Kuna dhana kuwa hakuna ukabila Tanzania, kwa maana ya ubaguzi au uhasama miongoni mwa makabila. Kwa ujumla dhana hiyo ni ukweli, hasa tukifananisha na baadhi ya nchi zingine.
Lakini, ni wazi kuwa wa-Tanzania wengi wameamua kubuni namna ya kuifanya nchi yetu ifurahie matunda ya ukabila. Kwa kuwa ubaguzi na uhasama wa makabila umeshindikana, wamegundua kuwa ubaguzi na uhasama unawezekana kwa njia ya vyama vya siasa.
Mimi ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa ninaangalia mambo wanayofanya wa-Tanzania wenye vyama, na ninaona jinsi yanavyofanana na yale yanayotokea katika nchi zenye ukabila.
Kwa mfano, katika nchi moja jirani, ukabila ulivyokolea, wahusika walikuwa wanaitana majina ya kudhalilisha, hasa ya wadudu au wanyama. Hiyo ilikuwa ni sehemu ya itikadi ya uhasama.
Hali hiyo tayari imeshamiri Tanzania. Watu hawaitwi binadamu, bali nyumbu, fisi, na kadhalika. Kule Rwanda, kabla ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, katika propaganda dhidi ya wale waliokusudiwa kuuawa walipewa majina kama "inyenzi" (kwa ki-Ingereza, "cockroaches").
Wa-Tanzania wenye vyama wanatupeleka huko huko. Maandalizi ya kiitikadi yameshakamilika. Vitendo vya kuhujumiana, vitisho, na hata mauaji vimekuwa vikifanyika, hasa wakati wa kampeni za uchaguzi, na kuna kila dalili kuwa vitendo hivi vitashamiri.
Mwalimu Nyerere kabla hajaaga dunia, alihofia hali iliyokuwa ikijitokeza Tanzania, akauliza iwapo wa-Tanzania tumechoshwa na amani. Ni wazi kuwa wa-Tanzania tuliziba masikio.
Wenye vyama wanazidi kuvuruga amani, sio tu kwa vitendo wanavyofanyiana, bali pia kwa hofu wanayoijenga mioyoni mwa sisi tusio na vyama, ambao ni watu wa amani. Ni ujinga kujidai kuwa sisi ni nchi ya amani, wakati mioyoni hakuna amani, bali hofu.
Enzi za Mwalimu Nyerere, kulikuwa na viongozi, ambao walitambua na kuzingatia umuhimu wa kudumisha mazingira ya amani nchini. Leo, wale wanaotegemewa kuwa viongozi ndio vinara na wahamasishaji wa uvunjifu wa amani. Ni kama ilivyokuwa Rwanda, kuelekea mwaka 1994.
Kwa kuwa hatujabahatika kuwa na ukabila kama wenzetu wa nchi zingine, wa-Tanzania wengi wameona tunahitaji nasi kufaidi matunda ya ukabila kwa kutumia vyama vya siasa. Mungu isamehe Tanzania.
No comments:
Post a Comment