Naenda kwa wa-Nyakyusa

Hivi karibuni, nitakuwa Tanzania na wanafunzi katika programu ya masomo inayoendeshwa na vyuo kadhaa vya Marekani kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam . Kabla ya kuwafikisha Chuo Kikuu Dar es Salaam ambapo watasoma kwa muhula mmoja, nitakuwa nao maeneo ya nyanda za juu, hasa Iringa. Lakini, katika kupanga safari hii, nimeamua kuwafikisha hadi Mbeya na Ziwa Nyasa , wakaone na kujifunza. Iringa naifahamu vizuri, ila Mbeya nilipita tu mara moja, miaka ya mwisho ya sabini na kitu. Wakati nangojea kwenda Mbeya, nawazia utamaduni wa wa-Nyakyusa. Mimi kama mtafiti, nimesoma kiasi kuhusu masimulizi yao ya jadi. Ninakumbuka maandishi ya watafiti kama Monica Wilson. Nina kitabu kiitwacho The Oral Literature of the Banyakyusa , kilichoandikwa na Christon S. Mwakasaka. Nadhani nilikinunua Dar es Salaam, nikawa nakisoma mara moja moja. Lakini wakati huu ninapongojea safari ya Mbeya, kitabu hiki kinanivutia kwa namna ya pekee. Kina hadithi za jadi, lakini vile vile nyimbo na tungo