Saturday, June 11, 2011

Waandishi Tumekutana Leo

Leo nilienda Minneapolis kushiriki mkutano wa waandishi wa-Marekani Weusi, kama nilivyoandika hapa. Mkutano huu, uliofanyika katika Center for Families, ni sehemu ya maandalizi ya maonesho ya vitabu ya tarehe 16 mwezi huu, katika maktaba ya Magers and Quinn. Waandaaji wa shughuli zote hizi ni Jeffrey Groves na Shatona Kilgore-Groves, wanaoonekana hapa juu.

Mkutano wa leo ulikuwa ni wa kufahamiana. Kila mtu alipata fursa ya kutoa maelezo mafupi kuhusu maisha na shughuli zake za uandishi. Baadhi ni chipukizi, ambao wamechapisha kitabu kimoja tu, na baadhi ni wazoefu, waliochapisha vitabu kadhaa. Baadhi ya vitabu vinahusu maisha binafsi; vingine vinahusu mafunzo mbali mbali, hadithi za kubuni, mashairi, na falsafa. Wengine wameandika vitabu vya watoto. Nami nilipata fursa ya kuongelea vitabu nilivyoandika.
Watu waliongelea maisha yao na kwa nini wanaandika. Baadhi, kama hao akina mama wanoonekana kushoto, wamepitia maisha machungu yasiyoelezeka, yanayowafanya baadhi ya wanadamu wajiue. Kuandika ni namna ya kujiponya ili kuendelea na maisha
Baadhi ya waandishi nilikuwa nimefahamiana nao kabla, kama vile Mahmoud el Kati, Joyce Marrie, Gerard Montgomery, na Jeff na Shatona Groves, ambao kitabu chao, A Black Parent's Memoir, ninakiandikia mapitio. Lakini imekuwa bahati leo kufahamiana na waandishi wengi kwa mpigo.

Mkutano wa leo umeleta msisimko mkubwa miongoni mwa washiriki. Tumekubaliana kuwa kukutana kwa namna hii ni hatua nzuri na muhimu; inatakiwa iwe jadi ya kuendelezwa. Kutokana na mafanikio ya mkutano wa leo, sote tunayangojea kwa hamu maonesho ya Juni 16, ambayo watu wengi wanategemewa kuhudhuria.

2 comments:

Christian Sikapundwa said...

Hongera sana Profesa kwa kukutana wanataaluma mahala pamoja,ni bahati ya pekee waandishi wa vitabu kukutana kubadilishana uzoefu.

Pia nategemea manesho hayo ya tarehe 16 yatajumuisha machapisho yako pia.

Mbele said...

Ndio Mzee Sikapundwa. Vitabu vyangu vyote vitakuwepo kwenye maonesho hayo ya tarehe 16. Sawa na vitabu vya waandishi wengine, viko tayari katika lile duka la Magers and Quinn ambalo ni kubwa kiasi kwamba Tanzania hatuna mfano wake. Lakini kwa hapa Marekani, maduka makubwa sana ya vitabu ni jambo la kawaida, sambamba na maduka ya wastani na pia madogo.

Kila ukiingia maduka haya ya Marekani utawakuta watu wanasoma au kununua. Ila, kama ninavyosema tena na tena katika blogu mbali mbali, usitegemee kumkuta m-Tanzania katika maduka hayo. M-Tanzania huwa hasogei, utadhani vitabu ni mabomu yatamlipukia.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...