Mhadhara kwa Wamarekani Waendao Afrika Mashariki

Jioni hii, nimetoa mhadhara kuhusu tofauti za utamaduni wa Mwafrika na ule wa Mmarekani, kwa walimu na wanafunzi wa vyuo vya St. Benedict/St. John's, kwenye mji wa St. Joseph, Minnesota. Nilialikwa na idara inayoshughulika na masomo ya amani. Mhadhara huo ulihudhuriwa pia na watu ambao hawako katika idara hii.

Walimu walionialika wamesoma na wanakitumia kitabu changu kinachoelezea tofauti za tamaduni hizi. Baadhi ya hao walimu na waliohudhuria wanajiandaa kwa safari ya kwenda Kenya na Tanzania wiki za karibuni.

Mhadhara wangu ulikuwa sehemu ya matayarisho ya safari. Nilifanya nilivyoweza kuwaeleza mambo muhimu ya kuzingatia, nikinukuu niliyoeleza katika kitabu changu. Jambo moja la msingi nililosisitiza ni kuwa tunapofanya uamuzi kushirikiana na watu wa utamaduni tofauti na wetu, tuzingatie sana suala la kujielimisha kuhusu tofauti za tamaduni zetu, tangu mwanzo na wakati wote wa mahusiano hayo, na baada ya hapo pia. Tusipofanya hivyo, tutajikuta katika matatizo yasiyo ya lazima.

Baada ya mhadhara wangu, kama kawaida, tulikuwa na kipindi cha masuali na majibu. Nilikuwa nimewaeleza kwa mfano, jinsi waMarekani wanavyotofautiana na waAfrika kuhusu suala la kuwahi. Nilisema wazi kuwa waMarekani, ambao kwao suala la kuwahi ni muhimu sana, wawe tayari kuona tofauti wanapokuwa Afrika. Mtu mmoja akaniuliza kama itakuwa ni sahihi kwake kuchelewa atakapokuwa Afrika Mashariki. Nilimjibu kuwa akiwahi ni sawa, ila asisumbue akili yake akiona watu wamechelewa. Atulie, maana watakuja tu, kwani wana majukumu mengi humo njiani, kama vile kusalimiana vizuri na watu wanaokutana nao.

Kama nilivyosema, baadhi ya watu hao wataenda Tanzania, sehemu za Dar es Salaam, Njombe na Songea. Nimevutiwa kwa namna ya pekee na kikundi hicho, kwani kule Songea wataishi kwa wiki moja mahali ambapo nilisoma shule ya kati, ambapo panaitwa Hanga. Wataenda pia Mbamba Bay. Niliposikia hivyo, nilikumbuka nilivyotembelea Mbamba Bay mwaka jana, nikaandika habari zake.

Comments

Umefanya vizuri kuwajulisha mapema hilo suala la kuchelewa. Kwana kwetu Afrika hakuna haraka utakuta mtu anakwenda sehemu na akikutana na rafiki basi anaongea naye na baadaye anaendelea na safari. Lakini kwa mtu usiyezoea utapata shida.
Bennet said…
Huyo aliyeuliza kwamba akichelewa sehemu ni sawa, aangalie asije akachelewa kwenye vombo vya usafiri kama ndege, mabasi na boti maana vitamuacha. Vyombo ya usafiri nilivyovitaja kwa hapa nchini vinaenda na muda.

Natumaini wataifurahia sana nchi yetu hasa kipindi hiki ambapo joto limepungua kidogo, natumai pia wanafahamu kwamba hiki ni kipindi cha mvua kwa sehemu nyingi za Tanzania.
Albert Kissima said…
Swala la kwenda na muda Afrika mashariki hususani Tanzania linachukuliwa kama ni utamaduni ijapokuwa wazi inajulikana kuwa ni udhaifu. Hivi hakuna namna kabisa ya kuweza kuondokana na hali hii, yani kuijengea jamii mazingira ya kujali muda kuliko kuchukulia hali hii kuwa ya kawaida? Mimi nadhani hili linawezekana kwani kuna miongoni mwetu ambao wanaweza kutunza muda ipasavyo. Tujiulize wao wanawezaje.

Hali hii tunaweza kuiepuka tukiipa msisitizo wa kutosha. Wenyewe huwa tunalea hali hii kwa kuwasubiria wachelewaji. Waliofika ktk muda muafaka waendelee ili na wengine wajifunze, watambue kuwa kujali muda ni jambo muhimu.


Kwa nini kumsubiria mchelewaji?
Atazoea lini kwenda na muda?
Mbele said…
Ndugu Kissima, suali lako ni gumu. Ninachoweza ni kujiuliza suali kutokana na suali lako: je, ni bora kuwa na utamaduni ulioko mahali kama Marekani, ambako kuwahi ni muhimu zaidi kuliko kuongea na watu, au ni bora utamaduni wetu wa kuongea na watu kuliko kuwahi?

Hisia zangu ni kuwa utamaduni wetu unajali ubinadamu: watu mnapokutana mnajuliana hali kwa undani. Kama mtu ana tatizo nyumbani, mnapeana hiyo taarifa, na kama kuna suala la kusaidiana, mnaelezana.

Hii ni tofauti na mahali kama Marekani, ambako watu wanapishana pengine bila hata salimio lolote, kwa vile wanakimbilia kuwahi mahali.

Suali ni je, wanawahi nini, na wanafaidikaje? Tunaweza kujibu kwa namna mbali mbali, lakini kitu kimoja kinachowakabili ni "stress." Hili ni tatizo kubwa katika maisha yao.

Ngoja niishie hapa, kwa leo.
Albert Kissima said…
Nashukuru Prof Mbele kwa majibu yako mazuri.Nimekuelewa, pia nina machache ya kuongezea.

Mpaka sasa, kuna tamaduni nyingi tu ambazo kizazi cha leo hapa Tanzania hakijazikuta, hii ikiwa na maana kwamba tamaduni zinabadilika.Hapa namaana kuwa hata tamaduni ambazo zinaonekana hazina manufaa hazinabudi kuachwa.

Kila jambo linawakati wake.Kila jambo lifanyike kwa wakati unaostahili.Mambo yafanyike kulingana na lazima na hiari. Kwa sababu kufika mahali fulani ipo kwenye ratiba yangu na wengine wanafahamu hivyo na wanategemea uwepo wangu, nalazimika kufika kwa wakati na kama ni kusalimiana(mfano) na watu ni lazima kuwe na mipaka, na jambo lolote litalohitaji uwepo wangu ktk jamii itanibidi nitoe taarifa mapema ili wale wanaonisubiria wajue fika kuwa sitatokeza.


Utamaduni wa waMarekani si mzuri na hata huu wa kwetu si mzuri.Mimi nadhani utamaduni unaotakiwa hapa ni wa kuwahi kule mtu aendako na angalao salam kwa watu si mbaya(ambazo hazihusishi stori ambazo zitapelekea mtu kuchelewa), na hili litawezekana kama watu tutakuwa wawazi, kwamba ninawahi mahali, labda tukutane muda fulani au kwa msaada zaidi fika hapo nyumbani.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini