Migogoro ya Kitamaduni Sehemu ya Kazi
Kadiri dunia inavyozidi kuwa kijiji, kwa maana kwamba umbali kutoka sehemu moja hadi nyingine unazidi kupoteza umuhimu, na mawasiliano baina ya watu yanazidi kuwa rahisi, na kukutana uso kwa uso inazidi kuwa rahisi, tutakuwa na kazi kubwa ya kujizatiti kukabiliana na tofauti za tamaduni duniani. Watu wa kila utamaduni wana namna yao ya kufikiri, kuelewa, kufanya mambo, kuongea, na kadhalika. Wao kwa wao wanaelewana. Lakini dunia ya leo si ya watu kukaa na wenzao wanaoelewana tu, bali ni ya kukabiliana na watu wa tamaduni tofauti. Haijalishi kama uko Dar es Salaam, Tokyo, au Los Angeles. Mchanganyiko wa watu wa tamaduni mbali mbali unazidi kuziathiri sehemu zote za dunia. Hapa Marekani, nimeona juhudi inayofanyika ya kujizatiti na hali hiyo. Sehemu za kazi, kwa mfano, kutokana na kuwa na wafanyakazi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wahusika wanaanza kuelewa umuhimu wa kujielimisha na kuelimishana kuhusu tofauti za tamaduni, ili kuzuia migogoro na kuboresha mahusiano kazini. Mimi m