Sunday, January 8, 2017

Msomaji Wangu Mpya

Jirani yangu mama Merri, mdau na mpiga debe mkubwa wa maandishi na shughuli zangu za uelimishaji, amenitambulisha kwa mwalimu Paul White anayeishi California. Alianza kuniambia habari za mwalimu huyu miezi kadhaa iliyopita, wakati aliponiambia kuwa anataka kumpelekea kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Alinunua, nikasaini, akampelekea.

Baada ya hapo, nami nilianza kutafuta taarifa za mwalimu huyu mtandaoni. Niliguswa sana na juhudi na mafanikio yake katika kuwafundisha na kuwapa mwelekeo vijana walioshindikana, waliokata tamaa, wahalifu, na ambao jamii iliwaona hawafundishiki wala hawawezi kuokolewa.

Katika maisha yangu yote, sijawahi kusoma kuhusu mwalimu mwenye mtazamo na moyo kama alio nao mwalimu White. Mfano moja wa taarifa zake zilizonigusa ni mahojiano haya hapa. Nilivyosoma taarifa zake, nilifikiwa na wazo la kuanzisha mpango kama wa kwake nchini mwangu, kuwaokoa vijana waliotemwa na mfumo wa elimu, waliokata tamaa, wahalifu, ambao jamii inaamini wameshindikana.

Hatimaye, kwa kuhimizwa na mama Merri, jana nilimpigia simu mwalimu White. Mke wake aliitika akaniambia kuwa mwalimu alikuwa ameondoka kodogo,  nikaacha namba ya simu. Baada ya nusu saa hivi, mwalimu alinipigia simu, tukaongea kwa msisimko wa furaha. Aliniambia kuwa anakifurahia kitabu changu, akanukuu sehemu mbili tatu kusisitiza tofauti baina ya wa-Afrika na Wamarekani.

Ameongea kirefu, akanihimiza niandae mhadhara wa TED, na pia nifikirie kwenda California kutoa mihadhara kuhusu masuala yanayoikabili jamii ya wa-Marekani, kama vile tofauti za tamaduni. Tumefurahi kuwasiliana na tunafurahi zaidi kuwa tutaendelea na mawasiliano. Nimeona nijiwekee hizi kumbukumbu zangu, kwani ni lengo langu moja muhimu katika kublogu. 

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...