yeye mwenyewe alivyofungwa kwa miaka miwili. Humo kifungoni alitumia muda wake kujichunguza nafsi na akili yake na masuala ya maisha na ulimwengu kwa umakini na utulivu mkubwa. Anaendelea na jadi hiyo, ambayo huitwa "meditation," kila siku. Amesema kuwa mifumo yote ya kihasama na ukandamizaji, fikra zote za kihasama na kikandamizaji ni mambo yaliyoundwa na wanadamu. Kwa hivyo, wanadamu wana uwezo wa kuleta mabadiliko kwa kuunda mifumo na fikra zenye kujenga maelewano, upendo, na maendeleo ya binadamu. Alisema kuwa tunapaswa kuviheshimu viumbe vyote, sio binadamu tu

Kitabu cha Uchambuzi wa "Hamlet"

Image
Mwandishi maarufu Ernest Hemingway alisema, "There is no friend as loyal as a book," yaani hakuna rafiki wa kweli kama kitabu. Vyovyote unavyotaka kuitafsiri kauli hii ya Hemingway, ukweli ni kuwa kusoma kitabu kizuri ni mithili ya kuongea na rafiki wa kweli. Baada ya kusoma Hamlet , kama nilivyoelezea katika blogu hii, nimeamua kusoma kitabu cha insha juu ya Hamlet , kinachoitwa Hamlet , ambacho kimehaririwa na Susanne L. Wofford. Ni kitabu cha insha ambazo zinaongelea nadharia za fasihi, na zinaichambua Hamlet kwa kutumia hizo nadharia tofauti. Nadharia hizo ni "Feminist Criticism," "Psychoanalytic Criticism," "Deconstruction," "Marxist Criticism," na "The New Historicism." Lakini, pamoja na maelezo ya kina ya nadharia hizo, na uchambuzi mbali mbali wa Hamlet, kitabu hiki kina pia tamthilia yote ya Hamlet , toleo la  The Riverside Shakespeare . Pia kitabu hiki kina maelezo ya maisha ya Shakespeare na mazingira

Zawadi Kutoka Ramble Pictures Kwa Heshima Ya Hemingway

Image
Wiki iliyopita nimepata zawadi ya picha kutoka Ramble Pictures, kampuni ya kutengeneza filamu. Kampuni hiyo ndiyo iliyotengeneza filamu ya Papa's Shadow, inayohusu maisha na safari za mwandishi maarufu Ernest Hemingway Afrika Mashariki, pamoja na maandishi yake kuhusu Afrika Mashariki. Sehemu kubwa ya filamu hiyo ni mazungumzo baina ya Mzee Patrick Hemingway na mimi, kuhusu masuala hayo. Picha niliyopewa inaitangaza filamu ya Papa's Shadow. Inamwonesha Ernest Hemingway, Patrick Hemingway na mimi, Kuna pia Mlima Kilimanjaro na nchi tambarare chini ya mlima, na pia ndege ikiwa angani. Hiyo picha ya mlima na mazingira yake, pamoja na ndege, inakumshia hadithi maarufu ya Hemingway, "The Snows of Kilimanjaro." Nimeguswa na picha hii. Ni heshima kubwa kuliko ninavyostahili kuwekwa sambamba na Ernest Hemingway na Patrick Hemingway. Ernest Hemingway alileta mapinduzi katika uandishi na alitunukiwa tuzo ya Nobel katika fasihi mwaka 1954. Patrick Hemingway ni mtu muhi

Msomaji Wangu Mpya

Image
Jirani yangu mama Merri, mdau na mpiga debe mkubwa wa maandishi na shughuli zangu za uelimishaji, amenitambulisha kwa mwalimu Paul White anayeishi California. Alianza kuniambia habari za mwalimu huyu miezi kadhaa iliyopita, wakati aliponiambia kuwa anataka kumpelekea kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences .  Alinunua, nikasaini, akampelekea. Baada ya hapo, nami nilianza kutafuta taarifa za mwalimu huyu mtandaoni. Niliguswa sana na juhudi na mafanikio yake katika kuwafundisha na kuwapa mwelekeo vijana walioshindikana, waliokata tamaa, wahalifu, na ambao jamii iliwaona hawafundishiki wala hawawezi kuokolewa. Katika maisha yangu yote, sijawahi kusoma kuhusu mwalimu mwenye mtazamo na moyo kama alio nao mwalimu White. Mfano moja wa taarifa zake zilizonigusa ni mahojiano haya hapa.  Nilivyosoma taarifa zake, nilifikiwa na wazo la kuanzisha mpango kama wa kwake nchini mwangu, kuwaokoa vijana waliotemwa na mfumo wa elimu, waliokata tamaa, wahalifu, ambao

Namshukuru Mteja

Image
Leo nimepita kwenye mtandao wa Amazon kuangalia vinapopatikana vitabu vyangu, nikaona ujumbe ulioandikwa jana na mteja kuhusu kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Ni mmoja wa wateja ambao baada ya kununua na kusoma kitabu, huweka maoni yao kuhusu kitabu hapo mtandaoni. Ninaguswa na wateja hawa na ninapenda kuwashukuru. Ninazingatia kuwa hela walizotumia kununulia kitabu changu wangeweza kuzitumia kwa mahitaji mengine. Halafu, ninawashukuru kwa kitendo chao cha kuandika maoni. Wananitangazia kitabu bila malipo bali kwa hisani yao. Huyu mteja aliyeandika jana, anaonekana ni m-Marekani, na amesema: Great book to compare things we do in the United States and how it differs in Africa. Some of the differences would be insulting to Africans and I would not have known it Highly recommend this book if you are traveling to Tanzania as author is from there. It is a short, easy read. Natafsiri Kitabu bora kwa ajili ya kufananisha mambo tufanyayo Marekani

Mazungumzo na Wanafunzi wa Chuo cha Gustavus Adolphus

Image
Leo mchana nilikuwa Mount Olivet Conference & Retreat Center katika maongezi na wanafunzi wa chuo cha Gustavus Adolphus wanaokwenda Tanzania kimasomo. Profesa Barbara Zust, alikuwa amenialika, kama nilivyoandika katika blogu hii. Wanafunzi wengi wa programu hii wanasomea uuguzi, na lengo la kwenda Tanzania ni kujifunza namna masuala ya afya na matibabu yalivyo katika mazingira tofauti na ya Marekani, kwa maana ya utamaduni tofauti. Kwa lengo hilo, wanafunzi husoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Kwa hivyo, hiyo jana, kama ilivyokuwa miaka iliyopita, niliwakuta wanafunzi wamesoma kitabu hiki na wamejizatiti kwa masuali ambayo yalinithibitishia kuwa ni wanafunzi makini wenye duku duku ya kujua mambo. Tulikuwa na mazungumzo ya kina yaliyodumu kwa zaidi ya saa mbili. Mwanafunzi mmoja, msichana, aliniambia kuwa yeye na mama yake walisoma kitabu changu pamoja. Taarifa hii imanigusa. Ni kama vile mzazi ametafuta namna ya kushiriki yale am

Shari ya Mwaka Mpya: "The Second Coming"

Image
Kwa kawaida, kwa kuwa wasomaji wengi wa blogu hii ni wa-Tanzania wenzangu, tunavyoanza mwaka mpya, ningewatakia heri ya mwaka mpya. Badala yake, kwa kuzingatia tunakoelekea kisiasa, ninaleta shairi la William Butler Yeats, "The Second Coming," ambalo niliwahi kuliweka katika blogu hii. Angalau kwa jinsi ninavyolisoma shairi hili, ninaona lina ujumbe unaofaa zaidi kuliko "heri ya mwaka mpya." The Second Coming Turning and turning in the widening gyre The falcon cannot hear the falconer; Things fall apart; the centre cannot hold; Mere anarchy is loosed upon the world, The blood-dimmed tide is loosed, and everywhere The ceremony of innocence is drowned; The best lack all conviction, while the worst Are full of passionate intensity. Surely some revelation is at hand; Surely the Second Coming is at hand. The Second Coming! Hardly are those words out When a vast image out of Spiritus Mundi Troubles my sight: somewhere in sands of the desert A shape